Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa watawa hawa amekazia kuhusu: Mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa watawa hawa amekazia kuhusu: Mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Watawa Zingatieni: Mang'amuzi, Majiundo Makini na Injili ya Upendo

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na Watawa wa Mashirika ya: Watawa Wamisionari Wadominikani wa Mtakatifu Sixtus;Watawa Wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu; Watawa Shirika la Kutolewa Bikira Maria Hekaluni pamoja na Shirika la Miito Mitakatifu Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa watawa hawa amekazia kuhusu: Mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanasukumizwa pembeni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mikutano mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inayoadhimishwa wakati huu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa kila Shirika la Kitawa na Kazi za Kitume, ili kulinda, kutunza na kuendeleza karama za waanzilishi wa Mashirika haya. Huu ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kuchunguza na kusoma ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kubaini masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu mamboleo. Rej, Gaudium et spes, 4. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Huu ni muda muafaka kwa kila mwanashirika kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha yake binafsi na ule wa kijumuiya, tayari kuzama katika maendeleo ya Shirika kwa sasa na kwa siku usoni. Tangu mwanzo wa Kanisa wamekuwepo watu kwa kutekeleza mashauri ya Injili walinuia kumfuasa Kristo Yesu kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu ambao unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, na unaojitoa kabisa kwa Mungu na kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, wanaamua kumfuata Kristo Yesu kwa karibu zaidi kwa kujisadaka na kuonesha upendo kwa Mungu, anayepaswa kupendwa kuliko vitu vyote. Rej. Perfectae caritatis, 1 na KKK, 916.

Maadhimisho ya Mikutano mikuu ya Mashirika ni wakati wa sala na tafakari
Maadhimisho ya Mikutano mikuu ya Mashirika ni wakati wa sala na tafakari

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Mambo msingi ni: mang'amuzi, majiundo makini na Injili ya upendo
Mambo msingi ni: mang'amuzi, majiundo makini na Injili ya upendo

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mikutano Mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na Watawa wa Mashirika ya: Watawa Wamisionari Wadominikani wa Mtakatifu Sixtus (Suore Domenicane Missionarie di San Sisto); Watawa Wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, (Suore della Società del Sacro Cuore di Gesù) Watawa Shirika la Kutolewa Bikira Maria Hekaluni (Suore della Presentazione di Maria Santissima al Tempio) pamoja na Shirika la Miito Mitakatifu (Padri Vocazionisti). Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa watawa hawa amekazia kuhusu: Mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Mang’amuzi ya miito ni dhana inayogusa Mashirika yote ya Kitawa na Kazi za Kitume; kama mtawa mmoja mmoja, lakini zaidi kama Wanashirika. Huu ni mchakato muhimu sana katika maisha na utume wa watawa, iwe nyakati za matukio makuu au katika maisha ya kila siku. Ni mchakato unaofumbatwa katika uhuru, ili hatimaye, uweze kufikia hatima yake; lakini unatekelezwa hatua kwa hatua, kama wito kwa kila mwamini na wito unaojitofautisha kwa kila mmoja. Hii ni kazi inayosimikwa katika utamaduni wa kusikiliza kwa makini kutoka kwa Kristo Yesu; utamaduni wa mtu mwenyewe kujisikiliza sanjari na kuwasikiliza wengine.

Sala, tafakari, uvumilivu, ujasiri na sadaka muhimu kwa watawa
Sala, tafakari, uvumilivu, ujasiri na sadaka muhimu kwa watawa

Ni mchakato unaofumbatwa katika maisha ya sala; tafakari ya kina ya Neno la Mungu, katika hali ya uvumilivu, ujasiri na sadaka ili kuchukua hatua stahiki, inayomkirimia mwamini furaha ya kweli. Ulimwengu mamboleo una kiu kubwa ya kugundua haki na uzuri wa kuamua, ili kufanya mageuzi makubwa katika maisha, kama yale yanayohusu wito! Kumbe, kuna haja ya kuwa na washauri wa maisha ya kiroho, watakaowasaidia vijana wa kizazi kipya kuweza kuwa huru na hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha. Vijana wawe huru, huku wakitumia akili na busara, sadaka na majitoleo, ili kukua na hatimaye, zawadi ya maisha ya wito iweze kukomaa na hivyo kuwawezesha vijana hawa kuwa na furaha, huku wakipenda kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao.

Injili ya huruma na upendo, itangazwe na kushuhudiwa na watawa
Injili ya huruma na upendo, itangazwe na kushuhudiwa na watawa

Majiundo makini ni tema inayowaunganisha watawa wa Mashirika yote kwani haya ni malezi na majiundo yanayomwelekeza mtawa katika njia ya utakatifu wa maisha, mbegu iliyopandwa ndani mwao kwa njia ya wito wa maisha ya kitawa. Majiundo haya hayana budi kujikita katika maisha ya sala katika kiwango cha mtu binafsi na kile cha jumuiya; maisha ya Kisakramenti; Kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Yote haya yakitekelezwa kwa umakini mkubwa yanasaidia kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kati ya mtawa na Kristo Yesu. Ni kwa njia ya majiundo makini, hapo mtawa anaweza kugundua kuwa anaweza kuwa ni mlezi kwa wengine, akiwa na uwezo wa kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yake; kwa kutafuta ile furaha katika ukweli, ili hatimaye, kuweza kuwashirikisha wengine Mwanga wa Mungu. Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo wanayo dhamana kubwa ya kinabii mintarafu hali ya kijamii na kitamaduni, kutokana na “bahari ya mawasiliano ya jamii”, ambayo kwa bahati mbaya ni dhaifu sana na hayawezi kujenga mahusiano thabiti ya kibinadamu. Kumbe, kuna haja ya kuwa na walimu ambao kwa njia ya upendo wanaweza kuwa ni wandani wa wale wanaowaamini katika safari ya maisha yao ya kiroho.

Watawa wazingatie majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya
Watawa wazingatie majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watawa wanapaswa kujibidiisha kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo; wawaelimishe vijana wa kizazi kipya, ili waweze kujibu kwa ari na moyo mkuu kuhusu Injili ya upendo, kama walivyofanya waasisi wa Mashirika yao, kama alama ya Injili ya upendo. Hata katika ulimwengu mamboleo, mbele ya macho yao, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, wapewe kipaumbele cha pekee, kwani hawa ndio wale watu wanaopaswa kuonjeshwa Injili ya huruma na upendo; na hiki ndicho kielelezo cha uwepo wa watawa ndani ya Kanisa na kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuzungumza nao kwa njia ya maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii. Siku ya mwisho, watu watahukumiwa kwa jinsi walivyowatendea maskini. Rej. Mt 25:31-45. Huduma yoyote ile inayotolewa kwa maskini ni kielelezo cha upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kutupa, usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; hapa kuna haja ya kushinda uchoyo, ubinafsi na mipasuko, mambo yanayoendelea kutawala katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashuruku watawa wote kwa huduma wanayoitoa kwa Kanisa, waendelee kuwa na imani katika maisha na utume wao.

Watawa

 

12 August 2024, 14:49