Hija ya Kitume ya Papa Francisko Luxembourg: Hotuba Kwa Watu wa Mungu Luxembourg
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kauli mbiu inayonogesha hija ya kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Luxembourg ni “Pour servir”, inayochota amana na utajiri wake kwenye Maandiko Matakatifu yanayomwelezea Kristo Yesu kwamba, hakuja kutumikiwa, bali “kutumika” na kutoa nafsi yake iwe ni fidia ya wengi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa Mama Kanisa kwa kufuata mfano wa Mwalimu wake, anaitwa na kutumwa kuwahudumia walimwengu. Kanisa kuu la “Notre-Dame” kuanzia mwaka 1794 linahifadhi Sanamu ya Bikira Maria Faraja ya wanaoteseka, akawa ni Mlinzi na Mwombezi wa watu wa Mungu nchini Luxembourg. Tangu tarehe 16 Oktoba 1666 kukaanzishwa hija ya watu wa Mungu kila mwaka, kwenye Kanisa kuu la “Notre-Dame.” Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 26 Septemba 2024 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya Waamini Wakatoliki katika Kanisa kuu la “Notre-Dame. Amesikiliza shuhuda, ameangalia sanaa za maonesho kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na baadaye, amewahutubia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Agano la Kale linatilia mkazo kwa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji, wajane na watoto yatima. Huu ndio wajibu unaotekelezwa na Serikali ya Luxembourg kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wahamiaji.
Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Jubilei ya Bikira Maria kama kielelezo makini cha faraja na huduma, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Amefafanua maana ya huduma mintarafu Mafundisho ya Kristo Yesu; Utume unaokita mizizi yake katika uaminifu kwa Kanisa sanjari na tunu msingi za Kiinjili na kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Watu wa Mungu nchini Luxembourg wanaadhimisha Jubilei ya Miaka mia nne tangu walipoanza Ibada kwa Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka na kwamba, faraja na huduma ni tunu msingi za Injili ya upendo, amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Kristo Yesu; changamoto kwa waamini kumwomba Bikira Maria ili awasaidie waamini waweze kuwa ni wamisionari tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mt 20:28; Mk 10:48. Huu ni mwaliko wa kujikita katika huduma inayosimikwa kwenye ukarimu, ukweli na uwazi; kwa kuwapokea na kuwahudumia wengine bila kuwatenga watu. Rej. Evangelii gaudium 47. Baba Mtakatifu anawataka watu watakatifu wa Mungu nchini Luxembourg kuendeleza utamaduni wa ukarimu kwa watu wanaohitaji msaada na ukarimu wao; kwa kuwaheshimu na kuwathamini wengine na kwa njia hii, watakuwa wanatangaza na kushuhudia upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza furaha ya Injili na wala si kwa waamini kuelemewa na majonzi pamoja na hali ya kukata tamaa, bali kukubali changamoto za maisha na hivyo kuendelea kuwa waaminifu kwa Kanisa sanjari na tunu msingi za Kiinjili, hali ambayo inalisukuma Kanisa kubadilika, kwa kushirikishana nyajibu na utume; na kuendelea kutembea pamoja kama Jumuiya ya wamisionari, tayari kujenga na kudumisha Kanisa la Kisinodi linaloimarisha umoja na mafungamano ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kimaadili na ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia uzuri wa kazi ya Uumbaji. Kazi ya wamisionari si wongofu wa shuruti, bali ni wito wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili zenye mvuto na mashiko, tayari kutangaza furaha ya Injili kwa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kutangaza furaha ya Injili kama ilivyokuwa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Hii inatokana na ukweli kwamba, imani ya Kikristo imesheheni furaha ni kama dansi na kwamba, kama watoto wapendwa wa Mungu wanapaswa kuwa na furaha, huku wakiwa wameunganika kwa sababu hata Mwenyezi Mungu anafurahia wokovu wa watu wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Willibrord aliinjilisha kwa njia ya dansi mitaani, kwa kusindikizwa na mahujaji wengi na wageni waliojiunga pamoja naye. Hawa walikuwa wanatangaza na kushuhudia uzuri wa kutembea pamoja, kwa kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu na hatimaye, kuweza kuizunguka Meza ya Ekaristi Takatifu na Neno la Mungu. Kumbe, watu wa Mungu nchini Luxembourg wanapaswa kujikita katika faraja, huduma na utume.
Kwa upande wake Kardinali Jean-Claude Hollerich, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Luxembourg, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea ili kuwaimarisha katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo, tayari kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Hili ni Kanisa ambalo linaendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani; tayari kuhudumia na kujadiliana; kwa kuendelea kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza, kwani Kristo Yesu alikuja kutumikia na na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mt 20:28.
Naye Sr. Maria Perpétua Coelho Dos Santos, amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kuhusu huduma zinazotolewa na Kanisa kwa wakimbizi na wahamiaji, kiasi cha wakimbizi hawa kujisikia kuwa ni sehemu muhimu ya Kanisa na kwamba, tofauti zao msingi ni changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi kila kukicha. Kijana Diogo Gomes Costa amewashirikisha uzoefu na mang’amuzi yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni iliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno na kwamba, matunda yake yameanza kuonekana kwa vijana wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Mungu kwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Naye Bi Christine Bußhardt amezungumzia kuhusu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika imani, matumaini na mapendo; kwa kujikita katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kusimama kidete kutafuta, kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano. Wanakumbana na changamoto pevu, lakini hawakati tamaam bali wanasonga mbele kwa imani na matumaini. Baada ya sala kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu ameweka shada la maua ya dhahabu kwa Sanamu ya Bikira Maria na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume. Baba Mtakatifu baada ya kuzawadiwa fedha kama mchango wao kwa ajili ya huduma ya mshikamano na upendo, ameziacha kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji nchini Luxembourg.
Mara baada ya mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko ameondoka kuelekea nchini Ubelgiji. Akiwa njiani amemtuma salam za shukrani kwa Mfalme wa Luxembourg kwa mapokezi makubwa, upendo na ukarimu waliomwonesha wakati alipowatembelea. Anapenda kuwahakikishia sala zake, ili Mwenyezi Mungu aendele kuwaimarisha katika umoja udugu wa kibinadamu na amani.