Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 amekuwa akifanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 amekuwa akifanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Barani Asia na Oceania: Mahojiano Maalum

Kwa ufupi amezungumzia kuhusu hija yake ya kitume Barani Asia na Oceania; mchakato wa uinjilishaji; upendo wake kwa watu wa Mungu Timor ya Mashariki; Umuhimu wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu, bila kusahau sadaka na majitoleo ya wamisionari katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Mama Kanisa anapenda kuimarisha mafungano na China kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 amekuwa akifanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi amekuwa ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema na kwamba, hija hii, imeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu! Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican Ijumaa tarehe 13 Septemba 2024 alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, amewashukuru kwa kumsindikiza katika hija hii ya kitume, ndefu kuliko zote alizowahi kufanya kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kujibu takribani maswali kumi na saba! Kwa ufupi amezungumzia kuhusu hija yake ya kitume Barani Asia na Oceania lakini kwa kujikita zaidi na nchi ya Singapore na mchakato wa uinjilishaji; upendo wake kwa watu wa Mungu Timor ya Mashariki; Umuhimu wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu, bila kusahau sadaka na majitoleo ya wamisionari katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Mama Kanisa anapenda kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungano na China kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu! Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, dhidi ya utamaduni wa kifo! Watu wa Mungu nchini Marekani wafanye uchaguzi kwa kufuata dhamiri zao nyofu! Vita Ukanda wa Ghaza ni hatari kwa mshikamano na mafungamano huko Mashariki ya Kati. Adhabu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba kashfa ya nyanyaso za kijinsia inapaswa kukemewa na kulaaniwa kwa nguvu zote!

Singapore: Majadiliano ya kidini, kitamaduni na mshikamano wa Kitaifa
Singapore: Majadiliano ya kidini, kitamaduni na mshikamano wa Kitaifa

Baba Mtakatifu amewasifu na kuwashukuru watu wa Mungu nchini Singapore kwa maendeleo yao makubwa, usafi, elimu, majengo makubwa lakini zaidi, maridhiano yanayosimikwa katika majadiliano ya kidini kwa ajili ya kulinda na kudumisha haki msingi, amani na mahusiano mema pamoja na mchakato wa kukuza mila, desturi na tamaduni njema pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Amefurahishwa kuona idadi kubwa ya watoto huko Timor ya Mashariki lakini, nchini Singapore idadi ya watoto ni kidogo zaidi, pengine ni kwa sababu ya maendeleo makubwa, lakini ustawi na maendeleo ya nchi yanategemea kwa kiasi kikubwa idadi ya watoto wanaozaliwa. Baba Mtakatifu amefurahishwa sana ukarimu na upendo wa watu wa Mungu Timor ya Mashariki na kwamba, uhuru wa kuabudu na kidini ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ustawi, maendeleo na amani ya watu wa Mungu. Maendeleo yanapaswa kusaidia mchakato wa maboresho ya watu mahalia, ndiyo maana Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anakazia umuhimu wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu na vipaumbele vyao. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji.

Papa Francisko amevutiwa sana na utamaduni na ukarimu wa Timor ya Mashariki
Papa Francisko amevutiwa sana na utamaduni na ukarimu wa Timor ya Mashariki

Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu ni: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Indonesia inapaswa kujikita katika mchakato wa maboresho ya mahusiano na mafungamano ya watu wake kijamii. Baba Mtakatifu anasema, Papua New Guinea ni nchi ambayo inaendelea kujikita katika maendeleo endelevu ya binadamu na kwamba, alitembelea Jimbo Katoliki la Vanimo na huko amejionea amana na utajiri mkubwa unaosimikwa katika sanaa na utamaduni; sanjari na mchakato wa wamisionari wanaosadaka maisha yao kila siku kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Amana na utajiri wa tamaduni katika mchakato wa uinjilishaji
Amana na utajiri wa tamaduni katika mchakato wa uinjilishaji

Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018. Kwa kutambua umuhimu wake, ukapyaishwa tena tarehe 22 Oktoba 2020 na hatimaye, Oktoba 2022 Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka miwili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linaipatia Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China wachungaji bora na waaminifu watakaotekeleza vyema utume wao. Lengo la Vatican ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Katoliki, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini China. Pili ni kuwapata wachungaji wema, bora na waaminifu watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa liko makini sana katika maisha, historia na maendeleo ya Kanisa nchini China. Baba Mtakatifu anasema, ametia nia ya kutembelea China, Mwenyezi Mungu akimjalia, kwani hii ni nchi yenye utamaduni wa kale, inayokita maisha yake katika majadiliano, demokrasia hata katika tofauti zao msingi na kwamba, Kanisa lina matumaini makubwa na China, ili kukuza na kudumisha misingi ya amani, zitihada za Kanisa zinazoendelezwa na Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI.

Mkataba kati ya China na Vatican ni kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa
Mkataba kati ya China na Vatican ni kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na aina mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao. Maisha ya mwanadamu ni matakatifu na zawadi ya pekee kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utoaji mimba ni kwenda kinyume na utashi wa Mwenyezi Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ya mwanadamu daima yanaonesha uhusiano na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumbaji. Kutokana na ukweli huu, kila tendo linalokwenda kinyume cha uhai wa mwanadamu ni jambo ambalo linapingana na haki na ukweli na hivyo ni kosa pia dhidi ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini, watunga sheria na sera kuhakikisha kwamba, wanathamini zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Hii ni haki msingi kwa kila mwanadamu, inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Hii si zawadi inayotolewa na Serikali kwa wananchi wake, bali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. Serikali zinawajibu wa kulinda na kutetea zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo, katika kila hatua yake ya maisha.

Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.
Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.

Kanisa linapenda kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu ili watu watambue haki msingi za binadamu pamoja na umuhimu wa maadili na utu wema katika sheria na sera zinazotungwa na wanasiasa, ili ziweze kusimamia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Vitendo vya utoaji mimba ni ukatili dhidi ya watoto ambao hawajazaliwa; watoto ambao wana haki zao msingi. Ni jukumu na dhamana ya Serikali kuhakikisha kwamba, zinadumisha utamaduni wa uhai kwa watu wake. Kumbe, sera za utoaji mimba pamoja na kuwakataza wakimbizi na wahamiaji kupata hifadhi nchini Marekani ni makosa yenye uzito, kumbe, wapiga kura nchini Marekani waongozwe na dhamiri nyofu wakati wa uchaguzi mkuu. Kutokushiriki kupiga kura ni kwenda kinyume cha maadili ya kisiasa, kumbe, watu waende kupiga kura kwa kuongozwa na dhamiri nyofu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafuatilia kila siku kuhusu mwenendo wa vita Ukanda wa Ghaza, inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, wito ni kusitisha vita na kuanza kujikita katika msingi wa haki, amani na maridhiano, kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Hija ya Kitume Barani Asia na Oceania imeacha chapa ya kudumu kwa watu
Hija ya Kitume Barani Asia na Oceania imeacha chapa ya kudumu kwa watu

Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Mfalme wa Yordani kwa kukuza na kudumisha amani. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Abbè Pierre ni kati ya viongozi wa Kanisa nchini Ufaransa waliojipambanua kwa kutenda mema kijamii, lakini akatumbukia kwenye kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kashfa hii ya kijamii inapaswa kulaaniwa kwa sababu vitendo hivi ni uhalifu na kashfa kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Lakini ikumbukwe kwamba, tafiti zinaonesha kwamba, asilimia 42% hadi 46% ya nyanyaso za kijinsia zinafanyika ndani ya familia. Ujumbe kwa watu wa Mungu nchini Venezuela ni kujikita katika mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano na kwamba, mara nyingi tawala za kidikteta zimeishia pabaya. Anapenda kwenda nchini Argentina, lakini bado kuna changamoto nyingi zinazoendelea kufanyiwa kazi. Umefika wakati wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Mahojiano Maalum 2024

 

14 September 2024, 15:34