Skauti Mtangazeni na Kumshuhudia Kristo Yesu Katika Jamii Yenu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba vyama vya kitume ndani ya Kanisa Katoliki vina nafasi ya pekee kabisa katika maisha yake kwani huu ni utajiri wa Kanisa ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji katika medani mbalimbali za maisha. Chama cha Skauti nchini Italia, kinaweza kuwa ni chachu ya Uinjilishaji kwa kudumisha madaraja ya majadiliano na jamii. Dhamana hii inaweza kutekelezeka ikiwa kama Skauti itaendelea kushikamana na Parokia zao pamoja na kushiriki kikamilifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa mahalia, kwa kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali. Wazazi wanawaamini walezi wa Chama cha Skauti kwa sababu wanatambua wema na hekima ya malezi ya kiskauti yanayojikita katika tunu msingi za maisha ya binadamu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maisha ya kiroho na imani kwa Mwenyezi Mungu.
Hizi ni mbinu zinazowafunda Maskauti kuwa kweli huru na kuwajibika barabara katika matendo yao; imani hii ya wazazi inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote, bila kulisahau Kanisa na kwamba, daima wanapaswa kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Jumuiya kubwa ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha kwamba, wanaongozwa na “Katiba ya Ujasiri” kielelezo cha mambo msingi wanayokumbatia na matarajio yaliyomo mioyoni mwao. Haya ni masuala ya elimu, usikivu makini unaopaswa kuoneshwa na viongozi wao, bila kusahau mchango wa Parokia na Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Muasisi wa Chama cha Skauti Bwana Baden Powell anakiri kwamba, dini ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya wanachama wa Skauti kwani ni sehemu ya utambulisho wa maisha yao, kwa kutambua na kuthamini uwepo wa Mungu na huduma. Hiki ni chama ambacho kinaendelea kuwekeza zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanachama wake wanapewa malezi ya imani; mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, kwa ajili ya mafao na ustawi wa wanachama wa Chama cha Skauti.
Ni wakati wa Njia ya Kitaifa ya Viongozi wa Jumuiya ya AGESCI, ambayo katika kipindi cha miaka 50 ya maisha na utume wake, imeinuia vizazi vya watu wanaostahili kutumainiwa kwa sababu wana uwezo wa kufanya wawezavyo kwa kuuacha ulimwengu ulio bora zaidi kuliko walivyoupata, wakitafuta furaha yao wenyewe na kuwashirikisha wengine. Kwa kutekeleza haya kila siku, wanajenga utamaduni wa kusikiliza, kutembea, kutazama, kushiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, pamoja na kushiriki Neno la Uzima na kwamba, tofauti zao ni tunu msingi ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni muda wa kuboresha rasimali muda ili kupata nguvu mpya, maneno mapya, maudhui na elimu mpya, zawadi makini kwa viongozi wa Kitaifa. Ni wakati wa kugundua tena sababu za kuchagua kuwa waelimishaji katika ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya; ni wakati ambao mizizi inapaswa kuamini maua na matunda yatatolewa kwa wingi. Viongozi wa Jumuiya ya AGESCI, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Agosti 2024 wamekuwa wakifanya mkutano wao, ulioongozwa na kauli mbiu “Kizazi cha furaha, Jumuiya ya Wakuu wa AGESCI, RN24, huko Verona, Kaskazini mwa Italia.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya AGESCI, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa matashi mema, kupitia kwa Don Andrea Turchini, Mshauri mkuu msaidizi wa Chama cha Viongozi na Skauti cha Italia. Anasema, huu ni wakati wa kuchota imani kutoka kwa Kristo Yesu, Mwalimu na Rafiki, ili kuendelea na safari ya furaha, utu na maisha ya kiroho ndani ya Kanisa, huku wakitangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika jamii. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu viongozi hawa katika malezi na makuzi ya Skauti vijana, wanaopaswa kusindikizwa kwa hekima, busara na utu wema. Mambo haya yanahitaji majiundo makini na yaliyo bora zaidi kwa wale ambao wameitwa na kutumwa kutekeleza utume huu nyeti ndani ya jamii; wajenge utamaduni wa kusikiliza, wawe ni watu watulivu hali ambayo inawezesha kuzaa matunda ya uinjilishaji mpya. Viongozi hawana budi kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kujadiliana na kusali; daima wakijifunza sanaa ya kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kukuza na kudumisha Injili ya upendo, kama anavyofundisha Kristo Yesu. Maandiko Matakatifu yanawafundisha waamini jinsi ambavyo Kristo Yesu aliweza kujipambanua kwa uwepo na kutokuwepo kwake; alitambua muda wa kusahihisha, kusindikiza, kutuma, ili hatimaye, Mitume wake, waweze kupambana na changamoto za umisionari. Ndivyo Kristo Yesu alivyofanya kwa Petro, Andrea, Yakobo na Yohane, alipogeuka sura yake mbele yao. Viongozi watambue dhamana na wajibu wao katika malezi ya Skauti vijana. Walezi wanafundisha kwa njia ya maisha yao adili na manyoofu, kuliko hata maneno yao.
Maisha ya mlezi, kwa msaada wa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, lazima yakue na kuelekea ukomavu kiutu na kiroho kama Mitume wa Kristo Yesu. Haya ni mambo msingi katika huduma kwa vijana wa kizazi kipya. Ushuhuda wa maisha, maneno na matendo yao katika majadiliano na usindikizaji wa vijana wa kizazi kipya ni muhimu sana katika malezi. Baba Mtakatifu anawapongeza wanachama wa Chama cha Skauti nchini Italia, nguzu msingi katika maisha ya Kikristo sanjari na ujenzi wa ushirika katika udugu wa kibinadamu; shule ya huduma kwa jirani lakini hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kamwe wasiruhusu kudhohofishwa na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali za maisha, bali daima wawe njiani kutafuta na kutekeleza mpango wa Mungu alio nao kwa kila mmoja wao. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka viongozi hawa wote, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu George.