Hija ya Kitume ya Papa Francisko Singapore: Majadiliano ya Kidini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji, linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani. Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu anakazia: Umuhimu wa watu kuishi katika umoja, upendo na mshikamano kwa sababu majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu, haki na amani ni mambo msingi ya maisha ya watu wa Mungu. Kwa njia ya majadiliano ya kidini, watu wanakutana, wanazungumza, wanafahamiana na hivyo kuanzisha mchakato wa kutembea bega kwa bega kama ndugu wamoja. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuwa ni shuhuda na chombo cha amani, kwa kufyekelea mbali yale yote yanayosababisha: chuki, kinzani na mipasuko ya kidini na kiimani. Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kuona Kanisa linajikita katika ufukara, kwa kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linataka kuendesha majadiliano na watu wa dini mbalimbali katika mwanga wa Injili, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ushirikiano huu unatambua na kuthamini amana na utajiri wa maisha ya kiroho unaobubujika kutoka katika dini mbali mbali duniani!
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate." Hili ni tamko linalokazia pamoja na mambo mengine: Dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa ajili ya mafao ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbalimbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba: Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 amekuwa akifanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Singapore kuanzia tarehe 11 Septemba hadi tarehe 13 Septemba 2024 imenogeshwa na kauli mbiu “Umoja na Matumaini”, kielelezo cha umoja, ushirika, maelewano na mafungamano ya kijamii kati ya waamini na ndani ya Kanisa na katika muktadha wa kijamii na mahusiano ya kifamilia. Hija hii ya kitume inadokeza mwanga wa matumaini kwa Wakristo nchini Singapore hasa wale wanaobaguliwa, kuteswa na kudhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 13 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na vijana kutoka katika dini mbalimbali, kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki “Catholic Junior College” huku wakiongozwa na kauli mbiu “Vijana wa Kidini Pamoja na Papa Francisko.” Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka vijana kuwa wapembuzi yakinifu, wajenzi wa jamii na wagunduzi wa njia mpya ya maisha; vijana waboreshe akili zao, tayari kutoka katika undani mwao, ili kutangaza na kushuhudia ukweli unaosimikwa katika ujasiri, ushirikishwaji na mang’amuzi. Kamwe vijana wasiogope kuteleza na kuanguka, bali wawe na ujasiri wa kusimama na kuendelea na safari ya maisha. Vijana wawe makini katika matumizi ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii na kamwe teknolojia isiwageuze na kuwafanya kuwa ni watumwa.
Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana nchini Singapore kwa kujikita kikamilifu katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kutambua na kuthamini imani na dini za watu wengine ndani ya jamii. Dini zote zinalenga kumwezesha mwamini kumfikia Muumba wake, yaani Mwenyezi Mungu, ambaye ni wa wote na kwamba, waamini wote ni watoto wa Mungu. Majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa vijana wa kizazi kipya yanahitaji ujasiri mkubwa, ili kuheshimiana na kuthaminiana katika imani zao. Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu “Cyberbullying” ambayo ni aina ya unyanyasaji kimtandao unaoweza kufafanuliwa kama shambulio la kisaikolojia, kimwili au vitisho ambalo hulenga kusababisha woga, mawazo au kumdhuru mwathirika. Unyanyasaji mashuleni huwa katika mazingira ambapo mwanafunzi hujikuta katika unyanyasaji wa kutoka kwa mwanafunzi mmoja au zaidi, kwa nia ya kumuumiza mwanafunzi mwenzao. Tafiti mbalimbali zinahusisha nyanyaso hizi na matatizo ya kisaikolojia ambayo husababishwa na matukio mengi katika maisha ya mtoto ikiwemo: kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi au walezi wake; kwa kulelewa katika familia tenge. Daima lengo la nyanyaso za kimtandao ni kuleta athari kwa wahusika na madhara yake ni makubwa kimwili na kisaikolia; kwa uvumi na taarifa za uongo kuhusu wenzao ili kuwadhalilisha. Uonevu huu unaweza kutokea katika mazingira halisi au katika mtandao kwa kupitia jumbe za simu, baruapepe au kwa njia yoyote ile ambayo watoto huitumia wawapo mtandaoni. Madhara yake huweza kuwa makubwa sana kwa sababu wazazi wengi hawana desturi ya kufuatilia kinachofanywa na watoto wao pale watumiapo mitandao ya kijamii na hufanya mtoto kuathirika kwa kiwango kikubwa.
Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kuachana na tabia ya kuwanyanyasa vijana na watoto na badala yake wajikite katika majadiliano ya kidini na kiekumene yanayofanyika kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Haya ni majadiliano yanayofanyika kati ya vijana wa madhehebu na dini mbalimbali; kati ya vijana na wana siasa. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana wa kizazi kipya kwa ujasiri wao wa kuweza kujadiliana. Amemshukuru Mungu kwa kuwakirimia ujasiri na kwamba, hili ni tukio ambalo limebakiza alama ya kudumu katika maisha yao, watakapokuwa watu wa familia na wazee, wajitahidi kuwafundisha watoto wao umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni amana na utajiri mkubwa, lakini pia ni changamoto ya kuendelea kujikita katika uvumilivu wakati wa kukutana na kubadilishana mawazo. Huu ni ujasiri unaowataka vijana kuchagua urafiki wa kijamii, kupenda, kukuza na kudumisha umoja. Vijana wajifunze kushirikishana kwa vitendo; waondokane na maamuzi mbele kwa kujenga mtandao wa mahusiano na majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuvunjilia mbali kuta za utengano. Vijana waendelee kujikita katika sanaa ya mang’amuzi ya ndani, wakiwa na uwezo wa kupembua mawazo ya wengine; kwa kuwa na matumizi bora ya mitandao ya kijamii na teknolojia ya kisasa. Wajenge utamaduni wa kuthamini Mapokeo na Imani ya watu wengine; wajenge umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; huku wakipendana. Vijana wawe ni kielelezo cha umoja na matumaini kwa taifa.
Kwa upande wake, Kardinali William Goh Seng Chye, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Singapore, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili azungumze na vijana wa kizazi kipya amesema, watu wa Mungu nchini Singapore wanao utamaduni wa kualikana wakati wa Sherehe kuu ili kujenga na kuimarisha mafungamano na urafiki wa kijamii pamoja na utekelezaji wa miradi ya pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kielelezo makini cha mshikamano na faraja. Wanao utamaduni wa vijana kutoka dini na Makanisa mbalimbali kufanya mashindano ya michezo yanayoratibiwa na Wizara ya Utamaduni, Jamii na Vijana. Kuna changamoto zinazotishia amani, usalama na mshikamano wa watu wa Mungu nchini Singapore, kwa kujikita katika kulinda, kudumisha na kuendeleza utu, heshima, haki msingi za binadamu; sanjari na kuhimiza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; malezi na makuzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Naye Bwana Edwin Tong Waziri wa Utamaduni, Jamii na Vijana amekazia kuhusu mchango wa dini katika kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii nchini Singapore na kwamba, dini zinaendelea kuchangia sana katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano na kwamba, dini zina mchango mkubwa katika maboresho ya maisha ya watu wa Mungu nchini Singapore. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kukoleza majadiliano, umoja, udugu pamoja na urafiki wa kijamii ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano na kwamba, Singapore inathamini sana mchango wa Vatican katika kukoleza majadiliano ya kidini. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza shuhuda za vijana katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene mintarafu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, faida na madhara yake. Wamegusia kuhusu changamoto zinazotolewa na vijana wenzao kiasi cha kuwachangamotisha kuhusu kutambua umuhimu wa fadhila ya upendo, mafungamano na urafiki wa kijamii. Wamegusia kuhusu changamoto za ujenzi wa mafungamano ya kijamii nchini Singapore; kwa kuheshimu na kudumisha maisha.