Hija ya Kitume ya Papa Francisko Barani Asia na Oceania: Salam Na Matashi Mema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 13 Septemba 2024 amehitimisha Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi. amekuwa ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Safari hii ni utekelezaji wa ndoto ya mwaka 2020 kabla ya kuibuka na hatimaye, kusambaa kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu amewatumia wakuu wa nchi zalama na matashi mema alipokuwa anapitia katika anga za nchi zao. Hawa ni wakuu wa Singapore ambapo Baba Mtakatifu amemshukuru Rais Tharman Shanmugaratnam na wananchi wote wa Singapore kwa mapokezi makubwa yaliyosheheni ukarimu wakati alipotembelea nchi yao. Anaendelea kuwaombea amani na umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu amewatumia salam na matashi mema wakuu wa nchi za: Malaysia, Thailand, Mynamar, India, Pakistan, Afghanistan, Tajikistan, Uzbekistan, Turkmenistan, Azerbaigian, Georgia, Uturuki, Ugiriki, Albania na hatimaye, Italia. Katika salam zake Baba Mtakatifu amekazia: Baraka, furaha na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; amani, ustawi, maendeleo, ukarimu na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwelezea jinsi alivyofurahi kukutana na Jumuiya za Wakristo zilizosimikwa katika imani, ukarimu; huku zikiendelea kujikita katika tunu msingi za Kiinjili kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kutimiza ndoto ya hija hii ya kichungaji. Anawashukuru watu wa Mungu nchini Italia na anaendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awakirimia ustawi na maendeleo kwa watu wa Mungu nchini Italia.
Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya kuwasili mjini Roma saa 12: 46 za jioni sawa na Saa 1:46 za Usiku kwa saa za Afrika Mashariki alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma ili kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama wakati wote wa hija yake ya kitume Barani Asia na Oceania.