Hija ya Kitume ya Papa Francisko Singapore: Maskini Ni Amana Na Utajiri wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.
Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Singapore, Ijumaa tarehe 13 Septemba 2024 amepata nafasi ya kutembelea Kituo cha Mama Theresa, ambacho kina zaidi ya miaka 90 ili kukutana na kusalimiana na wagonjwa na wazee wanaohudumiwa Kituoni hapo, akiwemo Askofu mkuu mstaafu Nicholas Chia Yeo Joo wa Jimbo kuu la Singapore. Amekutana na kusalimiana na wafanyakazi na watu wanaohudumiwa Kituoni hapo. Baba Mtakatifu amewaambia kwamba, anawakumbuka na kuwaombea. Amewaomba kuliombea Kanisa na watu wote katika ujumla wao. Amewashukuru kwa uvumilifu na sala zao na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.