Kuabudu Ekaristi Takatifu Kuabudu Ekaristi Takatifu  

Ujumbe wa Papa kwa Kongamano la Ekaristi huko Antsiranana,Agosti 23-25,2024

Katika ujumbe kwa washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Ekaristi Takatifu huko Antsiranana-Madagacar kuanzia 23 hadi 25 Agosti 2024,Papa anatumaini tukio hilo litasaidia washiriki kukuza hisia za upendo na mshikamano kwa wote ,hasa kwa wale wenye matatizo.Kati ya wale waliokata tamaa katika siku zijazo,waache washuhudie huruma ya Mungu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu amewaomba wanachama wa “Harakati ya Ekaristi ya Vijana” inayoadhimisha miaka mia moja tangu ilipoanzishwa, kuwasaidia wengine kufanya maisha yao kuwa sadaka kwa Mungu inayojulikana, kupendwa na kuhudumiwa na kwamba wawe wamisionari wa upendo wa Kristo. Haya yamo katika Ujumbe wake  kwa wale wanaoshiriki katika Kongamano la Kitaifa la Ekaristi Takatifu nchini Madagascar  linalofanyika  huko Antsiranana kuanzia tarehe 23 hadi 25 Agosti 2024. Katika ujumbe uliotumwa kwa Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu  Marie Fabien Raharilamboniaina, Baba Mtakatifu alisisitiza kwamba mkutano huo  ni wenye lengo la kuwarejesha waamini katika mambo muhimu, na kuwasaidia kugundua tena maana ya kuabudu Ekaristi, hamu ya kukaa pamoja na Kristo, na kwa lengo la kuwafanya wakue kama Wakristo, huchukua thamani fulani wakati wa kujitayarisha kwa ajili ya hitimisho la Sinodi ya Kisinodi. Papa ameandika kuwa “liwasaidie kugundua tena umuhimu wa kukutana, kusali na kujitolea wenyewe na wengine katika nyayo za Yesu katika Ekaristi” na akikumbuka, kama alivyosema katika Ujumbe wa kamati ya maandalizi ya Kongamano la Kitaifa la Ekaristi la Marekani, tarehe 19 Juni 2023, kwamba “Ekaristi inatusukuma kuwa na upendo wa dhati kwa jirani yetu.”

Miaka mia moja ya Harakati ya Ekaristi ya Vijana

Zaidi ya hayo, katika mwaka huu  2024 ambapo maadhimisho ya miaka mia moja ya “Harakati ya Ekaristi ya Vijana” inaadhimishwa, Papa Fransisko ameakisi kwamba leo “imani katika uwepo halisi wa Bwana ni changamoto kubwa” na amewaalika washiriki kuwasaidia wengine “kupata uzoefu wa Yesu katika Ekaristi.”Baba Mtakatifu aidha ameandika kuwa “Kongamano liwasaidie pia kufanya maisha yenu kuwa sadaka kwa Mungu kwa kuunganishwa na ile ya Yesu juu ya madhabahu, ili aweze kujulikana zaidi, kupendwa na kutumikia.

Kukuza hisia za upendo na mshikamano kwa kila mtu

Katika matashi ya Baba Mtakatifu Fransisko kwa washiriki wa Kongamano la Ekaristi ni kwamba mkutano huo uweze kumsaidia kila mmoja “kukuza hisia za upendo na mshikamano kwa kila mtu, na hasa kwa wale walio katika magumu, ambao kwao njia ya maisha inakuwa ngumu zaidi na zaidi.”  Kwa walio wengi hasa watu waliokata tamaa wanaotazamia siku zijazo kwa mashaka na kukata tamaa, kana kwamba hakuna kitu kinachoweza kuwapa furaha, Papa, akinukuu Waraka Kitume wa Spes non confundit, yaani Msikate Tamaa ambao ulitanganza Jubilei ya 2025 na kutoa maelekezo amesema ni muhimu kuwa na tumaini kwa Bwana. “Kuweni mashuhuda wa huruma yake na upendo wake wa huruma” na kuhitimishwa kwa kuomba maombezi ya Bikira ili kila mtu"aweze kuimarisha kila siku uhusiano wake na Kristo.”

Papa atuma ujumbe kwa washiriki wa Kongamano la Ekaristi Kitaifa huko Madagascar
23 August 2024, 17:21