Tafuta

2024.08.21 Papa Francisko amekumbuka Kumbukizi ya Mtakatifu Pio X Papa. 2024.08.21 Papa Francisko amekumbuka Kumbukizi ya Mtakatifu Pio X Papa.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko:makatekista kila mahali wawe mashuhuda jasiri!

Mara baada ya Katekesi katika salamu zake Papa alimkumbuka Mtakatifu Pio X,mwanzilishi wa katekisimu mashuhuri mwanzoni mwa karne ya XX na siku ambayo katika sehemu nyingi za ulimwengu zinafanya siku kuu ya Makatekista.Papa ameomba kutosahau Ukraine inayoteswa,Myanmar,Sudan Kusini,Kivu Kaskazini na nchi nyingi zilizo vitani.Tuombe amani na tusisahau Palestina na Israeli.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mara baada ya Tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 21 Agosti 2024, ametoa salamu mbali mbali kwa lugha tofauti. Papa Francisko akiwasalimu waamini wanaozungumza Kiarabu alisema“Roho Mtakatifu awe mwanzoni mwa kila shughuli, mkutano na tangazo. Analihuisha na kulifufua Kanisa. Bwana awabariki nyote na kuwalinda daima na mabaya yote! Papa Francisko hatimaye amewakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Hasa, kuwasalimi waamini wa Parokia za Mtakatifu Domenico huko Crotone, Mtakatifu Rocco huko Dolo na Bendi ya  Caprarola.

Papa akibariki wanandoa wapya
Papa akibariki wanandoa wapya

 

Katika kumbukizi ya Siku, Papa amesema “Leo, kumbukumbu ya Mtakatifu Pio X, na hivyo Siku ya Katekista inaadhimishwa katika sehemu nyingi za dunia. Hebu tuwafikirie makatekista wetu wanaofanya kazi nyingi sana na ambao, katika sehemu fulani za dunia, ni wa kwanza kuipeleka mbele imani. Leo tuwaombee makatekista, Bwana awatie moyo na waweze kusonga mbele. Hatimaye, mawazo yake yanawaendea vijana, wagonjwa, wazee na wenye ndoa za hivi  karibuni. Kwa mfano wa  Mtakatifu Pio amewatia moyo  kumfuata Kristo kwa kusikiliza Neno lake na kwa ushuhuda wa matendo mema. Na tafadhali, tusisahau Ukraine inayoteswa ambayo inateseka sana. Tusisahau Myanmar, Sudan Kusini, Kivu Kaskazini na nchi nyingi ambazo ziko vitani. Tuombe amani. Wala tusisahau Palestina na Israeli: Kuwe na amani huko. Baraka yangu kwenu nyote!”

Mkumbatio wa Baba anayependa waamini wake
Mkumbatio wa Baba anayependa waamini wake

Baba Mtakatifu kwa mahujaji wa Poland alisema “ Ulimwengu wetu, ulio na vita na migawanyiko, unahitaji matunda ya Roho Mtakatifu zaidi kuliko hapo awali. Kuanzia familia zenu na mazingira yenu ya kazi, melete upendo, amani na wema katika maisha yenu ya kila siku. Maombi yenu kwa ajili ya maombezi ya Mama Yetu wa Jasna Góra, ambaye wengi wenu mnafanya hija kwa miguu katika Majuma ya  hivi karibuni, aipatie dunia zawadi ya amani inayotamaniwa sana.” Kwa kuhitimisha Papa amewakabidhi kwa ulinzi wa mama Maria na ameibariki nchi yao.

Baba Mtakatifu akiwasalimia waamini wanaozungumza Kijerumani alisema “ Katika ubatizo huko  Yordani, Mungu, Baba wa mbinguni, alimfunua Yesu kuwa Mwana wake mpendwa. Kumrejesha Yesu Kristo katikati ya usikivu wa waamini wote pia ilikuwa hamu kubwa ya Mtakatifu Pio X, ambaye kumbukumbu yake tunaadhimisha leo. Kwa maombezi yake, Bwana awajalie daima kuonja ukaribu wake wa upendo! Na kwa wale wanaozungumza Kireno, Papa Francisko amewasalimia kwa moyo mkunjufu, kwa namna ya pekee mahujaji wa Parokia ya Mtakatifu Rita wa Cássia, ya Itumbiara. “Tukiwa tumetiwa mafuta na Roho Mtakatifu, zawadi isiyoelezeka kutoka kwa Mwenyezi, tunafanya upya ahadi yetu ya kimisionari kuleta harufu ya Kristo kwa ulimwengu wote. Mungu awabariki!”

Baraka ya Papa kwa Rosari mikononi mwa bi harusi
Baraka ya Papa kwa Rosari mikononi mwa bi harusi

 

Baba Mtakatifu Francisko aidha ametoa salamu za dhati kwa watu wanaozungumza Kifaransa, hasa kwa mahujaji wanaotoka katika parokia za Rives de la Bruche, Ufaransa, na kwa wale kutoka Burkina Faso na Jimbo la  Abidjan. “Katika kipindi hiki cha likizo, tuombe neema ya Roho Mtakatifu ienee, kadiri tuwezavyo na kila mmoja katika mazingira yake, harufu nzuri ya Kristo katika maisha ya kaka na dada zetu. Mungu awabariki!” Papa Francisko aidha aliwakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wote wanaozungumza Kiingereza waliokuwapo kwenye katekesi hiyo huku akiwatakia wote na familia zao,  furaha na amani ya Bwana wetu  Yesu Kristo. Mungu awabariki! Amehitimisha kwa kusali sala ya Baba Yetu… na baadaye ilifuatia kusalimiana kwa baadhi ya mahujaji waliofika.

Baada ya Katekesi 21 Agosti 2024
21 August 2024, 15:30