Papa:Kifo cha Wenyeheri mashahidi DRC kitie moyo njia za upatanisho na amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara bada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 18 Agosti 2024, Baba Mtakatifu Francisko amekumbuka tukio la kutangazwa wenyeheri wapya katika nchi ya Afrika. Papa amesema: “Huko Uvira katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Luigi Carrara, Giovanni Didoné na Vittorio Faccin, wamisionari Waxaveri wa Kiitaliano, leo hii walitangazwa kuwa wenyeheri, pamoja na Albert Joubert, Padre wa Congo, waliouawa katika nchi hiyo mnamo 28 Novemba 1964. Kifo chao cha kishahidi kilikuwa kilele cha maisha yaliyotumiwa kwa ajili ya Bwana na kwa ajili ya ndugu zao. Mfano wao na maombezi yao yatie moyo njia za upatanisho na amani kwa manufaa ya watu wa Congo. Tuwapigie makofi Wenyeheri wapya!
Papa akiendelea kutazama hali halisi ya ulimwengu wa vurugu kama kawaida yake amesema: “Na tunaendelea kuomba kwamba njia za amani ziweze kufunguliwa katika Mashariki ya Kati - Palestina, Israel - na vile vile katika Ukraine inayoteswa, Myanmar na katika kila eneo la vita, kwa kujitolea kwa mazungumzo na majadiliano na kujiepusha na kujibu kwa vitendo vya vurugu.
Papa amewaasalimia waamini wote kutoka Roma na mahujaji waliotoka Italia na nchi mbalimbali. “Hasa ninawasalimu wale wanaotoka Jimbo la Mtakatifu Paulo nchini Brazili; na pia Masista wa Mtakatifu Elizabeth. Papa aidha amesema: “Ninatuma salamu zangu na baraka zangu kwa wanawake na wasichana waliokusanyika katika Madhabahu ya Maria wa Piekary Šląskie huko Poland, na ninawatia moyo kushuhudia Injili kwa furaha katika familia na katika jamii.”
Papa aidha amewasalimu watoto wa Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria kutoka Roma. Hatimaye amewatakia Dominika njema, huku akiwaomba wasisahau kumuombe. Mlo mwema, mchana mwema na kwaheri ya kuonana.