Tafuta

Baada ya kuwasili na kufanyiwa mapokezi ya Kitaifa, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na Viongozi wa vyama vya kiraia kwenye Ukumbi wa mikutano wa “Cercle Citè.” Baada ya kuwasili na kufanyiwa mapokezi ya Kitaifa, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na Viongozi wa vyama vya kiraia kwenye Ukumbi wa mikutano wa “Cercle Citè.”   (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Luxembourg: Hotuba Kwa Viongozi

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu mchango wa Luxembourg katika matukio ya Kimataifa; Luxembourg kama nchi muasisi wa Umoja wa Ulaya, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Injili ya Kristo ni chemchemi na nguvu ya upyaisho wa maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake na kwamba, Luxembourg ni shuhuda wa amani, mshikamano na mjenzi wa amani na usalama na kwamba, Kanisa liko kwa ajili ya kuwahudumia walimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, huu ni wito na mwaliko wa kutembea pamoja kwenye barabara ambayo ni historia ya nchi ya Ubelgiji, lakini hii ni safari inayofumbata Injili, Njia ya Kristo Yesu, Tumaini letu. Kauli mbiu inayonogesha hija hii ya kitume nchini Luxembourg ni “Pour servir”, inachota amana na utajiri wake kwenye Maandiko Matakatifu yanayomwelezea Kristo Yesu kwamba, hakuja kutumikiwa, bali “kutumika” na kutoa nafsi yake iwe ni fidia ya wengi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa Mama Kanisa kwa kufuata mfano wa Mwalimu wake, anaitwa na kutumwa kuwahudumia walimwengu katika hali ya unyenyekevu! Baba Mtakatifu alianza hija hii, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, ili kusali na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi “Vergine Salus Populi Romani. Asubuhi ya tarehe 26 Septemba 2024, Kikundi cha maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanaopata hifadhi kuzunguka Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku wakiwa wamesindikizwa na Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo ambaye pia ndiye Mtunza sadaka ya Kipapa wamemtembelea na kusalimiana na Baba Mtakatifu kabla ya kuondoka mjini Vatican. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu amepata bahati ya kuwatumia salam na matashi mema wakuu wa nchi wa Italia, Australia, Ujeruman na Ubelgiji.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Luxembourg
Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Luxembourg

Baba Mtakatifu anasema, anayo nia ya kukutana na kuzungumza na ndugu zake katika Kristo nchini Ubelgiji na Luxembourg, ili kuwashirikisha Injili ya amani na matumaini na kwamba, anaendelea kuwaombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia: Amani, ustawi na maendeleo endelevu kwa watu wao; adumishe moyo wa udugu wa kibinadamu na mshikamano wa upendo; hekima, umoja na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Kwa wote hawa Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake za kitume. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa pili kutembelea Ubelgiji na Luxembourg, baada ya hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kutembelea: Holand, Ubelgiji na Luxembourg kunako mwaka 1985 na baadaye nchini Ubelgiji mwezi Juni 1995. Baada ya kuwasili na kufanyiwa mapokezi ya Kitaifa, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na Viongozi wa vyama vya kiraia kwenye Ukumbi wa mikutano wa “Cercle Citè.” Katika hotuba yake amekazia kuhusu mchango wa Luxembourg katika matukio ya Kimataifa; Luxembourg kama nchi muasisi wa Umoja wa Ulaya, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Injili ya Kristo ni chemchemi na nguvu ya upyaisho wa maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake na kwamba, Luxembourg ni shuhuda wa amani, mshikamano na mjenzi wa amani na usalama na kwamba, Kanisa liko kwa ajili ya kuwahudumia walimwengu.

Watu waliofurika kumpokea Baba Mtakatifu Francisko
Watu waliofurika kumpokea Baba Mtakatifu Francisko

Baba Mtakatifu mekazia kuhusu mchango wa Luxembourg katika matukio ya Kimataifa na kwamba, imekwisha kuvamiwa mara mbili na hivyo kupokwa uhuru wake na uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe. Lakini mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Luxembourg imejipambanua kwa kusimama kidete katika ujenzi wa umoja na udugu Barani Ulaya kwa kuondokana na utaifa usiokuwa na mguso wala mashiko na hivyo kujikita katika ujenzi wa nyakati mpya za amani. Luxembourg ni nchi muasisi wa Umoja wa Ulaya na Makao makuu ya Taasisi za Umoja wa Ulaya, ikiwemo “Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya “Court of Justice of the European Union” Mahakama ya Wakaguzi wa Hesabu Ulaya “The European Court of Auditors” na hatimaye ni Benki ya Kitega Uchumi Ulaya “The European Investment Bank.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, msingi thabiti wa demokrasia nchini Luxembourg imeiwezesha nchi hii kujipambanua katika kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine, kiasi kwamba, Luxembourg imejiinua sana katika Jumuiya ya Kimataifa katika masuala ya kiuchumi na kifedha; kwa kujenga na kuimarisha miundo mbinu na sheria, kiasi kwamba, utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yamepewa kipaumbele cha kwanza na hivyo kuondokana na sera za ubaguzi. Hii ni nchi ambayo imeendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa binadamu; maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza na kushirikishwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu.

Papa Francisko alipowasili nchini Luxembourg 26 Septemba 2024
Papa Francisko alipowasili nchini Luxembourg 26 Septemba 2024

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaendelea kukazia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaowawajibisha. Watu wa Mungu nchini Luxembourg wajitahidi kuwasaidia wale wote wanaofatuta: hifadhi, usalama na maisha bora baada ya kulazimishwa kuzikimbia nchi zao.

Luxembourg: Wanaitwa kutangaza Injili ya Matumaini
Luxembourg: Wanaitwa kutangaza Injili ya Matumaini

Leo hii Barani Ulaya, kinzani na migogoro inaendelea kuibuka, kiasi cha kujenga uadui hali inayoweza kupelekea vita na maafa makubwa kwa watu na mali zao kiasi hata cha kuweza kulitumbukiza Taifa katika hali ya umaskini. Kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa umwilisho wa tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kujifunza kutorudia makosa yaliyotendeka kihistoria kwa kutumia maendeleo makubwa ya teknolojia kwa ajili ya kudumisha utamaduni wa kifo. Leo hii, binadamu amefikia hatua kubwa sana ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, hatari kwa maisha yake. Baba Mtakatifu anasema, Injili ya Kristo ni chemchemi na nguvu ya upyaisho wa maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake; ina uwezo wa kuleta mabadiliko katika moyo wa binadamu, kwa kutenda mema hata nyakati ngumu, ili hatimaye, kuzima chuki na hasira na hivyo kuanza mchakato wa upatanisho, wito na mwaliko ni kwa watu wote wenye mapenzi mema wajibidiishe kuifahamu Injili ya Kristo Yesu aliyempatanisha mwanadamu na Mwenyezi Mungu na anayefahamu kuganga na kuponya madonda yaliyoko katika sakafu ya moyo wa mwanadamu.  Luxembourg ni nchi ambayo inaweza kuonesha umuhimu wa amani dhidi ya madhara ya vita; ushirikishwaji wa wahamiaji na wakimbizi, dhidi ya sera na mikakati ya ubaguzi; ushirikiano na mafungamano ya kijamii dhidi ya uchoyo na ubinafsi. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa majadiliano ili kutatua tofauti zinazojitokeza ili kujenga na kudumisha usalama na amani kwa wote. Kanisa litaendelea kumhudumia mwanadamu na kwamba, wote wanaitwa na kutumwa kuhudumia.

Huduma kwa walimwengu katika fadhila ya unyenyekevu
Huduma kwa walimwengu katika fadhila ya unyenyekevu

Waziri mkuu Luc Frieden wa Luxembourg katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake amegusia hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II, tarikbani miaka 40 iliyopita; umuhimu wa nchi hii katika medani za Kimataifa na ni nchi ambayo ni shuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii, bila kusahau mchango wa Mtakatifu Willbroad na mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi ya Luxembourg inayosimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni nchi inayosimikwa katika demokrasia inayoheshimu uhuru wa dhamiri; kuna tofauti msingi za utendaji wa shughuli zake kati ya Serikali na Kanisa; lakini zinashirikiana katika huduma, kanuni maadili na utu wema pamoja na utunzaji wa mazingora nyumba ya wote. Amani pamoja na tunu msingi za maisha ni mambo ambayo yanapaswa kulindwa na kudumishwa, kwani vita ina madhara makubwa kwa maisha na mali za watu. Waziri mkuu Luc Frieden wa Luxembourg amehitimisha hotuba yake kwa kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa amani, demokrasia, haki msingi za binadamu pamoja na Sheria ya Kimataifa.

Hotuba Luxembiurg
26 September 2024, 15:04