Tafuta

Jumanne tarehe 10 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jimbo kuu la Dili, nchini Timor ya Mashariki. Jumanne tarehe 10 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jimbo kuu la Dili, nchini Timor ya Mashariki.   (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Timor ya Mashariki: Mahubiri ya Misa Takatifu Taci Tolu

Jumanne tarehe 10 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jimbo kuu la Dili, nchini Timor ya Mashariki. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; huruma ya Mungu na uponyaji; Mwenyezi Mungu anafanya mwanga wake ung’ae na kwamba, anawaokoa watu wake kwa njia ya zawadi ya Mtoto. Mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika huruma, upendo na neema za Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano; mafungamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 ameanza hija yake ya kitume nchini Timor ya Mashariki. Hiki ni kituo cha tatu cha hija hii inayonogeshwa na kauli mbiu “Que a vossa fé seja a vossa cultura” yaani “Imani yako itokane na utamaduni wako.” Ni himizo na kutia moyo kuishi imani mintarafu utamaduni na mila za watu wa Timor ya Mashariki. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu atakuwa nchini Timor ya Mashariki kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba 2024.

Toba na wongofu wa ndani ni muhimu katika ushuhuda
Toba na wongofu wa ndani ni muhimu katika ushuhuda

Jumanne tarehe 10 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jimbo kuu la Dili, nchini Timor ya Mashariki. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; huruma ya Mungu na uponyaji; Mwenyezi Mungu anafanya mwanga wake ung’ae na kwamba, anawaokoa watu wake kwa njia ya zawadi ya Mtoto. Ujumbe wa Nabii Isaya unatolewa kwa Waisraeli waliokuwa wanaishi mjini Yerusalemu uliokuwa na maendeleo makubwa, lakini pia ulisheheni ukosefu wa kanuni maadili na utu wema; Kulikuwa na umati mkubwa wa maskini wa hali na kipato; ukatili wa kutisha hali iliyokuwa inahitaji toba, wongofu wa ndani pamoja na kujikita huruma ya Mungu na uponyaji. Nabii Isaya anatangaza matumaini na furaha kwa watu wa Mungu; Mwenyezi Mungu atawaangazia nuru kuu itakayowaokoa watu wake kutoka katika lindi la dhambi na mauti, wala hatafanya hivi kwa nguvu za silaha ya vita wala utajiri, bali kwa njia ya zawadi ya Mtoto. Sehemu mbalimbali za dunia, kuzaliwa kwa mtoto ni tukio la mwanga, furaha na sherehe inayoenea katika sakafu ya nyoyo za watu, kwa kuipyaisha ili iweze kurejea tena katika hali yake ya kawaida.

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu

Kuzaliwa kwa Mtoto mchanga ni kielelezo cha matumaini na mshangao mkubwa. Nuru ya Mungu ni kubwa, mwaliko wa pekee ni waamini kushiriki, huruma, upendo na neema za Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu, Neno wa Mungu amekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, changamoto na mwaliko kwa waamini kufungua nyoyo zao kwa upendo na huruma ya Mungu, ili aweze kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu ili kujenga na kudumisha msingi wa maisha ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya katika ngazi mbalimbali. Timor ya Mashariki ni nchi iliyobarikiwa kuwa na watoto na vijana wengi, mwaliko wa kujinyenyekesha mbele ya Mwenyezi Mungu kama anavyofundisha Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat.” Rej. Lk 1:46-49. Mama Kanisa anamwadhimisha Bikira Maria kama Malkia wa Mbingu kwa sababu ni Mama wa Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili aweze kuwa ni ndugu ya waja wake.

Mtoto mchanga ni kielelezo cha matumaini na mshangao wa zawadi ya Mungu
Mtoto mchanga ni kielelezo cha matumaini na mshangao wa zawadi ya Mungu

Bikira Maria alitambua upendeleo huu, akaendelea kubaki kuwa ni mnyenyekevu, katika sala na huduma kwa Kristo Yesu, huku akiendelea kujifunza mambo yale yaliyokuwa yakitendeka katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujinyenyekesha, kwa kusadaka maisha na rasilimali muda ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa jirani; Kristo Yesu kwa njia ya unyenyekevu wake, ameweza kumkomboa mwanadamu, mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha ukarimu, tayari kusimama kidete kuwalinda wanyonge na wasiokuwa na nguvu, ili kila mtu aweze kupata nafasi katika Ufalme wa Mungu. Madini ya “Kaibauk na Belak” yana thamani sana, kielelezo cha nguvu ya Mungu inayotoa maisha na kwamba, kwa njia ya neema na mwanga wa Neno la Mungu, hata waamini wanaweza kushiriki katika utekelezaji wa Mpango wa Mungu katika kazi ya ukombozi. Madini haya ni alama ya amani, uhai na unyenyekevu na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya madini ni alama ya upendo wa Baba na Mama, ufunuo wa Ufalme wa Mungu unaomwilishwa katika huruma na upendo, mwaliko kwa waamini kutafakari upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao.

Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu
Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu

Kwa upande wake Kardinali Virgilio Carmo da Silva, SDB, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dili na Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Maaskofu Katoliki Timor ya Mashariki, CET, katika hotuba yake ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu, amegusia hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili iliyofanyika kunako mwaka 1989 na kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko inapania kuimarisha mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati ya watu wa Mungu nchini Timor ya Mashariki ni kielelezo ukaribu wa Mungu kwa maskini, wanyenyekevu na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ni kielelezo cha upendo na moyo wa kibaba. Hii ni changamoto ya kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kujenga ushirikiano na mshikamano na Serikali; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini. Kwa hakika hija hii ya kitume itaendelea kuacha chapa ya kudumu kwa watu wa Mungu Timor ya Mashariki.

Misa Takatifu Timor
10 September 2024, 15:40