Tafuta

Jumuiya kutoka Seminari kuu ya “Mama yetu wa Mitume" wa Getafe, iliyoko nchini Hispania, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Jumamosi tarehe 3 Agosti 2024 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Jumuiya kutoka Seminari kuu ya “Mama yetu wa Mitume" wa Getafe, iliyoko nchini Hispania, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Jumamosi tarehe 3 Agosti 2024 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Umuhimu wa Malezi na Majiundo Makini ya Mapadre Katika Wito na Maisha Yao

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu: Ukomavu na ukarimu, kama njia ya kujibu wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watu kwa makini; Kusamehe na kusahau; Kipaumbele cha kwanza kikiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni mwaliko kwa Majandokasisi kufanya tafakari ya kina kuhusu wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee. Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni: Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Majiundo awali na endelevu ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa
Majiundo awali na endelevu ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kuliwezesha Kanisa kuwapata Mapadre: wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha wa malezi, majiundo na makuzi ya wito, maisha na utume wa Mapadre, Jumuiya kutoka Seminari kuu ya “Nuestra Señora de los Apóstoles di Getafe” yaani: “Mama yetu wa Mitume" wa Getafe, iliyoko nchini Hispania, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Jumamosi tarehe 3 Agosti 2024 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Seminari ya Mama Yetu wa Mitume inaadhimisha miaka 30 ya uwepo wake
Seminari ya Mama Yetu wa Mitume inaadhimisha miaka 30 ya uwepo wake

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu: Ukomavu na ukarimu, kama njia ya kujibu wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watu kwa makini; Kusamehe na kusahau; Kipaumbele cha kwanza kikiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni mwaliko kwa Majandokasisi kufanya tafakari ya kina kuhusu wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli.

Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu
Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Kumbe, hija hii ya Jumuiya kutoka Seminari kuu ya “Nuestra Señora de los Apóstoles di Getafe” yaani: “Mama yetu wa Mitume" wa Getafe ni muda muafaka wa kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2024 ameadhimisha kumbukumbu ya Miaka 165 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, mfano bora wa kuigwa na mapadre wote duniani katika wema, upendo, ukarimu, sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Maria Vianney alikuwa akisema, urithi mkubwa kutoka kwa Mapadre baada ya kifo chao hapa duniani ni ushuhuda wa upendo kama alivyofanya katika maisha na utume wa Kipadre. Baba Mtakatifu amewakumbusha Majandokasisi kwamba, wameitwa na kuitikia upendo wa Mungu, na kwa njia ya msaada wa malezi na majiundo, iko siku wataweza kupokea zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre.

Kristo Yesu ni Mlango wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mlango wa uzima wa milele

Kumbe, dira na mwongozo wao ni kujitahidi kumfuasa na kumwiga Kristo Yesu, Mchungaji mwema, katika shida na magumu ya maisha yao. Mambo msingi wanayopaswa kuzingatia ni: Maisha ya kiroho, Masomo, Maisha ya Kijumuiya pamoja na Shughuli za kichungaji; mambo wanayopaswa kuyatekelezwa kwa kuzingatia uwiano mzuri, kwani Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake, linataka kuona: Ukomavu na ukarimu, kama njia ya kujibu wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watu kwa makini; Kusamehe na kusahau; Kipaumbele cha kwanza kikiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Seminari kuu ya “Nuestra Señora de los Apóstoles di Getafe” yaani: “Mama yetu wa Mitume" imejengwa katikati ya mji wa Cerro de Los Angeles, kiini cha nchi ya Hispania. Hapa ni mahali ambapo pia kuna Makumbusho ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na Kituo cha “Mama Yetu wa Mitume, Mlinzi na Mwombezi wa mji wa Getafe, Hispania. Kristo Yesu awe ni kiini cha maisha na utume wao na kwamba, waendelee kujiweka karibu zaidi na Moyo Mtakatifu wa Yes una Bikira Maria, Mama Yetu wa Mitume, awalinde na kuwasindikiza katika safari na maisha ya wito wao wa Kipadre.

Malezi ya Kipadre
04 August 2024, 15:39