Papa Francisko ametia nia ya kutembelea Ubelgiji na Luxembourg kuanzia Alhamisi tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024, Papa Francisko ametia nia ya kutembelea Ubelgiji na Luxembourg kuanzia Alhamisi tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024,  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Ubelgiji na Luxembourg: Uso wa Kristo!

Ni hija inayopania kuboresha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ujasiri wa kukita matumaini na ujasiri wao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee: Zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa binadamu unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya! Ujasiri na Ushuhuda wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mialiko ya viongozi wa Serikali na Kanisa na hivyo ametia nia ya kutembelea Ubelgiji na Luxembourg kuanzia Alhamisi tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024, ili kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi pamoja na hija ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya sanjari na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu. Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji inanogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, huu ni wito na mwaliko wa kutembea pamoja kwenye barabara ambayo ni historia ya nchi ya Ubelgiji, lakini hii ni safari inayofumbata Injili, Njia ya Kristo Yesu, Tumaini letu. Kauli mbiu inayonogesha hija hii ya kitume nchini Luxembourg ni “Pour servir”, inachota amana na utajiri wake kwenye Maandiko Matakatifu yanayomwelezea Kristo Yesu kwamba, hakuja kutumikiwa, bali “kutumika” na kutoa nafsi yake iwe ni fidia ya wengi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa Mama Kanisa kwa kufuata mfano wa Mwalimu wake, anaitwa na kutumwa kuwahudumia walimwengu. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, Baba Mtakatifu ni shuhuda na mjumbe wa Uso wa Kristo!

Hija inapania kukoleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Hija inapania kukoleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Kumbe, hija hii pamoja na mambo mengine, inapania kuwasaidia watu wa Mungu Barani Ulaya kugundua ndani mwao mizizi ya tunu msingi za maisha, ili kuganga na kutibu madhara ya vita, misigano na mipasuko ya kijamii, pamoja na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya. Ni hija inayopania kuboresha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ujasiri wa kukita matumaini na ujasiri wao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee: Zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa binadamu unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Umoja wa Ulaya utaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama utaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya. Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, inayoendelea kushuhudiwa hata leo hii. Kuna umati mkubwa wa watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, njaa na umaskini; hawa ni watu wanaopaswa kuoneshwa mshikamano wa upendo ili kuandika tena ukurasa wa matumaini kwa ajili yao wenyewe pamoja na familia zao. Kumbe, wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani unaotoa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hizi ni tunu msingi zilizobainishwa na waasisi wa Umoja wa Ulaya, lakini ikumbukwe kwamba, mizizi ya tunu hizi ni utamaduni na Mapokeo ya Kikristo yanayozingatia kwa namna ya pekee kabisa: utu wa binadamu, uhuru na haki.

Ubelgiji: Wito wa kutemba pamoja katika mwanga wa tunu msingi za Injili
Ubelgiji: Wito wa kutemba pamoja katika mwanga wa tunu msingi za Injili

Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu kama sehemu ya mchakato unaopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, kila mtu ana haki ya kupata elimu, kwa kuzingatia uhuru wake, lakini Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu kama chimbuko la maisha, historia na ulimwengu katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu kwani elimu ni sawa na bahari haina mwisho, Kanisa limekuwa daima mdau mkuu katika sekta ya elimu, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, elimu inashiriki kikamilifu katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Lovanio, nchini Ubelgiji kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake na kimekuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu yanayojikita katika majadiliano kati ya imani na sayansi; ushirikiano na mshikamano. Huu ni wakati kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Lovanio kugundua tena mahusiano na mafungamano yake kati ya imani na sayansi. Itakumbukwa kwamba, Ubelgiji na Luxembourg ni nchi waasisi wa Umoja wa Ulaya na inasikitisha kuona kwamba, Bara la Ulaya limepoteza dira na mwelekeo wa umoja na mshikamano na kwamba, kuna hatari ya kutumbukia tena kwenye vita kama ilivyotokea Vita ya Pili ya Dunia.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Mwaka 1945 uliandika historia ya Umoja wa Ulaya iliyosimikwa katika matumaini, changamoto na mwaliko kwa Umoja wa Ulaya kujikita tena katika mchakato wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kuonesha ujasiri kwa kukumbatia Injili ya uhai, ili kuondokana na ukame unaopelekea idadi ndogo ya watoto kuzaliwa Barani Ulaya. Tabia ya kujitafutia umaarufu, ubaguzi na hofu anasema Kardinali Parolin ni matokeo ya uchovu wa maisha ya kiroho unaopelekea baadhi ya watu katika jamii kutafuta majibu ya maswali magumu kwa njia nyepesi, kwa kujikita katika misimamo mikali ambayo ni hatari kubwa katika maisha. Hotuba ya Baba Mtakatifu inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na umuhimu wa Msalaba katika maisha, kama sehemu ya mchakato wa kujenga jamii imara zaidi. Ili kupambana na kashfa ya idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya, kuna haja ya kujenga na kudumisha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, sanjari na kuimarisha sera, mikakati na utume kwa familia; kwa kusikiliza changamoto za maisha ya ndoa na familia; kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa watoto wanaozaliwa sanjari na kujikita katika Injili ya matumaini, ili kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi.

Kardinali Pietro Parolin: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Kardinali Pietro Parolin: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Bara la Ulaya linakita mizizi yake katika tunu msingi za Kiinjili zinazoshuhudiwa katika ujenzi wa Makanisa makuu, vyuo vikuu, sanaa na taasisi mbalimbali kama zinavyoonekana kwa sasa. Katiba ya Umoja wa Ulaya haioneshi chemchemi hizi, amana na urithi wake wa kitamaduni, uamuzi ambao hauwezi kulisaidia Bara la Ulaya kusonga mbele. Kumbe, kuna haja kwa Bara la Ulaya kugundua ndani mwake tena tunu msingi zilizopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wa Umoja wa Ulaya, tayari kuzimwilisha bila ya woga na huu utakuwa ni msaada mkubwa kwa Bara la Ulaya kupambana na changamoto mamboleo bila woga. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anahitimisha mahojiano haya maalum kwa kusema kwamba, hii ni hija ya mwanga wa matumaini, unaopania kuzimulikia tunu msingi za maisha Barani Ulaya ili ziweze kuibuliwa na kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu Bara la Ulaya na jinsi ya kuwa Kanisa Barani Ulaya; iwe ni fursa ya kusikiliza na kumwilisha ujumbe wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kufikiri na kutenda mintarafu mwanga na tunu msingi za Kiinjili.

Papa Ubelgiji
25 September 2024, 15:56