Papa anakutana na Zuncheddu,wa Sardegna alifungwa gerezani miaka 33 na kuachiliwa huru
Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 23 Agosti 2024 amekuta na mkutano wa falagha katika Maktaba ya Jumba la Kitume, na Beniamino Zuncheddu, mchungaji wa Sardegna nchini Italia ambaye alikaa gerezani kwa miaka 33 kwa tuhuma za mauaji ya mara tatu mnamo mwaka 1991 na kisha kuachiliwa huru mnamo Januari iliyopita.
Akiwa amekamatwa na umri wa miaka 26, Zuncheddu sasa ana miaka 60. Aliandika kitabu pamoja na wakili wake kiitwacho: “I am innocent” yaani “Mimi sina hatia”, ambacho alimpatia Papa Francisko asubuhi ya leo ambamo anasimulia tukio la kuhuzunisha aliloishi kwa muda mrefu.” Yeye amekuwa katika magereza tatu tofauti, wakati mwingine alishiriki chumba kidogo na watu kumi na moja, kwa shida kubwa hata kuoga na kulala tu. Uzoefu wa kinyama, alisema, lakini ni wakati ambao aliweza kusaidia wale ambao walikuwa na hali mbaya zaidi kuliko yeye. Alipata nguvu za kupinga kwa kumtumaini Mungu na kufikiria kuhusu familia yake. Zuncheddu aliwasamehe wale waliomsingizia kama muuaji wa watu wengi na kisha wakafuta shutuma hizo.