Tafuta

Baba Mtakatifu katika hotuba yake wa viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia: Amegusia kuhusu mafanikio makubwa ya kiuchumi nchini Singapore. Baba Mtakatifu katika hotuba yake wa viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia: Amegusia kuhusu mafanikio makubwa ya kiuchumi nchini Singapore.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Singapore: Hotuba Kwa Viongozi wa Kisiasa

Papa katika hotuba yake wa viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia: Amegusia kuhusu mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa kujikita katika haki jamii, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; changamoto ni kusimama kidete kulinda na kuwatetea maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga amani na utulivu; Mafanikio ya Singapore katika sekta ya elimu na afya ni mchango muhimui sana kutoka kwa Kanisa kama sehemu ya Uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Baba Mtakatifu nje ya Vatican zinapania pamoja na mambo mengine: kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, Kiutu na Kitamaduni katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji na kama sehemu mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko.  Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kumbukumbu ya Miaka 43 ya uhusiano wa kidiplomasia
Kumbukumbu ya Miaka 43 ya uhusiano wa kidiplomasia

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 ameanza hija yake ya Kitume nchini Singapore, nchi ambayo iko Kusini Mashariki mwa Bara la Asia; hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Umoja na Matumaini”, kielelezo cha umoja, ushirika, maelewano na mafungamano ya kijamii kati ya waamini na ndani ya Kanisa na katika muktadha wa kijamii na mahusiano ya kifamilia. Hija hii ya kitume inadokeza mwanga wa matumaini kwa Wakristo nchini Singapore hasa wale wanaobaguliwa, kuteswa na kudhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 12 Septemba 2024 amekutana kwa faragha na Waziri mkuu mstaafu wa Singapore Bwana Lee Hsien Loong, ametia mkwaju kwenye kitabu cha Wageni Maalum na hatimaye, kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaoziwakilisha Nchi na Mashirika ya Kimataifa pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana nchini Singapore kwa kujikita katika haki jamii, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; changamoto ni kusimama kidete kulinda na kuwatetea maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga na kudumisha amani na utulivu; Mafanikio ya Singapore katika sekta ya elimu na afya, ni mchango muhimu sana kutoka kwa Kanisa kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima kiroho na kimwili; majadiliano ya kidini sanjari na kumbukizi ya Miaka 43 tangu Singapore ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican na mwishoni ni mchango wa Singapore katika medani mbalimbali za Kimataifa, bila kusahau mchango wa familia sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Singapore kwa mapokezi makubwa na kwamba, Singapore ni nchi ambayo iko njia panda kwa ajili ya makutano ya watu, hali ambayo imeiwezesha Singapore kuwa ni kitovu cha maendeleo na biashara na hivyo kuchukua nafasi ya pekee sana katika Jumuiya ya Kimataifa.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Hii ni dhamana iliyovaliwa njuga na kusimamiwa kikamilifu na Waziri mkuu wa kwanza wa Singapore Lee Kuan Yew aliyeiongoza Singapore tangu mwaka 1959 hadi mwaka 1990 na kufanikiwa kuleta mageuzi makubwa nchini Singapore, kiasi cha kuisimika nchi hii katika haki jamii, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu mintarafu elimu na afya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa maendeleo utaweza kuwafikia wananchi wote wa Singapore. Katika mchakato wa maendeleo makubwa kiasi hiki, kuna hatari kwa baadhi ya watu ndani ya jamii kusahaulika, hawa ni maskini na wazee walioshiriki katika mchakato wa kuweka msingi wa maendeleo ya Singapore; bila kuwasahau wakimbizi na wahamiaji wanao changia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa nao wanapaswa kupewa mshahara sawa. Matumizi ya Teknolojia ya akili mnemba ni muhimu sana katika: Kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba isaidie kujenga na kudumisha mafungamano na maelewano ya kijamii; mshikamano kati ya wananchi na kamwe tekenolojia hii isiwe ni chanzo cha utengenano kati ya watu. Baba Mtakatifu ameipongeza Singapore kwa kujenga, kukuza na kudumisha amani na maridhiano nchini Singapore. Huu ni mwaliko wa kuendeleza mchakato wa majadiliano, kila mtu akipewa nafasi ya kuchangia katika utofauti ili kujenga umoja na mshikamano wa “kukata na shoka.” Kumbe, ushirikiano, majadiliano na uhuru wa kuabudu ni nyenzo muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani jamii. Huu ni wito wa kukataa kishawishi cha kutumbukia katika misimamo mikali ya kidini na kiimani; hali ya kutovumiliana, ili kukuza maendeleo endelevu. Mama Kanisa amechangia sana katika kujenga, kukuza na kuimarisha sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Yote haya yametekelezwa katika mwanga wa tunu msingi wa Injili. Kanisa liko mstari wa mbele nchini Singapore katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Papa Francisko akikaribishwa nchini Singapore
Papa Francisko akikaribishwa nchini Singapore

Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani msingi imara wa jamii inayosimikwa katika haki na amani. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Singapore ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 43 tangu Singapore na Vatican zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kwamba, hija hii ya Kitume inapania pamoja na mambo mengine kuwaimarisha Wakatoliki katika imani ili waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, huku wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika ujenzi wa Singapore, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kila mtu akiwa huru kutangaza na kushuhudia imani yake. Baba Mtakatifu anasema, Singapore ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Kimataifa, wito ni kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya ujenzi wa umoja wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Baba Mtakatifu anasema Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia zijengewe uwezo wa kurithisha tunu msingi za maisha, zisaidie kuwafunda vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; ili kujenga na kudumisha umoja wa familia kazi inayopaswa kutekelezwa na taasisi mbalimbali. Baba Mtakatifu ameonya pia kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, kumbe, matumizi bora ya sayansi na teknolojia, karama, vipaji na rasilimali watu, vitu na fesha zisaidie kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Singapore ni nchi ambayo iko mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira bora, mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine duniani. Huu ni wito wa kuendelea kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano; kwa kuwajibika katika ari na mwamko wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; ili kutekeza matamanio halali ya watu wa Mungu nchini Singapore.

Kumbukizi ya miaka 43 ya uhusiano wa kidiplomasia
Kumbukizi ya miaka 43 ya uhusiano wa kidiplomasia

Kwa upande wake, Rais Tharman Shanmugaratnam wa Singapore katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Singapore amesema, imegota miaka 38 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Singapore; amemsifu na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kusimama kidete katika kukuza, kudumisha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika utume kwa vijana wa kizazi kipya, ili kujenga mshikamano na kudumisha amani; tofauti zao msingi ni sehemu ya amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Singapore; ili kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu sanjari na uhuru wa kidini. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mada inayobeba uzito wa juu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni mada ambayo imepewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo nchini Singapore. Amelishukuru Kanisa Katoliki kwa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Singapore na kwamba, Singapore itaendelea kujizatiti katika ujenzi wa jamii shirikishi; kwa kukazia utu, heshima, amani na maelewano kati ya wananchi wake.

Viongozi wa Serikali
12 September 2024, 14:39