Papa Francisko:Wakristo wengine hawaenezi harufu ya Kristo bali dhambi!

Tunajua kwamba kwa bahati mbaya wakati mwingine Wakristo hawaenezi harufu ya Kristo,bali harufu mbaya ya dhambi zao wenyewe.Tusisahau kuwa dhambi hututenganisha na Yesu na hutufanya tutoe mafuta mabaya.Lakinia tutambue kila mmoja katika mazingira,wito huu adhimu wa kuwa harufu nzuri ya Kristo katika ulimwengu.Ni wito katika katekesi ya Papa tarehe 21 Agosti 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mada ya Roho na mchumba: Roho Mtakatifu anaongoza watu wa Mungu kukutana na Yesu Kristo, Tumaini letu, Jumatano tarehe 21 Agosti 2024 kwa waamini na mahujaji waliofika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, amejikita na sehemu ya 6 yenye mada: “Roho wa Bwana yu Juu yangu. Roho Mtakatifu katika Ubatizo wa Yesu. Papa aliongozwa na barua ya Mdo 10, 34.37-38 ambayo Petro alinena na kusema: “(…) Mnajua yaliyotukia katika Uyahudi wote, kuanzia Galilaya, baada ya ubatizo uliohubiriwa na Yohane; yaani, jinsi Mungu alivyomtia mafuta Yesu wa Nazareti kwa Roho Mtakatifu na nguvu.

Papa akiingia katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican
Papa akiingia katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko alianza kusema kuwa “Leo tunatafakari juu ya Roho Mtakatifu anayekuja kwa Yesu katika ubatizo wa Yordani na kutoka kwake kuenea ndani ya mwili wake ambao ni Kanisa. Katika Injili ya Marko tukio la ubatizo wa Yesu limefafanuliwa hivi: “Siku hizo Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa katika Yordani na Yohane. Mara alipotoka majini, aliona mbingu zimepasuka na Roho akishuka kama njiwa. Na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa nawe.” Ndivyo  Injili ya Marko inavyoeleza. Utatu wote ulikutana wakati huo kwenye ukingo wa Yordani! Kuna Baba anayejionesha kwa sauti yake; kuna Roho Mtakatifu anayemshukia Yesu kwa namna ya njiwa na kuna yule ambaye Baba anamtangaza kuwa ni Mwana wake mpendwa, Yesu,” Papa amesisitiza.

Papa akisalimia umati katika ukumbi wa Paulo VI
Papa akisalimia umati katika ukumbi wa Paulo VI

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu alisema kuwa: “Ni wakati muhimu sana wa msingi wa Ufunuo, ni wakati muhimu wa historia ya wokovu. Itatusaidia kusoma tena kifungu hiki kutoka katika Injili. Papa Francisko amesema lakini Ni nini kilitokea ambacho kilikuwa muhimu sana katika ubatizo wa Yesu hata Wainjili wote walizungumza juu yake? Tunapata jibu katika maneno ambayo Yesu alitamka, muda mfupi baadaye, katika sinagogi la Nazareti, akimaanisha waziwazi tukio la Yordani: “Roho wa Bwana yu juu yangu; kwa hiyo alinitia mafuta” (rej. Luka 4:18). Katika Yordani Mungu Baba “aliyetiwa mafuta na Roho Mtakatifu,” yaani, alimweka wakfu Yesu kuwa Mfalme, Nabii na Kuhani. Kwa hakika, katika Agano la Kale wafalme, manabii na makuhani walipakwa mafuta yenye manukato. Kwa habari ya Kristo, badala ya mafuta ya kimwili, kuna mafuta ya kiroho ambayo ni Roho Mtakatifu, badala ya ishara kuna ukweli: kuna Roho mwenyewe anayeshuka juu ya Yesu.”

Ishara ya Msalaba katika kuanza katekesi
Ishara ya Msalaba katika kuanza katekesi

Papa amesisitiza kuwa “Yesu alijazwa na Roho Mtakatifu tangu dakika ya kwanza ya Umwilisho wake. Hata hivyo, hiyo ilikuwa ni “neema ya kibinafsi”, isiyoweza kuambukizwa; sasa, hata hivyo, kwa upako huu, anapokea utimilifu wa karama ya Roho lakini kwa ajili ya utume wake ambao, kama kichwa, atawasiliana na mwili wake ambao ni Kanisa, na kwa kila mmoja wetu. Kwa sababu hiyo Kanisa ni “watu wa wapya wa  kifalme, watu wa kinabii, na watu wa kikuhani.” Neno la Kiebrania “Masiha” na neno la Kigiriki “Christós” yaani Kristo,” zote mbili zikirejea Yesu, humaanisha “mpakwa mafuta:” alipakwa mafuta ya shangwe, kutiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu. Jina letu lenyewe la “Wakristo” litafafanuliwa na Mababa kwa maana halisi: Wakristo maana yake ni “kupakwa mafuta kwa kumwiga Kristo”.

Ni Wakristo, waliotiwa mafuta kwa kumwiga Kristo, Papa amekazia kusema hilo. Kuna Zaburi katika Biblia inayozungumza juu ya mafuta yenye manukato, yaliyomiminwa juu ya kichwa cha kuhani mkuu Haruni na ambayo huteremka hadi upindo wa vazi lake (taz Zab 133:2). Picha hii ya kishairi ya mafuta yanayotiririka, inayotumiwa kuelezea furaha ya kuishi pamoja kama ndugu, imekuwa ukweli wa kiroho na ukweli wa fumbo ndani ya Kristo na Kanisani.  Kristo ndiye kichwa, Kuhani wetu Mkuu, Roho Mtakatifu ni mafuta yenye manukato na Kanisa ni mwili wa Kristo ambao ndani yake unaenezwa.

Papa akitoa tafakari yake 21 Agosti 2024
Papa akitoa tafakari yake 21 Agosti 2024

Tumeona kwa nini Roho Mtakatifu, katika Biblia, anafananishwa na upepo na, kwa hakika, alichukua jina lake kutoka kwake, Ruah  yaani upepo. Inafaa pia kujiuliza kwa nini inaoneshwa na mafuta, na ni mafunzo gani ya vitendo tunaweza kupata kutoka katika ishara hii. Katika Misa ya Alhamis Kuu, kuweka wakfu mafuta yaitwayo “Chrism,” Askofu, akimaanisha wale ambao watapata upako katika Ubatizo na Kipaimara, anasema hivi: “Upako huu uwapenye na kuwatakasa, ili wawe huru kutoka katika , uharibifu wa asili  na kuwekwa wakfu kama mahekalu ya utukufu wake, waeneze harufu ya maisha matakatifu.” Ni maombi ambayo yalianzia kwa Mtakatifu Paulo, ambaye aliwaandikia Wakorintho kuwa: “Kwa maana sisi ni harufu ya Kristo mbele za Mungu” (2 Kor 2:15).  

Kwa njia hiyo Upako unatupatia manukato, na hata mtu anayeishi upako wake kwa furaha analitia Kanisa manukato, kupaka jamii, kupaka familia kwa manukato haya ya kiroho. Baba Mtakatifu akiendelea kufafanua alisema kuwa “Tunajua kwamba, kwa bahati mbaya, wakati mwingine Wakristo hawaenezi harufu ya Kristo, lakini harufu mbaya ya dhambi zao wenyewe. Na tusisahau kamwe: dhambi hututenganisha na Yesu, dhambi hutufanya tutoe mafuta mabaya [inatufanya kuwa mafuta mabaya). Na shetani - msisahau hili - kwa kawaida,  huingilia kupitia mifuko – kuweni  waangalifu,” Papa ameonya. Na hili, hata hivyo, halipaswi kutuvuruga kutoka katika dhamira ya kutambua, kadiri tuwezavyo na kila mmoja katika mazingira yake, wito huu adhimu wa kuwa harufu nzuri ya Kristo katika ulimwengu. Harufu ya Kristo inaachiliwa kutoka katika  “matunda ya Roho”, ambayo ni “upendo, furaha, amani, uvumilivu, fadhili, uaminifu, upole, kiasi” (Gal 5:22).

Waamini katika Ukumbi wa Paulo VI
Waamini katika Ukumbi wa Paulo VI

Paulo alisema hivi, na ni vizuri jinsi gani kupata mtu ambaye ana fadhila hizo za: upendo, yaani mtu mwenye upendo, mtu mwenye furaha, mtu anayeunda amani,  na mtu mkarimu, wala sio mchoyo?; mtu mkarimu ambaye anakaribisha kila mtu, na mtu mzuri. Inapendeza kumpata mtu mwema, mwaminifu, mpole, asiye na kiburi,  lakini mpole...,” Papa ameshauri na kwamba: “ Tukijitahidi kukuza matunda haya, basi, bila sisi kutambua, mtu atanusa kidogo harufu nzuri inayotuzunguka ya Roho wa Kristo, tutkapowapata watu hawa.” Kwa kuhitimisha Papa amesema: Tuombe Roho Mtakatifu atufanye tuwe na upako wa ufahamu zaidi, upako wake.”

Katekesi ya Papa 21 Agosti 2024
21 August 2024, 15:32