Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Agosti 2024 ameandika Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Agosti 2024 ameandika Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre.  

Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre

Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre. Walengwa wakuu ni: Majandokasisi, mawakala wa malezi na majiundo ya shughuli za kichungaji na hatimaye, ni waamini wote wanaotaka kujikita katika majadiliano ya utamaduni wa nyakati, fasihi inakuwa ni nyenzo muhimu sana. Fasihi ina mchango mkubwa katika malezi na majiundo ya Majandokasisi kwa sasa na kwa siku za usoni; kwa kuzingatia ubinadamu wa Kristo Yesu unaobeba ndani mwake,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii iliyokusudiwa kwa sababu huumbwa kwa lugha katika hali ya kuvutia na kuweka madoido ya kila namna ili iweze kuvutia wasomaji au wasimuliaji wake, lengo lake kuu ni kufikisha ujumbe kwa jamii. Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisia zinazomgusa kwa kutoa kielelezo chenye maana. Hivyo unaona kazi za sanaa katika nyanja mbalimbali. Dhima za Fasihi: Kusisimua, Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii; Kudumisha na kuendeleza lugha; Kuelimisha jamii. Fasihi hukosoa, huonya na kurekebisha jamii; hueleza waziwazi wale wanaotenda kinyume na matakwa ya jamii, inabidi kukemea na kuonyana kwa kutumia methali na nahau. Fasihi Simulizi: ni fasihi ambayo hutumia masimulizi ya mdomo kufikisha ujumbe wake kwa jamii. Ni fasihi ambayo ni kongwe na ilianza tangu binadamu alipoanza kuishi duniani. Fasihi simulizi ina tanzu nne nazo ni: Hadithi, Semi, Ushairi na Maigizo. Fasihi Andishi hutumia maandishi ili kufikisha ujumbe kwa jamii. Fasihi andishi ina tanzu nne: Tamthilia, Ushairi, Ngonjera na Riwaya.

Fasihi ni muhimu sana katika malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi
Fasihi ni muhimu sana katika malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi

Ni katika muktadha wa Fasihi, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Agosti 2024 ameandika Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre. Walengwa wakuu ni: Majandokasisi, mawakala wa malezi na majiundo ya shughuli za kichungaji na hatimaye, ni waamini wote wanaotaka kujikita katika majadiliano ya utamaduni wa nyakati, fasihi inakuwa ni nyenzo muhimu sana. Fasihi ina mchango mkubwa katika malezi na majiundo ya Majandokasisi kwa sasa na kwa siku za usoni; kwa kuzingatia ubinadamu wa Kristo Yesu unaobeba ndani mwake, Umungu wake; tayari kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa. Kumbe, Fasihi ina umuhimu wake katika mchakato wa mang’amuzi yanayosimikwa katika upembuzi yakinifu, kwa kuonesha uhusiano uliopo kati ya Neno la Mungu na Ushirika katika Sakramenti za Kanisa; muungano kati ya Neno la Mungu na maneno ya binadamu; mambo yanayosimikwa katika utamaduni na huduma ya kusikiliza; huruma na karama; mambo yanayowajibisha na hivyo kutoa taswira ya kweli na wema inayofumbata uzuri. Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre, pamoja na mambo mengine, unafafanua kuhusu: Imani na utamaduni; Fumbo la Umwilisho; Umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusikiliza; Fasihi ni nguzo ya mang’amuzi; Kutazama kwa kutumia macho ya wengine na hatimaye ni nguvu ya maisha ya kiroho katika fasihi. Baba Mtakatifu anawaalika Majandokasisi kujenga utamaduni wa fasihi simulizi na andishi kwa kujisomea vitabu na kwamba, hii ni sehemu muhimu sana katika malezi na majiundo ya Majandokasisi, kwa sababu kila mtu ataweza kupata utambulisho wake kwa wahusika wakuu. Fasihi ni mwandani wa malezi na majiundo ya Kipadre.

Papa Francisko anakazia umuhimu wa fasihi katika majiundo ya Mapadre
Papa Francisko anakazia umuhimu wa fasihi katika majiundo ya Mapadre

Imani na Tamaduni: Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanapozungumzia ulinganifu kati ya utamaduni wa kibinadamu na mafundisho ya Kikristo wanasema, fasihi na sanaa, kwa maana zake, ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Maana, zinafanya juhudi ili kuijua tabia mahususi ya binadamu, pamoja na matatizo na mang’amuzi yake katika bidii anayoifanya ya kujifahamu na kujikamilisha mwenyewe na ulimwengu mzima. Tena fasihi na sanaa hujishughulisha kuitambua hali ya binadamu katika historia na katika ulimwengu; kufafanua unyonge na furaha zake, na hatimaye kueleza mahitaji na uwezo wake, pamoja na kudokeza hali ya kiutu iliyo nzuri zaidi. Na hivyo sanaa hizo huweza kuyainua maisha ya kibinadamu zinazoyaeleza kwa namna nyingi, kadiri ya mahali na nyakati. Rej. Gaudium et spes, 62. Fasihi inaweza kutumika kama sehemu ya kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; pamoja na kujikita katika kanuni maadili na utu wema; tayari kutangaza na kushuhudua Habari Njema ya wokovu. Fasihi inaweza kutumika kwa ajili ya Injili “Preparazio evangelica” na hivyo kulifanya kuingia katika majadiliano na tamaduni mbalimbali.

Fasihi inatumia lugha kufikisha ujumbe wake
Fasihi inatumia lugha kufikisha ujumbe wake

Fumbo la Umwilisho: Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni kuweza kukata kiu ya watu kukutana na Mwenyezi Mungu; watu waweze kusaidiwa kukutana na Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili katika historia ya mwanadamu. Huyu ni Kristo Yesu mwingi wa huruma na mapendo anayewatia shime waja wake kuonesha wema na ukarimu; toba na msamaha; umoja na mshikamano na kwa maneno machache wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “Kwa kweli ni katika Fumbo la Neno aliyefanyika mwili tu kwamba Fumbo la binadamu linaangazwa. Hili ni fumbo linalokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya binadamu: katika madonda, matamanio, kumbukumbu na matumaini katika maisha. Rej. Gaudium et spes, 22. Mafao Makubwa: Wanasayansi wengi wanasema, kuna faida kubwa ikiwa kama watu watajikita katika fasihi kwani huu ni msaada mkubwa wa kukuza na kudumisha kipaji cha akili na ugunduzi; inamsaidia mtu kuweza kuzama katika yale anayofanya na hivyo kumpatia mtu amani na utulivu wa ndani; tayari kupambana na changamoto mbalimbali za maisha; na hivyo kumfunda mtu maisha. Kumbe katika maisha ya kidini, katika upendo, kanuni maadili na utu wema; mtu anabaki jinsi alivyo. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuanza kujenga utamaduni wa kupenda fasihi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kwamba, ni hatari sana, ikiwa kama watu wanapoteza uwezo wa kusikiliza, kwani wanaweza kujikuta wanatumbukia katika ulemavu wa kutosikia kiroho. Mtakatifu Paulo VI anasema, maisha na utume wake katika Kanisa unahitaji uwepo wa watu wengine, ili kusaidia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Changamoto kubwa kwa waamini katika ulimwengu mamboleo ni imani kwa Mwenyezi Mungu na mbele ya wanadamu wengine.

Dhima za fasihi, kuhifadhi, kurithisha, kudumisha na kuendeleza lugha
Dhima za fasihi, kuhifadhi, kurithisha, kudumisha na kuendeleza lugha

Baba Mtakatifu Francisko anazidi kukaza akisema Fasihi ni nguzo kuu ya mang’amuzi. “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Ebr 4: 12-13. Neno la Mungu lina nguvu ya kuleta uhuru na kumwelekeza mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wake. Lakini hatua hii ni nyeti kwani inaweza kumkosesha mtu dira na mwelekeo sahihi katika maisha, ikiwa kama hatakuwa makini, kuhakikisha kwamba, anazama katika undani wa kile anachosoma na kutafakari. Jambo la muhimu ni kukuza na kudumisha mang’amuzi ya maisha! Hapo mfano wa mpanzi ni muhimu sana, ili mbegu iweze kuanguka katika udongo mzuri, tayari kuzaa matunda huyu mia, na huyu sitini na huyu thelathini. Rej Mt 13: 18-23. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutazama kwa kutumia macho ya wengine ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kushirikishana amana na utajiri wa manga’muzi ya wengine, yanayoacha chapa katika undani wa maisha ya msomaji, tayari kujenga na kudumisha huruma, uvumilivu na uelewa makini na kwamba, ni imani na upendo peke yake, vitakavyoweza kumwiimarisha mwamini; kutenda kwa wema na kuachana na ubaya. Huu ni mwaliko kwa mwamini kuzama katika undani wa maisha yake, ili kuangalia boriti la maisha yake “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Mt 7:3 Kristo Yesu anawauliza wafuasi wake! Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kwa kutambua uwepo angavu wa Roho Mtakatifu; neema ambayo inamfafanulia mwamini matumaini ya wokovu!

Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre
Waraka Kuhusu Dhamana ya Fasihi Katika Majiundo ya Mapadre

Mwishoni, Baba Mtakatifu anafafanua huku akielezea kuhusu nguvu ya maisha ya kiroho katika fasihi, kwa mwamini kuendelea kuwa wazi kiroho tayari kusikiliza sauti ya Mungu kati ya sauti nyingi; kwa kutoa nafasi ya Neno la Mungu ili liweze kuwa huru na wazi kwa ajili ya kuwatakasa watu, tayari kumpokea yule anayekuja kuyafanya yote kuwa ni mapya. Rej Uf 21: 5. Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu uwezo wa kuwapa majina viumbe wote, ndivyo ilivyo pia kwa Mapadre, ambao wanayo dhamana ya kulinda na kutunza kazi ya uumbaji, watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa ushirika kati ya kazi ya uumbaji na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, tayari kuangaza medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Padre kama msanii anaonekana katika muungano thabiti wa Kisakramenti kati ya Neno la Mungu na Maneno ya binadamu yanayogeuzwa na kuwa maisha kwa kusikilizwa na kueleweka kama jambo la kweli na jema linalofumbatwa katika uzuri. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa usomaji wa Neno la Mungu.

Fasihi Katika Malezi
08 August 2024, 13:59