Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Singapore: Misa Takatifu: Fadhila ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema mapendo ni fadhila ya Kimungu inayotuwezesha kumpenda Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake mwenyewe; na jirani kama sisi wenyewe, kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Kristo Yesu aliyafanya mapendo kuwa ni Amri kuu na mpya kwa kuwapenda walio wake upeo, kielelezo cha upendo kati ya Mitume ni kuiga ule upendo wa Kristo Yesu kati yao na hivyo kukaa katika pendo lake na Kristo Yesu ndiye kielelezo cha upendo wenyewe. Mapendo ni tunda la Roho na utimilifu wa sheria. Kristo Yesu anawaamuru wafuasi wake kuwapenda hata adui zao. Bila upendo mwamini si kitu kabisa. Upendo ni sura ya fadhila. Ni chemchemi la lengo la utendaji wao wa Kikristo. Upendo wathibitisha na kutakasa uwezo wetu wa kibinadamu wa kupenda, na huuinua katika ukamilifu wa kiroho wa mapendo ya Kimungu. Upendo humpa Mkristo uhuru wa watoto wa Mungu, huku akijibu mapendo ya yule aliyetupenda kwanza. Matunda ya upendo ni furaha, amani na huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kidugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana, hubaki huru bila kujitafutia faida; ni urafiki na umoja. Utimilifu wa kazi zetu zote ni upendo. Hapo ndipo lilipo lengo. Na kwa ajili ya kulipata nasi twakimbia, twalikimbilia hilo, na mara tufikapo tutapata pumziko letu ndani yake. Rej. KKK 1822 – 1829. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Septemba 2024 ameanza hija yake nchini Singapore, nchi ambayo iko Kusini Mashariki mwa Bara la Asia; ni hija inayonogeshwa na kauli mbiu “Umoja na Matumaini”, kielelezo cha umoja, ushirika, maelewano na mafungamano ya kijamii kati ya waamini na ndani ya Kanisa na katika muktadha wa kijamii na mahusiano ya kifamilia. Hija hii ya kitume inadokeza mwanga wa matumaini kwa Wakristo nchini Singapore hasa wale wanaobaguliwa, kuteswa na kudhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi.
Tarehe 12 Septemba ya kila mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Jina Takatifu la Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kumbukumbu hii ilianza kuadhimishwa kunako mwaka 1513, huko nchini Hispania. Kunako Mwaka 1587 Papa Sixtus V aliihamishia Sikukuu hii tarehe 15 Septemba na Mwaka 1622 Papa Gregori XV, aliidhinisha Sikukuu hii kuadhimishwa mjini Toledo. Na mwaka 1671 Sikukuu hii ikaanza kuadhimishwa nchini kote Hispania na pole pole ikaenea Naples hadi Italia na Hispania katika ujumla wake. Papa Innocent XI akabadilisha tarehe na hivyo kuiweka tarehe 12 Septemba na hatimaye, Mtakatifu Yohane Paulo II akaiimarisha Sikukuu hii kwenye Kalenda ya Kanisa zima. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Jina Takatifu la Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Taifa nchini Singapore, kwa kukazia fadhila ya upendo inayojenga na kuunganisha, bila upendo mwanadamu si mali kitu! Imani ni mwanga angavu unaoangazia upendo huu unaofumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; tayari kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; Upendo unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jina Takatifu la Bikira Maria ni kielelezo cha matumaini na furaha hata wakati wa mateso na mahangaiko, tayari kujibu wito huu, ili kujenga na kudumisha upendo, haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia wito uliotolewa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa kuhakikisha kwamba, waamini wanajenga ushirika katika upendo. Huu ni mwaliko na changamoto kwa watu wa Mungu nchini Singapore kujibidiisha katika majadiliano ya kidini na kiekumene.
Fadhila ya upendo inajenga na kudumisha yale yote yaliyopo. Bila upendo, ni nadra sana kupata maisha, kutenda na kuwa na nguvu za ujenzi. Upendo ni kinyume cha chuki na uhasama, kwani unakita mizizi yake katika mshikamano na ukarimu dhidi ya uchoyo na ubinafsi. Ujenzi ni dhamana inayowashirikisha watu wengi, kila mtu akiwa na dhamana na mchango wake na kwamba, hakuna kinachoweza kudumu pasi na upendo na kwamba, bila upendo, mwanadamu si mali kitu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, imani ni mwanga angavu unaoangazia upendo huu unaofumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Singapore kutangaza na kushuhudia fadhila ya upendo kwa wale wote wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu. Hakuna jengo, amana na utajiri mkubwa au uwekezaji bora zaidi machoni pa Mungu kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kamwe wasiwe ni makwazo kwa jirani zao. Rej. 1Kor 8:13. Waoneshe upendo kwa adui na kwamba, wawe wepesi kusamehe. Rej. Lk 6:27-38. Waamini wakumbuke kwamba, msamaha, imani na matumaini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kama ilivyokuwa kwa watakatifu, wafiadini na waungama imani; watu wanaoakisi huruma na upendo wa Mungu.
Bikira Maria ambaye, Kanisa linaadhimisha tarehe 12 Septemba kumbukumbu ya Jina Takatifu la Bikira Maria, ambaye amekuwa kweli ni kimbilio na matumaini kwa wengi; nyakati za furaha, majonzi na shida katika maisha. Bikira Maria ni kielelezo na ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Bikira Maria ni ushuhuda wa upendo wa kimama, unaofahamu na kusamehe yote, bila kumgeuzia mtu awaye yote kisogo! Ndiyo maana, watu wengi wanakimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama! Mtakatifu Francisko Xsaveri ni kati ya watakatifu wanaopendwa na kuheshimiwa nchini Singapore na mara ya mwisho kuwamo nchini humo ni tarehe 21 Julai 1552, miezi michache tu kabla ya kuitupa mkono dunia! Singapore ni nchi iliyopendwa sana na Mtakatifu Inyasi na Wafuasi wake wa kwanza, waliokuwa wanasukumwa na upendo wa kidugu kujisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Watu wa Mungu nchini Singapore kwa mfano wa Bikira Maria na Watakatifu wa mbinguni wawe tayari kusikiliza na kujibu na hatimaye kumwilisha ndani mwao fadhila ya upendo, haki na amani; fadhila zinazoendelea kuboreshwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Kardinali William Goh Seng Chye wa Jimbo kuu la Singapore, katika hotuba yake ya shukrani baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Amekuwa ni kiungo cha imani na upendo na kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yataendelea kuimarisha kifungo cha umoja, katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; kwa kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wa Kanisa. Ni matumaini yake kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni Sakramenti ya matumaini yanayosimikwa katika upendo, huruma, haki na ushirika. Kardinali William Goh Seng Chye amewashukuru wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Singapore inafanikiwa kwa kiwango cha juu.