Hija ya 45 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Barani Asia na Oceania: Ujumbe kwa Vijana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Changamoto kubwa iliyoko mbele ya vijana wengi ni utupu unaojionesha katika tamaduni kutokana na mawazo hafifu pamoja na kutopea kwa imani, kunakowafanya watu kushindwa kuzamisha maisha yao katika mambo msingi, kiasi cha imani kuonekana kuwa si mali kitu kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, hitimisho la namna hii ni kosa kubwa, kwani leo hii kuna vijana wanaochakarika kutafuta maana ya maisha; vijana wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makuu ya maisha. Kuna vijana wanaompenda na wanataka kuambatana na Kristo Yesu; hawa ni vijana wenye upendo mkubwa kwa binadamu. Kuna vijana wanaotafuta furaha, upendo wa kweli, mafanikio na hata utimilifu wa maisha ya ujana wao! Yote haya ni matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya, ambayo yanapaswa kuratibiwa kama alivyofanya Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji. Kanisa halina budi kuwasaidia vijana kuratibu na kudhibiti matamanio yao pamoja na kuwawezesha kuwa ni wadau, kwa kuwapatia nafasi, ili kweli waweze kuchachua matamanio yao! Ulimwengu wa vijana umegawanyika katika sehemu mbali mbali! Kumbe, kunahitajika: ubunifu unaofumbatwa katika wongofu wa kichungaji, ili kuwaonesha mapendekezo ya Kiinjili yanayoweza kuwasaidia kufanya mang’amuzi ya miito yao ndani ya Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, 2018 pamoja na Wosia wa Kitume: “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ni nyaraka muhimu sana zinazoweza kuyasaidia Makanisa mahalia katika sera na mbinu mkakati wa malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, ili waweze kujenga umoja na mshikamano na Kristo Yesu, kama mwenza wa safari ya maisha yao!
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Ni katika muktadha wa umuhimu wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 wakati wa hija yake ya Kitume nchini Papua New Guinea amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya katika Uwanja wa michezo wa “Sir John Guise” ulioko mjini Port Moresby. Katika hotuba yake amewasifia watu wa Papua New Guinea kwa kutunza mazingira nyumba ya wote; Tabasamu la furaha na matumaini; Mnara wa Babeli ni kiashiria cha kuchanganyikiwa na hali ya kukata tamaa, mwaliko wa kuambata lugha inayojenga umoja na ushirika; lugha ya upendo, ukaribu na huduma! Vijana wanapoteleza na kuanguka, wajitahidi kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; washikamane na kusaidiana kunyanyuana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, jitihada za ujenzi wa Mnara wa Babeli zilikuwa ni kiashiria cha binadamu kuchanganyikiwa na kukata tamaa! Hizi ni njia mbili tofauti za ujenzi wa jamii, moja ni kuelekea katika kuchanganyikiwa na nyingine katika hali ya amani na utulivu, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujenga jamii kwa kutumia lugha inayodumisha mchakato wa mahusiano na mafungamano ya kijamii.
Hii ni lugha ya upendo inayovunjilia mbali kuta za upinzani, uadui, chuki na tabia ya kutaka kulipizana kisasi; hali ya kutojali mateso na mahangaiko ya wengine na kwamba, tabia hii inakita mizizi yake katika uchoyo na ubinafsi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na bibi na babu zao au na wazee katika ujumla wao. Vijana waimarishe lugha ya moyo inayosimikwa katika upendo, ukaribu na kwamba, hii ni lugha ya huduma. Kamwe vijana wa kizazi kipya wasiogope kuteleza na kuanguka, bali wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele; washikamane na kusaidiana. Lugha hii iwe ni chombo cha ujenzi wa umoja na ushirika wa watu wa Mungu nchini Papua New Guinea, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na uhuru wao. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe ili kukoleza upendo na mawasiliano katika familia. Tafakari ya Neno la Mungu iwasaidie kujenga urafiki wa kijamii, amani na utulivu ili Papua New Guinea iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana wajitahidi kuvunjilia mbali kuta za utengano, wawe na ujasiri wa kukataaa na kupinga matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ulevi na picha za utupu zinazomwachia mwanadamu machungu katika maisha. Wawe imara katika imani, wajitose bila ya kujibakiza katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha; Wamwombe Mwenyezi Mungu awakirimie ujasiri wa upendo na imani; tayari kushikamana na kutembea kwa pamoja katika ndoto ya utamaduni wa upendo! Washikamane na kunyanyuana pale wanapoteleza na kuanguka!
Kwa upande wake Askofu John Bosco Auram wa Jimbo Katoliki la Kimbe, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Utume wa Vijana nchini Papua New Guinea amewaalika vijana kusoma, kutafakari na kuumwilisha Waraka wa Kitume wa Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ambao umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito.” Vijana watambue kwamba wao ni wadau wakuu wa mchakato wa Uinjilishaji kwani wanapaswa kuinjilishwa ili waweze kuinjilisha. Changamoto kubwa miongoni mwa vijana ni kumtambua Kristo Yesu katika hali na mazingira ya vijana, tayari kumtangaza na kumshuhudia.
Kwa upande wake Bernadette Turmoni, Mwakilishi wa Vijana wa Papua New Guinea, amegusia kuhusu; matatizo, changamoto na fursa za vijana wa kizazi kipya nchini Papua New Guinea; Nyanyaso kutoka ndani ya familia zinawafanya vijana wengi kujisikia kutopendwa wala kuthaminiwa, kiasi cha kupoteza imani na matumaini na matokeo yake ni idadi ya vijana kujinyonga. Changamoto ya pili ni umaskini wa hali na mali, inayowapelekea vijana wengi kujitumbukiza katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, wizi na ukahaba. Kati yao wamegeuka na kuanza kuishi katika mazingira magumu na hatarishi. Vijana watambue kwamba, wanaitwa kumpenda na kumtumikia Mungu; Kuinjilisha kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake; Vijana waendelee kujipyaisha katika maisha na utume wa Kanisa. Mwakilishi wa Chama cha Wanataaluma Wakatoliki Nchini Papua New Guinea, ametoa mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuendelea kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa kwa maneno na matendo yao adili na matakatifu. Wawe makini katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na waendelee kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wajitoe na kujisadaka kwa ajili ya huduma katika jamii. Ryan Vulum, Mwakilishi wa Vijana Papua New Guinea amegusia changamoto za vijana wanaotoka katika familia zilizotengana, lakini wameimarishwa na kutunzwa na Kanisa. Wengine wamekengeuka na kutopea katika malimwengu. Wanandoa wadumishe tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili vijana waweze kupata hifadhi na usalama wa maisha yao.