Tafuta

Katika Mwaka wa Masomo 2024-2025 Chuo Kikuu cha Louvain kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake. Katika Mwaka wa Masomo 2024-2025 Chuo Kikuu cha Louvain kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake.   (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Ubelgiji: Jubilei ya Miaka 600 Chuo Kikuu cha Louvain

Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain nchini Ubelgiji. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu kuwa ni mahali pa majiundo ya kiakili na kitamaduni, mahali pa kupanua ujuzi na maarifa; ukomo wa ujuzi unaosababiswa na mchoko wa kiakili, uwezo wa kufikiri na hatimaye, ni neno la shukrani kwa kupanua wigo wa ujuzi na maarifa unaojikita katika uwajibikaji na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024 inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, yaani “Safari na Matumaini.” Chuo kikuu ni mahali pa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini sanjari na mchakato wa malezi mtambuka unaotekelezwa na wadau mbalimbali ndani ya jamii. Hii ni dhamana ya majalimu wa Chuo kikuu, wanaopaswa kuhakikisha kwamba, moto huu unaendelea kuwaka hadi kieleweke. Elimu isaidie kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kujibu maswali msingi yanayotolewa na jamii, bila woga wala makunyanzi. Ukweli, uwazi na ukarimu ni amali za kijamii zinazopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali na kuwathamini wengine, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo.

Majaalimu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain
Majaalimu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain

Chuo Kikuu cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake kwa utashi wa Papa Martin V, katika Waraka wake wa Kitume wa “Sapientie immarcessibilis” uliochapishwa tarehe 9 Desemba 1425. Na hiki kikawa ni Chuo Kikuu cha kwanza cha Kikatoliki duniani. Kumbe, Mwaka wa Masomo 2024-2025 Chuo Kikuu cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake. Chuo kina jumla ya wanafunzi 60, 000 na wafanyakazi ni 10, 000. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu kuwa ni mahali pa majiundo ya kiakili na kitamaduni, mahali pa kupanua ujuzi na maarifa; ukomo wa ujuzi unaosababiswa na mchoko wa kiakili, uwezo wa kufikiri na hatimaye, ni neno la shukrani kwa kupanua wigo wa ujuzi na maarifa unaojikita katika uwajibikaji na matumaini. Baba Mtakatifu anasema, Chuo kikuu kina dhamana ya kuwajengea uwezo wanafunzi nyenzo za kufasiri mambo ya sasa na hivyo kupanga ya mbeleni. Vyuo vikuu ni chemchemi ya mwamko mpya wa maisha ya binadamu na kwamba, Chuo kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kuwa ni chumvi na mwanga wa Injili kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa. Huu ni mwaliko wa kupanua mipaka ya ujuzi na maarifa, ili vyuo hivi viweze kuwa ni chemchemi ya ujuzi na maarifa; mahali ambapo wanafunzi wanapata nyenzo za kufanya upembuzi yakinifu ili kufahamu na hatimaye, kuzungumzia kuhusu maisha, hii ni dhamana na wajibu mkubwa wa Chuo kikuu, tayari kuzama katika kutafuta ukweli, usiokuwa na mipaka.

Louvain ni Chuo Kikuu cha kwanza cha Kikatoliki kuanzishwa ulimwenguni
Louvain ni Chuo Kikuu cha kwanza cha Kikatoliki kuanzishwa ulimwenguni

Baba Mtakatifu anasema ukomo wa ujuzi na maarifa unasababishwa na mchoko wa kiakili. Mchakato wa kutafuta na kuambata ukweli unawataka wahusika kutoka katika undani wao na kuanza kuuliza maswali. Watu wasizame kwenye utamaduni wa “kiteknokrasi”, kwani huu ni utamaduni usiokuwa na “moyo” kiasi cha kushindwa kushangaa, ili hatimaye, kugundua ukweli uliofichika unaogusa maisha na maana yake; hatima ya binadamu na maana yake, ili kumsaidia binadamu aweze kujifahamu vyema zaidi. Hii ni changamoto kwa Vyuo vikuu kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kupanua wigo wa ujuzi na maarifa, ili hatimaye kwa nguvu za Roho Mtakatifu waweze kufikia katika utimilifu wa ukweli: “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yn 16:13. Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anawawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kuendelea kuwasha moto wa tafiti zao, daima wakiwa wazi kupokea changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu amewashukuru wadau wa Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” kwa kuendea kupanua wigo wake na hivyo kujenga mazingira ya ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ili kuwasaidia kusoma na kukua. Ulimwengu unahitaji utamaduni wa kupanua wigo, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wajibu mpana ambayo Chuo kikuu kimekabidhiwa kuutekeleza. Chuo kikuu ni kama “msitu unaowaka” ambao Mwenyezi Mungu anautumia kujifunua. Moto huu unapaswa kuendelea kuwaka kwa kupanua wigo, kwa kuendelea kutafuta ukweli, huku wakijitahidi kujenga na kudumisha utamaduni fungamanishi, wenye huruma na upendo; utamaduni unaosikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama njia ya kupambana na changamoto mamboleo!

Papa Francisko akisalimiana na watu wa Mungu nchini Ubelgiji
Papa Francisko akisalimiana na watu wa Mungu nchini Ubelgiji

Kwa upande wake Prof. Luc Sels, Gambera wa Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko azungumze na Majaalimu, amezungumzia kuhusu changamoto zinazomwandama binadamu katika ulimwengu mamboleo: Athari za mabadiliko ya tabianchi, madhara ya vita na mipasuko ya kijamii; Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Amegusia kuhusu wakimbizi: dhamana na wajibu wa Chuo kikuu cha Kikatoliki kama sehemu ya utekelezaji wa haki jamii na uwajibikaji kwa wakimbizi na wahamiaji; Kanisa katika utekelezaji wa kanuni maadili na utu wema pamoja Chuo kikuu: Hapa amegusia changamoto ya nyanyaso za kijinsia, watu wenye shauku ya mapenzi ya jinsia moja na jinsi ya Kanisa kuwaonesha ukaribu wake, kama kielelezo cha ujenzi wa umoja na tofauti zake msingi, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Kanisa linahamasishwa kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta zinazowagawa na kuwatenganisha watu.

Jubilei ya Miaka 600
27 September 2024, 17:07