Papa Francisko,Mashariki ya Kati:kusitisha mapigano katika nyanja zote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi iliyonza tena mara baada ya mapumziko ya mwezi Julai, Jumatano tarehe 7 Agosti 2024 hakuweza kuficha wasiwasi wake kuhusu hali ya Mashariki ya Kati. Wakati hofu inaongezeka juu ya uwezekano wa shambulio la Iran kwa Israeli na mvutano na Lebanon ukiendelea, Papa Francisko kwa mara nyingine tena aliomba uhasama usitishwe. Haya yamesikika wakati akitoa salamu kwa lugha ya Kiitaliano kwa mahujaji waliokusanyika katika Ukumbi wa Paul VI mjini Vatican.
“Narudia wito wangu kwa pande zote zinazohusika ili mzozo usienee na kwamba moto ukome mara moja katika pande zote, kuanzia Gaza, ambapo hali ya kibinadamu ni mbaya sana na haiwezi kudumu.”
Upendo utawale
Matumaini ya Papa Francisko ni kwamba upendo unashinda na kwamba uhasama unatatuliwa kwa msamaha. “Ninaomba kwamba utafutaji wa dhati wa amani uzime mabishano, upendo ushinde chuki na kisasi kiondolewe kwa msamaha.”
Kuwe na amani katika Ukraine, Myanmar na Sudan
Baba Mtakatifu Francisko pia alionesha wasiwasi wake kwa Ukraine na kuwaalika waamini kuiombea nchi ya Ulaya Mashariki na mataifa yaliyo katika vita ambapo watu wanaendelea kuteseka na matatizo na maumivu makali.
“Ninawaomba muungane na katika maombi yangu kwa ajili ya Ukraine inayoteswa, Myanmar na Sudan. Wacha watu hawa, waliojaribiwa sana na vita wapate amani inayotamaniwa haraka iwezekanavyo.”
Kuondoa ubaguzi nchini Pakistan na Afghanistan
Hatimaye, Papa Francisko ambaye kabla ya Katekesi alikutana na uwakilishi kutoka chama cha Jumuiya ya Afghanistan nchini Italia aliomba, pia Pakistan na Afghanistan ambapo wengi bado wanabaguliwa.
“Tuunganishe juhudi na maombi yetu ili kuondoa ubaguzi wa kikabila katika mikoa ya Pakistan na Afghanistan, hasa ubaguzi dhidi ya wanawake.”