Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Papua New Guinea: Mahubiri Katika Ibada ya Misa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 8 Septemba 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Sir John Guise na kuhudhuriwa na umati mkubwa waamini na watu wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Ujasiri na kamwe wasiogope! Umuhimu wa kumtenga kiziwi na mwenye utasi na kumweka faragha na hatimaye, ni ukaribu wa Kristo Yesu katika muktadha wa kumgusa, kumponya na kumtakasa, ili kutambua kwamba, kila mtu ni mwana mpendwa wa Mungu na kwamba, wao wote ni ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii, Mwenyezi Mungu anawaambia watu wateule na watakatifu wa Mungu kutoka Papua New Guinea wasiogope, kufungua malango ya nyoyo zao kwa Injili ya Kristo, ili waweze kukutana na Mwenyezi Mungu; wawe tayari kufungua nyoyo zao ili kushirikishana upendo kati ya ndugu wamoja. Kamwe asiwepo mtu awaye yote anabaki kiziwi na mwenye utasi katika kuitikia na kuimwilisha changamoto hii. Kristo Yesu awe ni kiini cha maisha yao, tayari kupokea na kumwilisha ndani mwao Habari Njema ya Wokovu, ili hatimaye, wote waweze kumtukuza Mungu kwa kuimba upendo wake usiokuwa na mipaka! Ujasiri na kutoogopa ni ujumbe mahususi kutoka kwa Nabii Isaya, anayewaalika Waisraeli kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwani Mwenyezi Mungu atakuja na kuwakomboa, ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Rej. Isa 35:5.
Unabii huu unapata utimilifu wake kwa Kristo Yesu, anayetumwa na Baba yake wa mbinguni kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; wadhambi wapate toba na maondoleo ya dhambi na wagonjwa wapate kugangwa, kutibiwa na kuponywa, kama inavyooneshwa na Mwinjili Marko: Mk 7: 31-37 anayekazia mambo makuu mawili: Akamtenga yule kiziwi na mwenye utasi, kielelezo cha ukaribu wa Kristo Yesu kwa wenye shida na mahangaiko. Hili ni tukio linalotendeka kwenye viunga vya Dekapoli, pembezoni mwa Yerusalemu, kiini cha Ibada. Huu ni mji uliokuwa pembezoni na wenyeji wake wengi walikuwa ni “wapagani” watu waliokuwa mbali na Mungu. Mtu huyu alikuwa ametengwa na watu wengine kutokana na ulemavu wake; alikuwa ametengwa na ushirika pamoja na urafiki na Mungu pamoja na jirani zake. Hii ndiyo hali inayowakumba waamini pale wanapoelemewa na uchoyo, ubinafsi na woga; chuki na hasira haya ni kati ya mambo yanayomtenga mtu na uwepo wa Mungu na jirani, kiasi cha kushindwa kupata ile furaha ya maisha. Umbali huu unafupishwa na Mwenyezi Mungu kwa ukaribu wa Kristo Yesu anayejitaabisha kuwagusa, kuwaganga na kuwaponya wagonjwa; ni Kristo Yesu anayewakirimia toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi. Mwinjili Marko anasema, “akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi.” Mk 7: 33. Hawa ndio watu wale ambao Mtakatifu Paulo Mtume anasema, Kristo Yesu amekuja kuwatangazia amani. Kwa njia ya ukaribu wa Kristo Yesu, ule umbali kati ya Mungu na jirani, unafupishwa, tayari kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha! Hata leo hii, Kristo Yesu anamwambia kila mwamini “Efata! Yaani “Funguka.” Mk 7:34.
Huu ni mwaliko wa kuondoka kwenye hofu na wasiwasi zinazoziba masikio na kufunga ndimi, ili kushindwa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu na kwamba, wao ni ndugu wamoja! Huu ni wakati wa kumfungulia Mungu na jirani malango ya maisha, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Ni wakati wa kufungua malango ya maisha kwa Kristo Yesu na Imani ya Kanisa, tayari kujenga na kudumisha mawasiliano na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Papua New Guinea katika umoja na tofauti zake msingi. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu, amewaongoza watu wa Mungu kusali Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 8 Septemba, Kumbukumbu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu amewaaminisha watu watakatifu wa Mungu katika hija ya maisha yao katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo “Maria Helpim.” Awasindikize, awalinde na kuwaimarisha katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa familia, awawezeshe vijana kuwa wajasiri, awalinde na kuwafariji wazee, wagonjwa na wale wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu Francisko ameungana na watu wa Mungu kusali kwa ajili ya kuombea amani Barani Asia, Oceania na katika Bahari ya Pacifik. Amani kati ya kazi ya uumbaji, kwa ajili ya kulinda na kutunza kazi ya uumbaji, ili kuwepo na amani kati ya binadamu na kazi ya uumbaji. Bikira Maria Msaada wa Wakristo na Malkia wa amani awasaidie waamini kuongokea mpango wa Mungu unaofumbatwa katika haki na amani kwa ajili ya familia kubwa ya binadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amesikitika kusema kwamba, katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria, Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, nchini Ufaransa yamekumbwa na mafuriko makubwa.
Kwa upande wake, Kardinali John Ribat, M.S.C., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Port Moresby, nchini Papua New Guinea, katika ujumbe wake wa salam, shukrani na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko, ameonesha historia ya uinjilishaji nchini humo, iliyoanza kunako tarehe 29 Septemba 1882 na tangu wakati huo, kumekuwepo na mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume, yanayoendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wakati huu, Papua New Guinea inapofanya kumbukizi ya miaka 142 ya maisha na utume wa Kanisa. Mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu umekumbwa na magumu, vita, mauaji, uharibifu wa mali za watu pamoja na mazingira. Ndiyo maana watu wa Mungu Papua New Guinea wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, upyaisho na uponyaji wa maisha na hatimaye, waweze kujipatia neema na baraka kutoka kwa Mungu. Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo imekuja kwa wakati muafaka, kwa kushiriki pamoja katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa na kwamba, hija hii ya kitume imekuwa na mashiko makubwa kwa watu wa Mungu. Mwishoni wanamwombea Baba Mtakatifu Francisko anapoendelea kutekeleza dhamana na majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.