Umuhimu wa Liturujia Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika Liturujia kwa kutambua nafasi ya Liturujia katika Fumbo la Kanisa, kwani Liturujia ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa, kimsingi lina asili mbili ile ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na kibinadamu kwa sababu linawaambata binadamu. Hivyo Liturujia ya kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe Hekalu la Roho Mtakatifu, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo. Liturujia inaimarisha nguvu za waamini katika mchakato wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kielelezo cha imani tendaji. Lengo ni kujenga na kudumisha: umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini. Ni Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliotambua na kuthamini umuhimu wa kutafsiri vitabu vya Liturujia ili Ibada mbalimbali ziweze kufahamika na wengi: kwa kukazia ukamilifu na ufahamu wa Ibada inayoadhimishwa. Liturujia irekebishwe kulingana na hali za watu na Mapokeo yao, kwa maneno mengine, huu ulikuwa ni mwanzo wa jitihada za utamadunisho wa Liturujia katika uhalisia wa maisha ya waamini sehemu mbalimbali za dunia. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji!
Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza ambayo mwamini anaweza kuchota roho ya kweli ya kikristo. Ni katika muktadha wa majiundo ya Kiliturujia, Jimbo kuu la Modena-Nonantola ndilo mwenyeji wa Maadhimisho ya Juma la 74 la Liturujia Kitaifa nchini Italia lililofunguliwa kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 29 Agosti 2024 huko Modena, Kaskazini mwa Italia. Juma hili linanogeshwa na kauli mbiu “Liturujia Sala ya Kweli ya Kanisa la Watu wa Mungu na kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa ya daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.” Rej. Ebr 13:15. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Claudio Maniago wa Jimbo kuu la Catanzaro-Squillace ambaye pia ni Rais wa Tume ya Liturujia, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, anakazia umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, Sala ya Liturujia, Muziki Mtakatifu ndani ya Liturujia, ukimya unaoelimisha wakati wa Liturujia na hatimaye, ni fumbo la Liturujia linalofumbatwa katika ushirika na Kristo Yesu, Ushiriki mkamilifu katika Liturujia pamoja na utume. Kauli mbiu “Liturujia Sala ya Kweli ya Kanisa la Watu wa Mungu na kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa ya daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.” Rej. Ebr 13:15 inagusa umuhimu wa sala na Liturujia kwani Liturujia ni pia ushirika katika Sala ya Kristo Yesu inayoelekezwa kwa Baba katika Roho Mtakatifu. Ndani yake kila sala ya Kikristo hupata chemchemi yake na kikomo chake. Huu ndio ushirikishwaji unaofanywa na Mama Kanisa anayewawezesha waamini kujisikia kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya waamini Mitume wa mahali na nyakati zote. Rej. KKK 1073.
Hii ni shule ya ushirika unaoondoa tabia ya kutojali; kwa kuwaweka watu karibu na Kristo Yesu ambaye ni Mwalimu anayewaunda sanjari na kuwaelimisha katika Kanisa pamoja na hali nzuri ya Habari Njema ya Wokovu. Huu ni ufunuo wa utimilifu wa ukweli katika sala, ukweli unaomwilishwa kwa njia ya sala na kuwafikia waamini wote. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anajitahidi kutoka katika ubinafsi na uchoyo wote akiwa tayari kujenga ushirika wa watu wa Mungu ndani ya Kanisa katika sala. Baba Mtakatifu anakazia majiundo makini katika matendo ya Kiliturujia, watu wa Mungu wanapokutana katika sala: namna ya kusimama, kukaa na kupiga magoti; ukimya na ushiriki; matumizi bora ya njia za fahamu; zote hizi ni njia za mwamini kushiriki kikamilifu katika Ibada; kila mwamini anapaswa kugundua upekee wake na kwamba, wote kwa pamoja wanaunda mwili mmoja. Liturujia kama sala ya kweli ya Kanisa anakazia matumizi sahihi ya lugha asilia na sauti hizi zinapoungana zinatengeneza kwaya, huku waamini wakiwa wameungana pamoja. Huu ndio ukweli unaojionesha katika Sala ya Kanisa, inayopaswa kuhamasishwa kwa waamini, ili iwe ni Sala ya watu wa Mungu. Sala ya Zaburi, inawasaidia waamini kumwilisha Liturujia katika maisha; kwa kukazia tunu msingi za umoja na ushirika. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mapokeo ya kimuziki ya Kanisa lote ni hazina yenye thamani isiyopimika, inayozidi aina nyingine ya sanaa, kwa sababu kuimba kutakatifu, kukiunganika na maneno, ni sehemu ya lazima na ya ndani ya Liturujia ya sherehe. Muziki mtakatifu unapounganika na tendo la Liturujia linanogesha sala na kuonesha umoja wa mioyo na kuleta heshima katika maadhimisho. Hiki ni kielelezo cha utukufu wa Mungu na kutakatifuzwa kwa waamini na huu ni ufunuo wa Ibada inayoadhimishwa. Rej. Sacrosanctum concilium, 112.
Mtakatifu Paulo VI anasema, waamini wanapoimba wanashiriki kulijenga Kanisa, wanatunza imani na maisha ya Kikristo. Kumbe, kuna haja ya kuwa na maandalizi kamambe ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kila Dominika na kwamba, nyimbo nzuri ni kielelezo cha furaha na ushuhuda wa Jumuiya ya waamini, wanaoadhimisha na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Juma la 74 la Liturujia Kitaifa nchini Italia, anakazia umuhimu wa ukimya katika Ibada ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha mshikamano na mafungamano na upendo wa Kristo Yesu; ni fursa ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kutafakari na hivyo kulipatia Neno la Mungu nafasi ya kuzama katika akili na nyoyo za waamini. Hii ni nafasi muhimu kwa sala, ili kutoa fursa kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaletea mabadiliko na hatimaye, kumsikiliza Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao. Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Fumbo la Liturujia linalofumbatwa katika ushirika na Kristo Yesu, Ushiriki mkamilifu katika Liturujia pamoja na utume, kielelezo makini cha ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Liturujia inahitaji majiundo endelevu ili kujenga na kudumisha huduma katika ushirika.