Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!  Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!   (Vatican Media)

Uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2027: Seoul Korea ya Kusini

Kardinali Andrew Soo-jung Yeom, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, katika mahubiri yake, amewataka vijana kujisikia kuwa ni wahusika wakuu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na historia yao. Wahakikishe kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini. Waendelee kujikita katika ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa Korea. Siku ya Vijana Ulimwenguni 28 Julai - 3 Agosti 2025.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini, mapendo na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!  Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi. Hili ni Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Siku ya Vijana Ulimwenguni: Seoul, Korea ya Kusini mwaka 2027
Siku ya Vijana Ulimwenguni: Seoul, Korea ya Kusini mwaka 2027

Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni na kijamii. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa kwa kujishikamanisha na: huruma pamoja na upendo wa Kristo Yesu.  Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake!

Siku ya Vijana Ulimwenguni: Upyaisho wa Imani na Matumaini
Siku ya Vijana Ulimwenguni: Upyaisho wa Imani na Matumaini

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma ya Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa kipindi cha zaidi ya miaka arobaini. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yataadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake. 

Vijana wa Korea ya Kusini ni mashuhuda wa imani na matumaini
Vijana wa Korea ya Kusini ni mashuhuda wa imani na matumaini

Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho haya. Anasema, Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini, hivi karibuni limezindua, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yatakayoadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini. Hili ni tukio ambalo limehudhuriwa na wawakilishi kutoka katika Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao pamoja na viongozi wa Serikali ya Korea. Hii ni fursa ambayo imeiwezesha Serikali ya Korea ya Kusini kutengeneza ajira zipatazo 24, 000. Kardinali Andrew Soo-jung Yeom, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, katika mahubiri yake, amewataka vijana kujisikia kuwa ni wahusika wakuu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na historia yao. Wahakikishe kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini. Waendelee kujikita katika ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa Korea.

GMG Korea
10 August 2024, 15:30