Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Ubelgiji: Hotuba Kwa Viongozi wa Kisiasa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024 inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, yaani “Safari na Matumaini.” Huu ni wito na mwaliko wa kutembea pamoja kwenye barabara ambayo ni historia ya nchi ya Ubelgiji, lakini hii ni safari inayofumbata Injili, Njia ya Kristo Yesu, Tumaini letu. Baba Mtakatifu amewasili nchini Ubelgiji jioni tarehe 26 Septemba 2024 na kuelekea moja kwa moja kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Ubelgiji. Ijumaa tarehe 27 Septemba 2024, ameianza siku kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa kilichoko kwenye Ubalozi wa Vatican na baadaye akaelekea kwenye Kasri ya Mfalme wa Ubelgiji huko Laeken kwa mapokezi rasmi. Baba Mtakatifu amekagua gwaride la heshima na baadaye amepata muda wa kuzungumza kwa faragha na Mfalme Filippo Leopold Lodewijk Maria wa Ubelgiji aliyekuwa ameandamana na familia yake. Baadaye, Baba Mtakatifu amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amegusia mchango wa Ubelgiji katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ushirikiano na ushirikishwaji; Ukoloni na Unyonyaji, Ubelgiji ni mwalimu wa maisha sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na mchakato wa kuasili watoto kwa nguvu uliofanyika nchini Ubelgiji kati ya Mwaka 1950 hadi mwaka 1970.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mama Kanisa ataendelea kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Watu wa Mungu waongozwe daima na dhamiri nyofu, kwa kutambua kwamba, Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Baba Mtakatifu anasema, ubora wa nchi haupimwi kwa ukubwa wake kijiografia, lakini kwa kuangalia mchango wake, kama ilivyokuwa nchi ya Ubelgiji katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ushirikiano na ushirikishwaji. Ubelgiji ni nchi ambayo imekuwa ni daraja linalowakaribisha watu, ili kuweza kubadilishana mawazo, na kutafuta kwa pamoja misingi ya amani na utulivu katika makubaliano. Ni daraja linaloragibisha biashara kwa kuunganisha tamaduni katika majadiliano. Hili ni daraja linalowasaidia watu kukataa kishawishi cha kuingia vitani na badala yake, kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani. Bara la Ulaya linaihitaji Ubelgiji, ili kujikumbusha historia yake inayofumbatwa katika watu na tamaduni zao, Makanisa makuu na Vyuo vikuu, mafanikio, pamoja na madhara ya vita yaliyopelekea ukoloni na unyonyaji, Bara la Ulaya linaihitaji Ubelgiji ili kuendelea kujikita katika mchakato wa njia ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kujikita katika kuheshimu mikataba na kuondokana na vita inayosababisha maafa makubwa kwa wat una mali zao. Amani na utulivu ni dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa kwa moyo wa uvumilivu, daima watu wanapaswa kukumbuka mateso, mahangaiko na gharama kubwa za vita.
Baba Mtakatifu anasema, Kanisa la Kristo Yesu linataka kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya matumaini kwa watu wote wa Mungu, ili waweze kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Baba wa milele anayewatakia wema na amani. Waamini wanapaswa kumwangalia Kristo Yesu kwa unyenyekevu na moyo mkuu. Mama Kanisa anataka kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ili kuwawezesha watoto wa Kanisa kuishi Injili katika usafi na utilimifu wake, kwa kuendelea kuwa ni shuhuda wa tunu msingi za maisha. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa.
Kumbe, huu ni wakati wa kuwasikiliza kwa makini waathirika wa nyanyaso hizi, kuwasindikiza katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda yao pamoja na kutekeleza sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso kama hizi zisijitokeze tena ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na mchakato wa kuasili watoto kwa nguvu uliofanyika nchini Ubelgiji kati ya Mwaka 1950 hadi mwaka 1970; hivi ni vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa sheria vilivyosheheni kwa nyakati zile. Kuna watu kwa kusukumwa na dhamiri nyofu walidhani kwamba, walikuwa wanatenda jambo jema kwa Mama na Mwana. Huu ndio ukweli uliojitokeza kwa wanawake ambao walikuwa hawakuolewa kwenye miaka hiyo, kiasi cha kukimbilia kuasili watoto. Kwa bahati mbaya, kuna wanawake ambao hawakupata nafasi ya kuchagua kati ya kuwatunza na kuwalei watoto wao wenyewe au kuwatoa ili waweze kuasiliwa. Mama Kanisa anapaswa kujitambua na kusimama imara dhidi ya tamaduni zinazotawala, ili kulinda na kudumisha tunu msingi za Kiinjili, ili kuepuka mateso na tabia ya ubaguzi; kwa kutafuta na kudumisha amani. Baba Mtakatifu anasali ili kwamba, watu wa Mungu waweze kuongozwa na dhamiri nyofu; kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili waweze daima kuchagua wema.
Kauli mbiu ya Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024 inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, yaani “Safari na Matumaini.” Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesuna kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Ubelgiji kumwomba Mungu ili aweze kuwakirimia kipaji cha matumaini katika safari ya maisha yao.
Kwa upande wake, Mfalme Filippo Leopold Lodewijk Maria wa Ubelgiji katika hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni, amekumbushia hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II, iliyofanyika takribani miaka thelathini iliyopita; mchakato wake katika kutetea utu, heshima, haki msingi za binadamu. Ni kiongozi ambaye ameendelea kujipambanua katika kutafuta na kudumisha amani kama kikolezo cha maendeleo endelevu kwa njia ya huduma makini ya: elimu, afya na haki jamii. Amesimama kwa ujasiri katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa na kwamba, imechukua muda mrefu kwa Kanisa nchini Ubelgiji kuweza kurekebisha kasoro hizi. Ubelgiji imempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na majadiliano na watu katika medani mbalimbali za maisha. Ujumbe wa haki, amani na upatanisho ni changamoto kubwa kwa walimwengu ili kujikita katika Injili ya upendo. Amegusia kuhusu Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” pamoja na mchango wa vyama vya kiraia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Ubelgiji. Mtakatifu Yohane Paulo kunako mwaka 1995 alimtangaza Mtumishi wa Mungu Damian de Veuster, Maarufu kama Damian di Molokai, mmisionari aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa wakoma, kiasi hata cha kupoteza maisha kwa ugonjwa wa Ukoma, huko Hawaii kuwa Mtakatifu.
Naye Waziri mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko mabadiliko makubwa yaliyofanyika nchini Ubelgiji tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipowatembelea, kwa sasa watu wanaishi kwa amani zaidi; huku wakitolea ushuhuda wa imani yao inayomwilishwa katika matendo; Kanisa linaendelea kutangaza Injili ya upendo na kwamba, waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapaswa kusikilizwa; ukweli ufahamike na haki iweze kutendeka kama kielelezo cha kanuni maadili pamoja na kurejesha tena uaminifu kwa Kanisa; daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Ujio wa Baba Mtakatifu nchini Ubelgiji ni kikolezo cha ujenzi wa madaraja na majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha umoja, tayari kupambana na changamoto mamboleo! Baada ya mkutano na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya kiraia na kitamaduni, Baba Mtakatifu amepta fursa ya kutembelea “Home of St. Joseph” Brussels maalum kwa ajili ya wazee, maskini na watu wanaokabiliwa na ukata wa maisha. Hii ni nyumba inayoongozwa na kusimamiwa na Watawa wa Shirika la Dada Wadogo wa Upendo “Piccole Sorelle della Carità.”