Hija ya Kitume ya Papa Francisko:Lebanon,kila ulinzi usio na uwiano ni kinyume cha maadili
Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko alizungumza Dominika tarehe 29 Septemba 2024 na waandishi wa habari walioambatana naye katika Ziara yake ya 46 ya Kitume kwenda Luxembourg na Ubelgiji wakati wa mkutano wake wa kawaida wa ndani ya ndege. Yafuatayo ni maandishi ya Kiswahili yaliyotafsrisiwa katika mkutano na waandishi wa habari:
Matteo Bruni, Msemaji Mkuu wa Vyombo vya habari Vatican: Kwa wote habari za jioni. Asante, Baba Mtakatifu, kwa muda unaotutolea mwisho wa safari hii fupi lakini nzito sana. Labda ungependa kusema neno kabla hatujaanza na maswali ya wanahabari.
Papa Francisko: Habari za asubuhi. Ninapatikana kwa maswali.
Michael Merten(Luxemburger Wort): Baba Mtakatifu, mimi ni Michael kutoka "Luxemburger Wort", gazeti la Luxemburg, Baba Mtakatifu, Luxemburg ilikuwa nchi ya kwanza, na watu wengi wanakumbuka ziara yako kwenye duka la kahawa. Ningependa kukuuliza kuhusu maoni yako juu Luxembourg na kama kuna jambo lolote lililokushangaza.
Papa Francisko: Asante, ziara yangu kwenye duka la kahawa ilikuwa jambo la ujana. Wakati ujao nitatembelea pizzeria. Luxembourg ilinivutia sana kama jamii yenye usawaziko mzuri, yenye sheria zinazozingatiwa vyema, na vilevile utamaduni tofauti. Hili lilinivutia sana, kwa sababu sikulifahamu. Ubelgiji, kwa upande mwingine, nilijua vizuri zaidi, kwa sababu nimekuwa huko mara nyingi. Lakini Luxembourg ilishangaza kwa sababu ya usawa wake na ukarimu; ni kitu ambacho kilinishangaza. Ninaamini kuwa labda ujumbe ambao Luxembourg inaweza kutoa Ulaya ni huo.
Valerie Dupont (TV ya Serikali ya Kifaransa-Lugha ya Ubelgiji): Baba Mtakatifu, asante kwa kuwezekano wako. Tafadhali samahani sauti yangu, lakini nimenyeshewa na mvua kidogo. Maneno yako kwenye kaburi la Mfalme Baldwin yamesababisha mshangao huko Ubelgiji ...
Papa Francisko: Lakini unajua kwamba mshangao ni mwanzo wa falsafa, na hiyo ni sawa.
Valerie Dupont: Labda. Wengine pia wameiona kama uingiliaji wa kisiasa katika maisha ya kidemokrasia ya Ubelgiji. Mchakato wa kutangazwa mwenyeheri wa mfalme unahusishwa na nyadhifa zake. Na tunawezaje kupatanisha haki ya kuishi na utetezi wa maisha na haki ya wanawake kuwa na maisha bila mateso?
Papa Francisko: Ni kuhusu maisha yote, unajua… Mfalme alikuwa jasiri kwa sababu, akikabiliwa na sheria ya kifo, hakutia saini na akajiuzulu. Hilo linahitaji ujasiri, sivyo? Anahitajika mwanasiasa "halisi" kufanya hivyo. Inahitaji ujasiri. Hata yeye alitoa ujumbe na hili, na alifanya hivyo kwa sababu alikuwa mtakatifu. Yeye ni mtakatifu na mchakato wa kutangazwa mwenyeheri utaendelea, kwa sababu alinipatia uthibitisho wa hili. Wanawake. Wanawake wana haki ya kuishi: maisha yao wenyewe na maisha ya watoto wao. Tusisahau kusema hivi: kutoa mimba ni mauaji. Sayansi inakuambia kuwa ndani ya mwezi wa mimba, viungo vyote viko tayari vimekamilika. Mwanadamu anauawa. Na madaktari wanaojihusisha na hili ni-niruhusu neno wao ni wauaji. Hili haliwezi kupingwa. Maisha ya mwanadamu yanauawa. Na wanawake wana haki ya kulinda maisha. Jambo tofauti ni njia za uzazi wa mpango; hilo ni jambo jingine. Usiwachanganye. Sasa ninazungumza juu ya utoaji mimba tu. Na hili haliwezi kupingwa. Nisamehe, lakini ni ukweli.
Andrea Vreede (TV ya Ubelgiji ya Flemish na Uholanzi): Baba Mtakatifu, katika ziara hii nchini Ubelgiji pia, ulikuwa na mkutano mrefu na kundi la wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia. Mara nyingi katika simulizi zao, kuna vilio vya kukata tamaa kuhusu kukosekana kwa uwazi katika taratibu, milango iliyofungwa, ukimya dhidi yao, ucheleweshaji wa hatua za kinidhamu, siri ulizozungumza leo, na masuala ya fidia kwa uharibifu uliopatikana. Mwishowe, mambo yanaonekana kubadilika pale tu wanapoweza kuzungumza na wewe, ana kwa ana. Huko Bruxessels, waathiriwa pia walitoa maombi kadhaa. Je, unakusudia kuendelea vipi na maombi haya? Na je, haingekuwa bora, pengine, kuunda idara iliyojitolea katika Vatican, labda chombo huru, kama baadhi ya maaskofu wanavyoomba, kushughulikia vyema janga hili katika Kanisa na kurejesha imani ya waamini?
Papa Francisko: Asante. Katika hatua ya mwisho ... Kuna idara huko Vatican, ndiyo. Kuna muundo; kwa sasa, rais ni askofu wa Colombia kwa ajili ya kesi za unyanyasaji. Kuna Tume, na iliundwa na Kardinali O’Malley. Inafanya kazi! Mambo yote yanapokelewa Vatican na kujadiliwa. Hata Vatican nimepokea watu walionyanyaswa, na ninatoa nguvu ya kusonga mbele. Hii ni hatua ya kwanza. Pili, nimesikiliza watu walionyanyaswa. Naamini ni wajibu. Wengine wanasema: takwimu zinaonesha kwamba 40-42-46% ya walionyanyaswa ni katika familia na jirani wa mitaa; na salimia 3% tu katika Kanisa. Sijali kuhusu hilo; Ninawachukulia wale wa Kanisa! Tunabeba jukumu la kusaidia watu ambao wamenyanyaswa na kuwatunza. Wengine wanahitaji matibabu ya kisaikolojia; lazima tuwasaidie kwa hili. Pia kuna mazungumzo ya fidia kwa sababu iko katika sheria za kiraia.
Katika sheria ya kiraia, ninaamini ni euro 50,000 nchini Ubelgiji; hiyo ni ya chini sana. Sio kitu kinachohitajika. Ninaamini kiasi ni hicho, lakini sina uhakika. Lakini ni lazima tuwasaidie watu walionyanyaswa na kuwaadhibu wanyanyasaji, kwa sababu unyanyasaji sio dhambi ya leo hii kwamba labda kesho haitakuwapo. Ni mtindo; ni ugonjwa wa akili, na kwa sababu hiyo, lazima tuwape matibabu na kuwafuatilia. Huwezi kumwacha huru mnyanyasaji ili aishi maisha ya kawaida, akiwa na majukumu katika parokia na shule. Maaskofu wengine walitoa kazi kwa mapadre ambao wamefanya hivyo, baada ya kesi na hatia, kwa mfano, katika maktaba, lakini bila kuwasiliana na watoto shuleni na parokia. Lakini lazima tusonge mbele na hili. Niliwaambia maaskofu wa Ubelgiji wasiogope na wajitahidi kwenda mbele, wasonga mbele. Aibu ni kuficha; hakika hii ndiyo aibu.
Courtney Walsh (TV ya Marekani): Asante sana kwa muda wako. Tumesoma asubuhi ya leo kwamba mabomu ya kilo 900 yalitumika kwa ajili ya kumuua Nasrallah. Kuna zaidi ya elfu moja waliokimbia makazi yao, wengi wamekufa. Je, unafikiri kwamba Israel labda imekwenda mbali sana na Lebanon na Gaza? Na hili linaweza kutatuliwaje? Je, kuna ujumbe kwa watu hawa huko?
Papa Francisko: Kila siku naita parokia ya Gaza. Zaidi ya watu 600 wapo, ndani ya parokia na chuo, na wananiambia kuhusu mambo yanayoendelea, ikiwa ni pamoja na ukatili unaotokea huko. Unachoniambia - Sikujuwa kabisa jinsi ambavyo mambo yamekuwa (yakibadilika.)-lakini ulinzi lazima uwe sawia na shambulio hilo. Wakati kuna kitu kisicho na uwiano, mwelekeo wa kutawala unaopita zaidi ya maadili huonekana. Nchi ambayo, pamoja na majeshi yake, hufanya mambo haya—ninazungumzia nchi yoyote—inayofanya mambo haya kwa njia “ya hali ya juu,” haya ni matendo maovu. Hata katika vita, kuna maadili yanayopaswa kulindwa. Vita haina maadili, lakini sheria za vita zinaonesha maadili fulani. Lakini jambo hili lisipoheshimiwa, unaweza kuona—kama tusemavyo huko Argentina—“damu mbaya” ya mambo haya.
Annachiara Valle (Famiglia Cristiana): Asante, Baba Mtakatifu. Jana, baada ya mkutano katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain, taarifa ilitolewa ambayo, nilisoma, "Chuo kikuu kinachukia misimamo ya wahifadhi iliyotolewa na Papa Francisko kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii." Wanasema kuwa ni vikwazo kidogo kuzungumzia wanawake tu katika masuala ya uzazi, na matunzo na kwamba kwa hakika huu ni ubaguzi kwa kiasi fulani, kwa sababu ni jukumu ambalo pia ni la wanaume. Na kuhusiana na hili, vyuo vikuu vyote viwili vimezungumzia suala la huduma zilizowekwa rasmi katika Kanisa.
Papa Francisko: Kwanza kabisa, taarifa hii ilitolewa wakati nilipokuwa nikizungumza. Iliandikwa kabla, na hii sio maadili. Kuhusu wanawake, mimi huzungumza kila mara kuhusu hadhi ya mwanamke, na katika muktadha huu nilisema jambo ambalo siwezi kusema kuhusu wanaume: Kanisa ni mwanamke; yeye ni bibi arusi wa Yesu. Kulifanya Kanisa kuwa mwanamume, kuwafanya wanawake kuwa wanaume si utu; sio Ukristo. Mwanamke ana nguvu zake mwenyewe. Kwa hakika, wanawake—ninasema daima—ni muhimu zaidi kuliko wanaume kwa sababu Kanisa ni la kike; Kanisa ni bibi harusi wa Yesu. Ikiwa hii inaonekana kuwa ya kuhifadhi kwa wanawake hao, basi mimi ni Carlo Gardell (mwimbaji mashuhuri wa tango ya Argentina na). Kwa sababau haieleweki… mimi ninaona kuna akili finyu ambayo haitaki kusikia kuhusu hili.
Mwanamke ni sawa na mwanaume. Kiukweli, katika maisha ya Kanisa, mwanamke ni bora kwa sababu Kanisa ni la kike. Kuhusu huduma, fumbo la mwanamke ni kubwa kuliko huduma. Kuna Mtaalimungu mkuu ( Balthazar)ambaye alisoma hili, akiuliza ni lipi kubwa zaidi: huduma ya Petro au huduma ya Maria. Huduma ya Maria ni kubwa zaidi, kwa sababu ni huduma ya umoja inayohusisha wengine; nyingine ni huma ya usimamizi. Asili ya kimama ya Kanisa ni asili ya kimama ya mwanamke. Huduma ni huduma ndogo zaidi, inayokusudiwa kusindikiza waamini, daima ndani ya asili ya uzazi. Wataalimungu mbalimbali walijifunza jambo hili, na kusema hili ni jambo halisi; Sisemi kisasa, lakini halisi; haijapitwa na wakati. Madai ya wanawake iliyokithiri, ambayo ina maana kwamba wanawake wanakuwa wanaume haifanyi kazi. Jambo moja wa mfumodume ambao hauko sawa; mwingine ni mfumo kike ambao hauko sawa. Kinachofanya kazi ni Kanisa la kike kuwa kubwa kuliko huduma ya ukuhani. Na hii haizingatiwi mara nyingi. Lakini asante kwa swali. Na asanteni nyote kwa safari hii na kwa kazi mliyofanya. Samahani muda umebanwa hapa. Lakini asante, asante sana. Nakuwaombea; nami mniombee. Omba kwa niaba yangu!
(Papa alikumbushwa juu ya mkasa wa watu hamsini waliopotea baharini katika pwani ya Visiwa vya Canary.)
Papa Francisko: Inaniuma sana kusikia watu hao wote wamekosa Canary. Leo, wahamiaji wengi wanaotafuta uhuru wanapotea baharini au karibu na bahari. Tunaweza kufikiria Crotone, sawa? Mita 100 ... (akizungumza na mwandishi mmoja wa habari). Hebu fikiria hilo. Hili ni jambo la kulilia." Papa alisema. (Hii ni tafsiri na unukuzi uliofanyiwa kazi. Kwa hiyo maneno na misemo katika mabano yanatolewa kwa uwazi.)