Baba Mtakatifu yuko nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024. Baba Mtakatifu tarehe 9 Septemba 2024 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, mabalozi na wawakilishi wa vyama. Baba Mtakatifu yuko nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024. Baba Mtakatifu tarehe 9 Septemba 2024 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, mabalozi na wawakilishi wa vyama.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Timor ya Mashariki: Hotuba Kwa Viongozi wa Serikali

Baba Mtakatifu yuko nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024 Tarehe 9 Septemba 2024 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Mabalozi wanaowakilisha nchi na mashirika yao ya Kimataifa nchini Timor ya Mashariki pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu mchakato wa Uinjilishaji wa kina nchini Timor ya Mashariki uliobeba ndani mwake machungu,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano; mafungamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 ameanza hija yake ya kitume nchini Timor ya Mashariki. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Timor ya Mashariki. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu atakuwa nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024.

Papa Francisko akiwa na viongozi wakuu wa Timor ya Mashariki
Papa Francisko akiwa na viongozi wakuu wa Timor ya Mashariki

Baba Mtakatifu tarehe 9 Septemba 2024 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Mabalozi wanaowakilisha nchi na mashirika yao ya Kimataifa nchini Timor ya Mashariki pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu mchakato wa Uinjilishaji wa kina nchini Timor ya Mashariki uliobeba ndani mwake machungu, hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II na matukio ya tarehe 28 Novemba 1975 na Uhuru mwezi Mei 2002; Upatanisho na Indonesia; Tamko Kuhusu Udugu wa Kibinadamu; Changamoto mamboleo ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi, umaskini; majanga jamii; Umuhimu wa Mafundisho jamii ya Kanisa; mafungamano kati ya vijana na wazee. Baba Mtakatifu Francisko anasema mchakato wa uinjilishaji huko Timor ya Mashariki ni juhudi za Wadominikani kwenye Karne ya Kumi na Sita, hawa wakatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Awamu hii ya uinjilishaji imepitia katika kipindi cha machungu, ghasia na umwagaji wa damu.

Mapokezi ya kukata na shoka kwa Papa Francisko nchini Timor ya Mashariki
Mapokezi ya kukata na shoka kwa Papa Francisko nchini Timor ya Mashariki

Kuanzia tarehe 28 Novemba 1975 hadi tarehe 20 Mei 2002, Timor ya Mashariki ikafufuka na kuanza hija ya amani, maendeleo, maboresho ya maisha ya watu; thamani ya rasilimali watu na utajiri wa Timor ya Mashariki; lakini wakati wote huu, watu wa Timor ya Mashariki waliendelea kuwa na matumaini, baada ya kipindi cha giza, mateso na mahangaiko makubwa na hatimaye, amani na uhuru wa watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki. Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989 alikazia umuhimu wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili katika mwanga wa Heri za Mlimani, matumaini kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, msamaha na mapendo. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho wa Kitaifa na Indonesia kwa kujikita katika imani, amani, upatanisho na ushirikiano. Katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 20 ya Uhuru wa Timor ya Mashariki wameamua kumwilisha “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Mazungumzo ya faraha na Rais Josè Ramos Horta wa Timor ya Mashariki
Mazungumzo ya faraha na Rais Josè Ramos Horta wa Timor ya Mashariki

Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amegusia pia changamoto mamboleo zinazowaandama watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki nazo ni: Wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji; umaskini wa hali na kipato; majanga ya kijamii ikiwa ni pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia pamoja na ukahaba, unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, changamoto na mwaliko wa kujikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni msingi imara na madhubuti wa ujenzi wa jamii ya watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki, kwa kuwa na mwono wa matumaini. Timor ya Mashariki asilimia 65% ya idadi ya watu wote nchini humo ni vijana, changamoto na mwaliko wa kuwekeza katika sekta ya elimu katika familia na shuleni, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Vijana na wazee wajenge mahusiano na mafungamano ya dhati, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, Vatican itaendelea kushirikiana na Timor ya Mashariki kadiri Makubaliano ya pande hizi mbili yaliyotiwa mkwaju tarehe 3 Machi 2016.

Hotuba ya Papa Francisko kwa viongozi Timor ya Mashariki
Hotuba ya Papa Francisko kwa viongozi Timor ya Mashariki

Timor ya Mashariki leo hii ni nchi ya amani, utulivu na demokrasia, inayoendelea kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika mshikamano na udugu wa kibinadamu; kwa nchi majirani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Timor ya Mashariki itaendelea kujikita katika kukabiliana na changamoto zake kwa kutumia akili na ubunifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili anayejulikana nchini humo kama “Virgem de Aitara, ili awasindikize katika mchakato wa ujenzi wa Papua New Guinea inayosimikwa katika uhuru, deomkrasia na mshikamano, ili kila mwananchi aweze kuishi katika amani, huku utu wao ukipwa msukumo wa pekee. Rais Josè Ramos-Horta, wa Timor ya Mashariki katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na viongozi wa Serikali na wanadiplomasia amemshukuru baba Mtakatifu kwa kuwatembelea wakati huu, wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu walipojipatia uhuru wa kweli kutoka kwa Wareno, yaani tarehe 25 Aprili 2024. Tarehe 15 Septemba 2024 Timor ya Mashariki inaadhimisha kumbukumbu ya Miaka Ishirini na mitano ya INTERFET na miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipotembelea Timor ya Mashariki, yaani tarehe 12 Oktoba 2024 na kwamba, wameamua kumwilisha “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Baba Mtakatifu Francisko anawatembelea wakati huu, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Timor ya Mashariki. Ameombea amani katika nchi mbalimbali zinazoendelea kuogelea katika vita, mapigano na machafuko.

Viongozi Timor ya Mashariki
09 September 2024, 16:33