Kauli mbiu “Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang'anywa.” Lk 10:42. Kauli mbiu “Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang'anywa.” Lk 10:42.  

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Kwa Siku ya 35 ya Vijana Kimataifa Huko Medjugorje: 2024

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 35 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, anakazia utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Vijana waimarishe uelewa wa Neno la Mungu kwa njia ya Sakramenti na kwamba, vijana wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Maria alikaa kimya, huku akimsikiliza Kristo Yesu. Neno la Mungu na Sakramenti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia, kuna maanisha ujenzi wa mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tafakari ya Neno la Mungu ndani ya familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, umeliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira, mwongozo na mwanga katika mapito ya maisha yao. Ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye maisha ya mtu binafsi, familia, jumuiya ndogondogo za Kikristo na kwenye vyama vya kitume. Tafakari makini ya Neno la Mungu inaweza kuwapatia mwanga wa imani, matumaini na mapendo wanafamilia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kuna uhusiano wa pekee kati ya Neno la Mungu, Kanisa na maisha ya Ndoa na Familia, ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanandoa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa kuwalea watoto wao kadiri ya imani na mafundisho ya Kanisa, kwani wao kimsingi ni watangazaji wa kwanza wa Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili, matakatifu na ukarimu.

Kauli MBiu: Mariam amelichagua fungu llililo jema: Lk 10:41
Kauli MBiu: Mariam amelichagua fungu llililo jema: Lk 10:41

Kimsingi Kanisa linapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, lakini wakati mwingine, tunu hizi zinakosekana na ushuhuda wa Kanisa unatoweka kama ndoto ya mchana! Ushuhuda mkubwa uliotolewa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake ni ukaribu wake kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Watu hawa akawarejeshea tena utu na heshima yao; akawakirimia mahitaji yao msingi; akawaponya magonjwa na hatimaye, akawaondolea dhambi zao. Mwinjili Luka anamwonesha Kristo Yesu akiwa ndani ya familia ya Martha, Maria na Lazaro. Maria aliketi miguuni pake Yesu akasikiliza maneno yake, lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi, kiasi cha kumwendea Yesu na kumtaka amwambie Maria aende kumsaidia kazi jikoni kama ushuhuda wa ukarimu. Lakini, Yesu akamjibu na kumwambia: “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang'anywa.” Lk 10:41-42. Ni katika muktadha huu wa usikivu makini wa Neno la Mungu pamoja na fadhila ya ukarimu inayomwilishwa katika matendo mema, ndicho kiini cha Maadhimisho ya Siku ya 35 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosto 2024, Sherehe ya Kung’ara Bwana, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang'anywa.” Lk 10:42.

Umati wa vijana ukisherehekea Ibada ya Misa Takatifu
Umati wa vijana ukisherehekea Ibada ya Misa Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 35 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, anakazia utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Vijana waimarishe uelewa wa Neno la Mungu kwa njia ya Sakramenti na kwamba, vijana wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Maria alikaa kimya, huku akimsikiliza Kristo Yesu. Bikira Maria ni mwanafunzi mwingine wa Kristo Yesu aliyekuwa na ujasiri wa kufuata Njia ya Msalaba hata kudiriki kusimama chini ya Msalaba wakati wa mateso na kifo cha Kristo Yesu pale Mlimani Kalvari, akasindikizana na Mitume wa Yesu, siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Bikira Maria anawaonesha waamini njia ya kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yao. Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye kumwilisha Neno la Mungu, vijana watakuwa na fursa ya kumfahamu zaidi Kristo Yesu, Mpatanishi na Utimilifu wa Ufunuo wote “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu.” Ebr 1:1-3. Kutofahamu Maandiko Matakatifu anasema Mtakatifu Jerome ni kutokumfahamu Kristo Yesu. Vijana watambue kwamba, wanayo dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waimarishe ujuzi na utambuzi wa Neno la Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Wajenge na kukuza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kama njia ya kuweza kukutana na uso kwa uso na Kristo Yesu.

Muhimu: Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti
Muhimu: Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti

Mtume mwaminifu na mwenye busara anapaswa kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika familia, maeneo ya masomo, kazi na katika zile za “utawala binafsi.” Baba Mtakatifu anawataka vijana kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, kielelezo cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu. Wajikite katika tunu msingi za Kiinjili, ili kweli waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu; wajenzi wa ubinadamu mpya. Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ni ishara ya matumaini juu ya bahari ya dunia iliyochafuka kwa mawimbi mazito mazito, atawasaidia na kuwaongoza kuelekea kwenye bandari salama, amani na utulivu wa ndani. Katika kipindi hiki cha likizo ya kiangazi, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kuwa karibu na Kristo Yesu katika: Sala, Neno, Sakramenti na kwa njia ya huduma makini kwa jirani, kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Wajiweke karibu zaidi na Kristo Yesu, ili apate kuwapumzisha. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu amewakabidhi vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kwa maombezi yake, vijana waweze kujitwika nira ya upendo, upole na unyenyekevu wa Kristo Yesu na kuanza kumfuasa. Kwa kukutana na vijana wengine, wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani. Itakumbukwa kwamba, Padre Slavko Barbarić (11 Machi 1946 – 24 Novemba 2000) ndiye muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina.

Siku ya Vijana 2024
03 August 2024, 15:34