Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Timor ya Mashariki; kielelezo cha utimilifu wa maisha na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Timor ya Mashariki; kielelezo cha utimilifu wa maisha na matumaini.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Timor ya Mashariki: Hotuba Kwa Vijana

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Timor ya Mashariki; kielelezo cha utimilifu wa maisha na matumaini, changamoto kwa vijana hawa ili waweze kuwa ni washindi wa upendo. 1Kor 9: 23-27. Bado Timor ya Mashariki ina kabiliana na changamoto kubwa za ujenzi wa nchi yao, jumuiya na jamii inayosimikwa katika haki, uaminifu, umoja na mshikamano mintarafu mwanga wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka saini kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi.” Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito.” Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Wosia huu wa kitume umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Safari hii ni utekelezaji wa ndoto ya mwaka 2020 kabla ya kuibuka na hatimaye, kusambaa kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Christus vivit ni dira na mwongozo wa maisha na utume kwa vijana
Christus vivit ni dira na mwongozo wa maisha na utume kwa vijana

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 ameanza hija yake ya kitume nchini Timor ya Mashariki. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Timor ya Mashariki. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.”Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Timor ya Mashariki; kielelezo cha utimilifu wa maisha na matumaini, changamoto kwa vijana hawa ili waweze kuwa ni washindi wa upendo. 1Kor 9: 23-27. Bado Timor ya Mashariki ina kabiliana na changamoto kubwa za ujenzi wa nchi yao, jumuiya na jamii inayosimikwa katika haki, uaminifu, umoja na mshikamano mintarafu mwanga wa Injili!

Utume kwa vijana ni kipaumbele cha Kanisa katika ulimwengu mamboleo
Utume kwa vijana ni kipaumbele cha Kanisa katika ulimwengu mamboleo

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu amana na utajiri wao unaobubujika kutoka katika imani, ushuhuda wa kifodini, msamaha na upatanisho unaosimikwa katika tunu msingi za kijamii kama vile uhuru, dhamana na udugu wa kibinadamu. Uhuru wa kweli ni changamoto inayowasukuma kutoka katika uchoyo, ubinafsi na hali ya kujitafuta wenyewe, tayari kujikita katika wajibu na watu huru kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawataka kuwa waangalifu katika maamuzi na vipaumbele vyao vitakavyowasaidia katika mchakato wa ujenzi wa ushirika; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; tayari kujikita katika ujenzi wa amana na ukarimu hasa katika nyakati ngumu! Vijana wanapaswa kusimama kidete kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kuhakikisha kwamba, wanawajibika katika maamuzi yao; kwa kulinda na kuboresha upendo unaojenga mahusiano na mafungamano ya kijamii. Kuwa huru maana yake ni kufanya maamuzi, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi; kwa kuheshimu na kuthamini fadhila ya upendo, hata kama inawagharimu kiasi gani!

Vijana wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Vijana wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Vijana wakumbuke kwamba, nyakati ngumu katika maisha zinaunda watu makini zaidi na kwamba, watu wenye nguvu wanaunda mazingira mepesi na kwamba, mazingira mapesi yanaunda watu dhaifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni dhamana inayowataka kujizatiti kikamilifu katika maisha yao na kamwe wasikubali kuelea katika ombwe na kuzamishwa katika ulaji wa kupindukia. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza kufanya kazi, ili kujenga mazingira rahisi ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha duniani. Nchini Timor ya Mashariki msingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu; ni mambo yanayoendelea kutendeka, changamoto na mwaliko wa kuendelea kufanya mazoezi, ili kujiimarisha zaidi, ili hatimaye, kuweza kupewa taji. Rej. 1 Kor 9: 25. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya nchini Timor ya Mashariki, kujizatiti kikamilifu katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, ambaye hapo awali alitumia nguvu zake nyingi si kwa kujenga na kuimarisha umoja, bali kwa kuharibu na kutenganisha, hadi pale alipokutana uso kwa uso na Kristo Mfufuka akiwa njiani kuelekea Damasko kuwakamata, kuwatesa na kuwaua wafuasi wa Kristo Lakini kwa neema na upendo wa Kristo aliweza kuongoka na hatimaye kuwa ni chombo bora cha ushuhuda wa Kristo Mfufuka, badala ya kuendekeza chuki na kulipiza kisasi, akawa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu; na mtangazaji hodari wa Habari Njema ya Wokovu; na mjumbe wa matumaini, ushirika na upendo. Rej. Fil 3: 7-11.

Vijana wakimsikiliza Baba Mtakatifu Francisko kwa shauku kubwa
Vijana wakimsikiliza Baba Mtakatifu Francisko kwa shauku kubwa

Huu ni mwaliko kwa vijana wote kushindana katika umoja bila kulegeza mwendo, ili kuendelea kuwa ni mashuhuda wa matendo mema. Wasikubali kuathiriwa na mitandao ya kijamii na kamwe wasitumie nguvu kwani wote ni ndugu wamoja na wala wasikubali kutumbukizwa katika vita kwa sababu kilio cha damu ya ndugu zao, kinamfikia Mungu. Rej. Mwa 4:9-10. Vijana wasijijengee maadui kwani kila mmoja wao ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba, maisha ni matakatifu. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma ya Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kipindi cha miaka yote hiyo! Hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kupokea Msalaba katika maisha yao na hatimaye, kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa maboresho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kuangalia tofauti za kikabila, umri, hali ya kijamii au imani ya mtu!

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Injili ya matumaini
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Injili ya matumaini

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika vijana kutoka Timor ya Mashariki kushiriki katika Jubilei ya Vijana Mjini Roma, ili kwa pamoja waweze kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Amewashukuru watu wa Mungu kwa upendo na ukarimu waliomwonesha wakati wote wa hija yake ya kitume nchini mwao!

Vijana Mahujaji wa Matumaini 2027
Vijana Mahujaji wa Matumaini 2027

Padre Francisco Indra do Nascimento, Rais wa Tume ya Vijana Wakatoliki wa Timor ya Mashariki Kitaifa, CNJCTL katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuzungumza na vijana wa Timor ya Mashariki, amempongeza kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya na kwamba, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa vijana nchini Timor ya Mashariki. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo; changamoto kwa vijana kujizatiti kuboresha mazingira, ili Timor ya Mashariki iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi, kwa kuheshimiana na kuendelea kujikita katika: upendo, ujenzi wa udugu wa kibinadamu, urafiki wa kijamii, uzalendo kwa nchi yao sanjari na upendo kwa Kanisa la Kkristo Yesu. Baba Mtakatifu kabla ya kutoa hotuba yake kwa vijana nchini Timor ya Mashariki amepata nafasi ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa vijana wanne yaani: Cecilia Efranio BonaparteIlham Mahfot Bazher; Rogéria dos S. X. Baptista; pamoja na Nelson M. da Conceição. Vijana hawa wamezungumzia kuhusu athari za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika malezi, makuzi na urithishwaji wa imani na tunu msingi za maisha kwa watoto, kiasi kwamba, ndani ya familia ule umoja, upendo na mshikamano vinaanza kutoweka taratibu na kwamba, mawasiliano ndani ya familia yanaanza kusuasua. Vijana wanapaswa kusimama imara katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni wakati kwa vijana kumwilisha ndani mwao Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi.” Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito.”

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila
Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba, binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo. Ni tafakari ambazo zimezingatia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, tiba ya mwanadamu pamoja na maboresho makubwa yanayoendelea kujitokeza katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Viongozi hawa wakuu, walitafakari kwa kina na mapana kuhusu hali na kiwango cha umaskini, vita, kinzani na athari zake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Vijana Timor ya Mashariki
11 September 2024, 15:21