Sikukuu ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka Sikukuu ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka  

Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Ukuu Na Utukufu wa Fumbo la Umwilisho

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Sikukuu ya Kung’ara Bwana tarehe 6 Agosti 2024 anawaalika waamini akisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17:5. Siri ya maisha inasimikwa katika utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa. Chukua Injili, soma na sikiliza kile ambacho Kristo Yesu anataka kukuambia katika roho yako, kwa sababu Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka na tukio hili linaadhimishwa tarehe 6 Agosti ya kila mwaka. Kristo Yesu akiwa ameambatana na Mitum wakee: Petro, Yakobo na Yohane akapanda nao mlimami kusali. Akiwa anasali sura yake ikageuka, ikang’ara na mavazi yake yakawa meupe wanatokea Musa na Eliya. Hawa ni watu muhimu sana katika historia ya wayahudi. Musa ndiye anayewakilisha Torati, yaani sheria na taratibu zinazoongoza maisha yote ya Wayahudi. Eliya yeye anawakilisha Manabii. Zaidi ya hapo uwepo wa pamoja Musa na Eliya, yaani Torati na Manabii, katika lugha ya kibiblia maana yake ni ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Torati na Manabii ni neno lililotumika kumaanisha Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale. Mwisho wa tukio hilo ni kwamba linashuka wingu na ndani ya wingu hilo inasikika sauti ikisema: “Huyu ni mwanangu mpendwa msikieni Yeye.” Wingu na sauti hii ni ile ile iliyosikika siku ya ubatizo wa Yesu. Wingu ni alama ya uwepo wa Mungu kumbe sauti hiyo inayosikika inaonekana moja kwa moja kuwa ni ushuhuda wa sauti ya Mungu: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.” Mk 9:7: Haya pia ni maandalizi ya ufunuo wa Siku ya Mwisho, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda
Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda

Tukio hili linaonesha mabadiliko ambayo Kristo Yesu aliyapata daima alipokuwa akisali na kuzungumza na Baba yake wa mbinguni.  Linaonesha utukufu wa Mungu ambao daima ulifichika katika ubinadamu wake na linaonesha utukufu ambao Yesu na wote wanaomwamini wataupata baada ya adha ya Msalaba na mahangaiko ya maisha ya duniani; linaonesha Yesu kama utimilifu wa Torati na Manabii na linaagiza kumsikiliza yeye, yaani kulipokea Neno lake na kuliishi kama wafuasi wake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Sikukuu ya Kung’ara Bwana tarehe 6 Agosti 2024 anawaalika waamini akisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17:5. Siri ya maisha inasimikwa katika utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa. Chukua Injili, soma na sikiliza kile ambacho Kristo Yesu anataka kukuambia katika roho yako, kwa sababu Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.  #TransfigurationOfTheLord.

Mtakatifu Paulo VI Alifariki dunia tarehe 6.8.1978
Mtakatifu Paulo VI Alifariki dunia tarehe 6.8.1978

Baba Mtakatifu Benedikto XVI, akifanya tafakari kuhusu Sikukuu ya Kung’ara Bwana anasema kwamba, huu ni muhtasari wa Mafumbo ya Imani ya Kanisa, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya Kristo Yesu na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene. Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele!

Papa Benedikto XVI: Sikukuu ya Kung'ara: Muhtasari wa Imani ya Kanisa
Papa Benedikto XVI: Sikukuu ya Kung'ara: Muhtasari wa Imani ya Kanisa

Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo. Baba Mtakatifu Benedikto anakaza kusema, huu ni mchakato wa toba na wongofu wa ndani, unaopania kumsafisha na kumtakasa mwamini katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili siku moja aweze kuufikia utukufu wa maisha na uzima wa milele. Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu.”

Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda
Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda

Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kung’ara Bwana, Kanisa kwa mwaka huu, 2024, linafanya kumbukizi ya miaka 46 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mtakatifu Paulo VI anasema, Sikukuu ya Kung’ara kwa Kristo Yesu inaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe yaani Petro, Yakobo na Yohane ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya Nafsi yake. Rej Mt 17:2. Tukio hili linautukuza ubinadamu wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Hapa Yesu anadhihirisha utukufu wa Fumbo la Pasaka, kielelezo makini cha sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kustahilishwa kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Mwili uliotukuka mbele ya Mitume wa Kristo Yesu ni mwili wa Kristo na kwamba, hata mwili wa binadamu utapata urithi wa mwanga wa uzima wa milele, kwa kushiriki katika utukufu na kwa njia hii wapate kushiriki tabia ya Uungu kwa kuokolewa na uharibifu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa.

Utukufu wa Kristo Umetundikwa juu ya Mlasaba
Utukufu wa Kristo Umetundikwa juu ya Mlasaba

Hii ni sehemu ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, iliyokuwa imeandaliwa na Mtakatifu Paulo VI kwa ajili ya Sikukuu ya Kung’ara kwa Yesu, tarehe 6 Agosti 1978, lakini kutokana na homa kali iliyomshika siku hiyo, hakuweza kutokeza mbele ya waamini na matokeo yake, jioni akafariki dunia katika amani ya Baba wa milele! Mtakatifu Paulo VI anakaza kusema, waamini wanasubiri kushirikishwa utukufu wa Mungu ambao walianza kuutafuta kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mtakatifu Paulo VI katika tafakari yake, aliwakumbuka hata wale ambao kutokana na sababu mbalimbali walikuwa wanateseka, ili nao, hata katika hali na mazingira kama haya, waweze kupata walau mwanya wa mapumziko. Hawa ndio wale watu wasiokuwa na fursa za ajira, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu katika familia na jamii katika ujumla wake. Ni watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia pamoja na wale wote walioathirika kutokana na sera na mikakati tenge ya uchumi na maendeleo jamii. Kutokana na mahitaji msingi ya umati wote huu, Kanisa linapenda kumtolea Bikira Maria sala na maombi yake, ili aweze kusaidia kuombea umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Kung'ara Bwana
06 August 2024, 14:01