Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 10 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na Makleri, Watawa, Majandokasisi na Makatekista waliokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 10 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na Makleri, Watawa, Majandokasisi na Makatekista waliokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.   (ANSA)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Timor ya Mashariki: Hotuba Kwa Viongozi wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amemshukuru Mungu kwa idadi kubwa ya miito mitakatifu kutoka nchini Timor ya Mashariki; amekazia umuhimu wa Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa katika shule ya huduma ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu. Amekazia umuhimu wa utamadunisho wa Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili; amewataka viongozi wa Kanisa kutoka kifua mbele kutangaza Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano; mafungamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 ameanza hija yake ya kitume nchini Timor ya Mashariki. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Timor ya Mashariki. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu atakuwa nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024.

Papa Francisko amepata nafasi ya kukutana na makleri, watawa na makatekista
Papa Francisko amepata nafasi ya kukutana na makleri, watawa na makatekista

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 10 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na Makleri, Watawa, Majandokasisi na Makatekista waliokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amemshukuru Mungu kwa wingi wa miito nchini Timor ya Mashariki, kiasi kwamba, idadi kubwa ya mapadre, watawa, waseminaristi na makatekista ilibaki nje ya Kanisa, changamoto kwa Jimbo kuu la Dili kusoma alama za nyakati na kuangalia uwezekano wa kulipanua Kanisa hili ili kukidhi mahitaji ya nyakati! Makatekista ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Wao wamekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa awali na wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwatayarisha wakatekumeni ili kupokea Sakramenti za Kanisa.

Papa Francisko anamshukuru Mungu kwa zawadi ya miito mitakatifu
Papa Francisko anamshukuru Mungu kwa zawadi ya miito mitakatifu

Makatekista wameonesha umuhimu wa pekee katika kuzisimamia na kuziongoza Jumuiya ndogondogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu. Kwa njia ya mifano bora ya Makatekista kutoka sehemu mbalimbali za Timor ya Mashariki, Kanisa limeweza kuzamisha mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu. Maaskofu mahalia wanapaswa kuhakikisha kwamba Makatekista wanapewa majiundo awali na endelevu: kiakili, kimafundisho, kimaadili na kichungaji, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makatekista ni zawadi kubwa kwa Kanisa mahalia na kwamba, Habari Njema ya Wokovu inapaswa kuwa ni kitovu cha uinjilishaji, kwa kutambua kwamba, wabatizwa wote ni wamisionari, vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu anasema anatambua matatizo, fursa na changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Makleri, watawa, waseminari na makatekista wawe ni mashuhuda wa Injili
Makleri, watawa, waseminari na makatekista wawe ni mashuhuda wa Injili

Kristo Yesu akiwa nyumbani kwa akina Lazaro, Maria na Martha kule Bethania, ukafika wakati ambapo Maria alipotwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi akampaka Kristo Yesu. Rej. Yn 12:1-11. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, harufu nzuri ya Kristo Yesu na Injili inatunzwa na kusambazwa huko Timor ya Mashariki. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, amewajalia waja wake zawadi ya Roho Mtakatifu na kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu waamini wote ni manukato ya Kristo Yesu. 2 Kor 2:15. Haya ndiyo manukato yaliyompelekea Malkia wa Sheba kwenda kumtembelea Mfalme Sulemani. 1 Fal 10: 12. Watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki watambue kwamba wao ni manukato ya Kristo Yesu na Injili yake; ni wafuasi wamisionari waliopakwa manukato ya Roho Mtakatifu ili kuzama katika maisha ya watu watakatifu wateule wa Mungu. Manukato waliyokirimiwa hayana budi kulindwa, kutunzwa na kudumishwa katika upendo na kwamba, manukato haya ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kamwe wasitumbukie na hatimaye kumezwa na malimwengu.

Papa Francisko amesikiliza shuhuda za maisha na utume wa Kanisa
Papa Francisko amesikiliza shuhuda za maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioshuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa maisha ya wakfu, Padre aliyewasindikiza waamini wake wakati wa ukoloni na Shemasi aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, mwaliko wa kulipenda Kanisa na kuendelea kuhifadhi imani na kuendelea kuipyaisha kwa majiundo ya awali na endelevu; kwa kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili, Kitamaduni na Kiutu. Mila, tamaduni na desturi njema zinapaswa kutakaswa mintarafu mwanga wa Mafundisho ya Kanisa. Kila utamaduni na kila kikundi cha kijamii kinahitaji kutakaswa na kukua. Rej. Evangelii gaudium, 69. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linaitwa na kutumwa kwenda kuinjilisha, kwa ujasiri kwa kutambua kwamba, Kanisa daima liko safarini kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuzindua mchakato wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika upatanisho, haki na amani; kwa kuwasaidia maskini na wale wanaoteseka kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Viongozi wa Kanisa wanaojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili
Viongozi wa Kanisa wanaojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili

Baba Mtakatifu amewataka viongozi wa Kanisa nchini Timor ya Mashariki kuwa makini na rushwa na kwamba, manukato ya Injili yasaidie kupambana na mambo yote yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; ulevi wa kupindukia; ukosefu wa heshima kwa wanawake na wasichana. Kimsingi wanawake wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwani wao ndio wanaowahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwa ni akina mama. Kanisa linawahitaji viongozi walioandaliwa barabara, wabunifu katika huduma; watu wanaotambua na kuthamini historia na utamaduni wa watu wao, kamwe wasijisikie kuwa ni bora kuliko watu wao, wasimezwe na kiburi wala uchu wa mali na madaraka na kwamba, utume wao usimikwe katika huduma makini kwa watu wa Mungu; maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza kwani wao ni amana na utajiri wa Kanisa. Mapadre wawe ni vyombo vya baraka, faraja na upendo, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu. Mapadre na watawa wapende ufukara wa Kiinjili na kwamba, manukato ya Injili ni chemchemi ya utajiri na chanzo cha furaha ya kweli. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwambea Mapadre na watawa wazee; watu waliosadaka maisha yao kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa; hawa ni mfano bora wa kuigwa!

Makatekista ni zawadi kubwa kwa Kanisa mahalia
Makatekista ni zawadi kubwa kwa Kanisa mahalia

Kwa upande wake, Askofu Norberto do Amaral wa Jimbo Katoliki la Maliana, na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Timor ya Mashariki, CET., katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko, amekumbushia hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989 iliyoleta baraka, faraja na amani. Timor ya Mashariki ni nchi iliyobarikiwa na idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki Barani Asia na ina idadi kubwa ya vijana, changamoto na mwaliko wa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Mungu Timor ya Mashariki. Baba Mtakatifu alipata fursa ya kusikiliza shuhuda za maisha na utume zilizotolewa na Padre Sancho Amaral, mwenye umri wa miaka 68, Padre wa Jimbo anasema, kunako mwaka 1991 alimsaidia Kamanda Kay Rala Xanana Gusmao kuhama kutoka Dili hadi Ossu, jambo ambalo alilifanya baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, sala, mang’amuzi na ujasiri mkuu. Wakiwa njiani walisimamishwa na askari kutoka Indonesia, lakini walipomwona na vazi la kipadre, wakaruhusiwa kupita. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anajua kuwalinda na kuwatunza waja wake, aliowaita na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu.

Watu wengi walibaki nje ya Kanisa kwa kukosa nafasi ya kuingia ndani.
Watu wengi walibaki nje ya Kanisa kwa kukosa nafasi ya kuingia ndani.

Naye Sr. Florentino de Jesus Martins, mwenye umri wa miaka 89, Katekista katika maisha na utume wake, amewaandaa waamini kupokea Sakramenti za Kanisa; akatembea umbali mrefu ili kutoa huduma, kwa ari na moyo mkuu. Kutokana na umri kuwa mkubwa na changamoto za magonjwa, kunako mwaka 2017 aling’atuka kutoka katika utume wa Ukatekista, lakini anaendelea kutoa ushauri kwa Makatekista vijana. Amekuwa ni Katekista kwa muda wa miaka 56, anamshukuru Mungu kwa msaada na maombezi ya Bikira Maria ameweza kujalia maisha marefu na yenye furaha. Naye Sr. Rosa Sarmento, Fdcc., anamshukuru Mungu kwa uwepo wa umati mkubwa wa watawa wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni wakati wa kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kujenga na kuimarisha umoja, ushirika na utume wa Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, watu wa Mungu kutoka Timor ya Mashariki wanakwenda Barani Ulaya ili kuinjilisha.

Mapadre na Watawa 2024

 

10 September 2024, 15:06