Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija ya kitume nchini Ubelgiji na Luxembourg kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024. Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija ya kitume nchini Ubelgiji na Luxembourg kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024.   (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Ubelgiji na Luxembourg: Ushuhuda!

ametia nia ya kutembelea Ubelgiji na Luxembourg kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024, ili kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi pamoja na hija ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya sanjari na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu na ushuhuda wa imani katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mialiko ya viongozi wa Serikali na Kanisa na hivyo ametia nia ya kutembelea Ubelgiji na Luxembourg kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024, ili kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi pamoja na hija ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya sanjari na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Ubelgiji ni kati ya nchi ambazo zimeathirika sana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo kiasi cha kupelekea Askofu Roger Vangheluwe wa Jimbo Katoliki la Bruges kuvuliwa wadhifa wake na sasa ni mwamini mlei.

Ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa ni muhimu
Ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa ni muhimu

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, huu ni wito na mwaliko wa kutembea pamoja kwenye barabara ambayo ni historia ya nchi ya Ubelgiji, lakini hii ni safari inayofumbata Injili, Njia ya Kristo Yesu, Tumaini letu. Kauli mbiu inayonogesha hija hii ya kitume nchini Luxembourg ni “Pour servir”, inachota amana na utajiri wake kwenye Maandiko Matakatifu yanayomwelezea Kristo Yesu kwamba, hakuja kutumikiwa, bali “kutumika” na kutoa nafsi yake iwe ni fidia ya wengi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa Mama Kanisa kwa kufuata mfano wa Mwalimu wake, anaitwa na kutumwa kuwahudumia walimwengu.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni agenda muhimu
Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni agenda muhimu

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko inafuatia hija kama hii iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Ubelgiji na Luxembourg kunako mwaka 1985 na kunako mwaka 1995 alipomtangaza Mtumishi wa Mungu Damian de Veuster, Maarufu kama Damian di Molokai, mmisionari aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa wakoma, kiasi hata cha kupoteza maisha kwa ugonjwa wa Ukoma, huko Hawaii. Baba Mtakatifu Francisko naye atamtangaza Mtumishi wa Mungu Anna de Jesus kuwa ni Mwenyeheri. Wakristo katika nchi hizi mbili wanakabiliwa na changamoto ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya uhalisia wa maisha yao, hasa Barani Ulaya, ambako idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki inaendelea kuporomoka kila kukicha. Kumbe, hija hii pamoja na mambo mengine, inapania kuwatia shime watu wa Mungu Barani Ulaya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama sehemu ya ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.
Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee watu wa Mungu Barani Ulaya kuwekeza katika ukarimu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; haki na amani, ili kuondoa hofu ya kuzuka kwa vita Barani Ulaya. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, atakazia umuhimu wa Elimu Katoliki katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Kuna uwezekano wa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na waathirika wa kashfa ya nyanyaso za ngono kwa watoto wadogo. Viongozi wakuu kutokana Vatican wanaoshiriki hija hii ya kitume ni pamoja na: Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri pamoja na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu.

Hija ya Kitume ya 46
24 September 2024, 15:43