Papa kwa Shirika la Knights Of Columbus:Salini kwa ajili ya haki na amani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika nyakati hizi zenye vita vipya, migogoro na machafuko ya kijamii, tuombee haki, amani na upatanisho katika familia yetu ya kibinadamu. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko ambayo kwa mara nyingine tena ametoa msisitizo bila kuchoka kwa wakristo wote. Amefanya hivyo kupitia ujumbe wake uliotiwa saini na Kardinali, Pietro Parolin, Katibu wa Vatican kwa Patrick E. Kelly, Mkuu wa Shirika la Kijeshi la Knights of Columbus, wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wao wa 142 katika Jiji la Quebec nchini canada kuanzia tarehe 6 hadi 8 Agosti 2024. Katika ujumbe huo, tunasoma kwamba Baba Mtakatifu “anatoa shukrani kwa ajili ya jitihada za Shirika hilo la Knights katika kutunza mahitaji ya kaka na dada zetu wa Ukraine iliyoharibiwa na vita; ya Jumuiya za Kikristo za Mashariki ya Kati na wale wote wanaoteseka kwa ajili ya imani yao katika Kristo. Ni sababu ambazo ziko karibu sana na moyo wake kama Mchungaji wa Kanisa la Ulimwengu.”
Shirika linatoa misaada na kutetea zawadi ya uhai
“Pamoja na shughuli za upendo Halmashauri zake mahalia ulimwenguni kote, Shirika lao, linaendelea kutoa msaada wa kipekee na kutia moyo juhudi za kutetea zawadi ya Mungu ya uhai katika kila hatua ya maendeleo yake, kutunza heshima ya taasisi ya ndoa na ili kuendeleza utume wa Kanisa katika nchi zinazoendelea”. Katika maandishi hayo ya Baba Mtakatifu yanalenga hasa mada ya tukio, On Mission, "iliyolenga mwelekeo wa kimisionari wa ufuasi wa Kikristo ambao Baba Mtakatifu amekuwa akisisitiza tangu siku za kwanza za upapa wake katika Waraka wake wa Evangelii Gaudium yaani Injili ya Furaha ambapo ametaja kuwa: “Kila Mkristo ni mmisionari kwa kiwango ambacho amekutana na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu”. Kwa hakika, “haja ya dharura ya kushuhudia upendo huo, hasa katika huduma kwa maskini na katika ari ya kitume kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa katika umoja, udugu na uaminifu wa ukweli wa Injili unaookoa na ambao ni msingi wa Shirika la Knights of Columbus. Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake uliotiwa saini na Katibu wa Vatican, anasisitiza kuwa: “Katika kutekeleza malengo haya mashuhuri, ya Shirika hili tangu asili yake, limezingatia sana malezi ya washiriki wake kama watu wa imani na familia."
Familia na vijana
Kwa vizazi vingi, Shirika hili limefanya kazi ya kuimarisha maisha ya familia kupitia programu za katekesi na ukuaji wa kiroho, wameshuhudia hadharani umuhimu wa familia kama kiini cha msingi cha jamii na wameunga mkono msururu wa mipango ya kusaidia familia katika jamii zao muhimu na dhamira ya elimu.” Aidha ahadi hii ya kihistoria imejumuisha mahangaiko maalum la kueneza imani kwa vizazi vipya, kusisitiza maadili yenye afya na kusindikiza vijana wanapokua kuelekea ukomavu kama wanaume na wanawake wenye uadilifu, hekima na huduma kwa jamii wanamoishi. Hawa ni vijana wale wale ambao Papa Francisko katika hotuba na maandishi yake alionya juu ya hatari, katika jamii ya kisasa na mara nyingi isiyo na maana, ya kujitenga na mizizi ya kidini na kiutamaduni ambayo hutoa utambulisho wao wa ndani zaidi. Kwa sababu hiyo, Papa Francisko amewatia moyo hasa juu ya mpango wa Cor dei Cavalieri yaani Moyo wa kishujaa
Hija ya Ekaristi huko Marekani
Ujumbe huo pia unakumbusha juu ya hija ya Ekaristi huko Marekani, iliyohamasishwa na Shirika hilo, ambayo ilitoa ushuhuda wa kuvutia, na sio tu kwa imani ya Kanisa katika nguvu ya ukombozi wa sadaka ya Kristo msalabani, bali pia kwa ajili ya ufuatiliaji wake wa daima wa Kanisa katika Hija yake kupitia historia. Na kwa Shirika hilo na Familia zao, Baba Mtakatifu Francisko amewaomba waendelee kutoa sala na Misa kwa ajili ya “Ushindi wa amani ya Kristo katika mioyo ya waamini wote na kwa ajili ya ujenzi wa ustaarabu wa upendo.
Matazamio ya Mahujaji kupitia mlango Mtakatifu
Kwa kuhitimishwa katika ujumbe wake huku akizingatia maandalizi ya Jubilei ijayo, Baba Mtakatifu, amewafikiria mahujaji wasiohesabika watakaopitia kwenye Mlango Mtakatifu waKanisa kuu la Mtakatifu Petro, na kueleza matumaini kwamba "kwa kutafakari juu ya dari kubwa la Bernini linalofunika Kaburi la Mtakatifu Petro, ambalo shukrani kwa ukarimu wa Shirika la Knights of Columbus, limerudishwa katika uzuri wake wa asili waweze kuimarishwa na kutiwa ngumu ya imani umoja na Mrithi wa Petro".