Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Papua New Guinea, Dominika tarehe 8 Septemba 2024 ametembelea Jimbo Katoliki la Vanimo na kupata nafasi ya kuzungumza na kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu Jimboni humo. Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Papua New Guinea, Dominika tarehe 8 Septemba 2024 ametembelea Jimbo Katoliki la Vanimo na kupata nafasi ya kuzungumza na kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu Jimboni humo.   (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Papua New Guinea: Hotuba Jimboni Vanimo: Ushuhuda wa Uinjilishaji

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Papua New Guinea, Dominika tarehe 8 Septemba 2024 ametembelea Jimbo Katoliki la Vanimo na kupata nafasi ya kuzungumza na kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu Jimboni humo. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; uinjilishaji wa kina katika mazingira wanamoishi waamini; umoja wa familia na upendo kwa Mungu na jirani. Ushuhuda wa imani tendaji ni muhimu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Baba Mtakatifu nje ya Vatican zinapania pamoja na mambo mengine: kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, Kiutu na Kitamaduni katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji na kama sehemu mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko. Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Utu, heshima na utamaduni wa watu mahalia unapaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa kwani kutokana na changamoto za maendeleo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, watu hawa na tunu zao msingi wanaweza kujikuta wametelekezwa na hatimaye kung’olewa katika maeneo na makazi yao; hali inayodhalilisha utu wa binadamu.

Papa amekutana na kuzungumza na waamini wa Jimbo Katoliki la Vanimo
Papa amekutana na kuzungumza na waamini wa Jimbo Katoliki la Vanimo

Wenyeji wa Papua New Guinea ni ushuhuda makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, binadamu anaweza kuishi vyema, huku akitunza na kuendeleza mazingira, nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika vipaumbele na uhalisia wa maisha ya watu, kwani kazi ya uinjilishaji inahusika na inadai ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, Mwenyezi Mungu anataka watoto wake waishi kwa raha katika ulimwengu huu. Rej. Evangelii gaudium, 182. Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Papua New Guinea, Dominika tarehe 8 Septemba 2024 ametembelea Jimbo Katoliki la Vanimo na kupata nafasi ya kuzungumza na kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu Jimboni humo. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; uinjilishaji wa kina katika mazingira wanamoishi waamini; umoja wa familia na upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ni juhudi zilizofanywa na wamisionari, watawa na makatekista kunako karne ya kumi na tisa. Watu hawa wametangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu iliyomwilishwa katika huduma makini katika sekta ya: elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu kiasi kwamba, wamegeuka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani na upendo, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafuta na kuambata ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amana na utajiri wa maliasili ni changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Papua New Guinea kuilinda, kuitunza na kuiendeleza. Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya upendo wa Mungu unaookoa; upendo unaokita mizizi yake katika Sakramenti ya Ndoa, Upendo kwa Mungu na jirani pamoja na uzuri wa Injili ya Kristo Yesu.

Papa Francisko amesikiliza shuhuda za uinjilishaji wa kina Jimboni Vanimo
Papa Francisko amesikiliza shuhuda za uinjilishaji wa kina Jimboni Vanimo

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wabatizwa wote ni wakala wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, hii ni dhamana na wajibu wa kila mbatizwa, kwani kila mwamini ameonja upendo wa Mungu unaookoa, changamoto na mwaliko wa kuutangaza na kuushuhudia na kwamba, kila Mkristo ni mmisionari dhamana inayopaswa kuanzia ndani ya familia, shuleni, mahali pa kazi kwa kupendana kwa dhati na kwa njia ya upendo huu, watu wote watawatambua kuwa wao ni wanafunzi wa Kristo, wakiwa na upendo wao kwa wao. Re. Yn 13:35; Mt 22:35-40. Baba Mtakatifu amekazia pia umoja unaosimikwa katika tofauti zao msingi kama njia ya kuganga na kuuponya ulimwengu, ushuhuda makini uliotolewa na Mwenyeheri Pietro To Rot, Mwanandoa, Baba wa familia, Katekisita na shuhuda wa imani nchini Papua New Guinea, aliyethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kutetea na kulinda umoja wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya wale wote waliotaka kubomoa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Amana na utajiri mkubwa kuliko vyote ni upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wanaokutana nao; furaha na tabasamu kutoka kwa watoto; mambo msingi wanayopaswa kuyatunza katika sakafu ya maisha yao.

Mchakato wa uinjilishaji wa kina uanzie nyumbani.
Mchakato wa uinjilishaji wa kina uanzie nyumbani.

Askofu Francis H. Meli wa Jimbo Katoliki Vanimo katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na Wanajimbo wa Vanimo amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kusaidia kujenga na kuimarisha, matumaini, umoja na amani kati ya watu wa tamaduni, makabila, lugha, jamaa na Taifa. Hija hii ni alama ya: matumaini, umoja, amani na upendo dhidi ya ghasia zinazoharibu maisha ya binadamu. Tarehe 17 Januari 1995 Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alitembelea Papua New Guinea na kumtangaza Mtumishi wa Mungu To Rot kuwa ni Mwenyeheri, aliyeonesha umuhimu wa Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na utume wa Uinjilishaji. Askofu Francis H. Meli wa Jimbo Katoliki Vanimo amepongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchangia katika mchango wa Uinjilishaji na Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; nyaraka zinazowakumbusha walimwengu kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maisha na utume wa Kanisa ni juhudi za Wamisionari wa shirika la Mapadre wa Mateso “Congregatio Passionis Iesu Christi, C.P.) na baadaye walifuatia Wamisionari Wafranciskani. Kwa upande wake Sr. Jaisha Josep, DPMT amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko maisha na utume wao Jimboni humo katika kufundisha Katekesi, Kutembelea Familia, Utume wa Vijana wa kizazi kipya na kwamba, wanatekeleza utume wao katika sekta ya elimu, afya, maendeleo ya jamii bila kusahau huduma makini kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Papua New Guinea iliamsha miito mingi na kwamba, hija hii ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko itapyaisha tena utambuzi wa tunu msingi za maisha ya kifamilia na kitawa, tayari kujibu mwaliko wa wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Papa Francisko ameguswa na ukarimu na furaha ya waamini wa Vanimo
Papa Francisko ameguswa na ukarimu na furaha ya waamini wa Vanimo

Nayo familia ya David na Maria Kulo, wanandoa wanasema, wao ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazosimikwa katika furaha, upendo, amani. Kama wanandoa wanashirikishana dhamana na majukumu; wanakuza na kudumiza mawasiliano bora, ili kuvuka vikwazo na magumu ya maisha; tayari kusameheana na kuanza upya. Ni matumaini yao kwamba, vijana wengi wa kizazi kipya watajizatiti katika maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, Agano la Ndoa linapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kudumishwa mbele ya Mungu. Kwa upande wake Maria Joseph, kutoka Kituo cha Lujan kwa ajili ya wanawake, ametoa ushuhuda wa maisha yake katika kukabiliana na changamoto za afya, kiasi kwamba, akawa ni sehemu ya familia ya Masista waliokuwa wanamtunza. Wanaweza kwenda shule, kukua na kukomaa katika nyanja nyingi za maisha. Ni matumaini yake kwamba, iko siku atakuwa “Wakili Msomi” ili kuisaidia jamii yake. Ushuhuda wa mwisho umetolewa na Steven Abala, Katekista, ambaye pamoja na Makatekista wenzake wanajitahidi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwaandaa waamini kupokea Sakramenti za Kanisa; kuwasaidia katika maisha ya sala na huduma Dominika isiyokuwa na Padre. Katika maisha na utume wao, wanakabiliana na changamoto nyingi: ikiwemo ada ya shule kwa watoto wao, mahitaji ya makazi, huduma za elimu na afya pamoja na usafiri. Jimbo Katoliki la Vanimo lina Makatekista 50 wengi wameacha kutoa huduma kutokana na changamoto za maisha, lakini bado kuna mahitaji makubwa ya Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa.

Jimbo Katoliki la Vanimo
08 September 2024, 14:36