Hija ya Kitume ya Papa Francisko Timor ya Mashariki: Utamadunisho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano; mafungamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 Baba Mtakatifu Francisko ameanza hija yake ya kitume nchini Timor ya Mashariki. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Timor ya Mashariki. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu amemtumia telegramu Bob Dadae, Gavana mkuu wa Papua New Guinea, akimshukuru kwa niaba ya viongozi wote wa Papua New Guinea kwa ukarimu na mapokezi ya “kukata na shoka” waliyompatia wakati wa hija yake ya Kitume nchini humo. Amewahakikishia sala na sadaka yake kwa watu wa Mungu nchini Papua New Guinea na kwamba, anawaombea amani na utulivu.
Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anaingia kwenye anga la Australia amemtumia ujumbe Sam Mostyn, Gavana mkuu wa Jumuiya ya Madola ya Australia, akiwatakia kheri na fanaka; na kwamba anapenda kuwahakikishia sala na baraka zake. Baba Mtakatifu amewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dili na kulakiwa na viongozi wa Serikali na Kanisa. Hii ni hija kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 11 Septemba 2024.