Ukristo, historia ya nyuso
ANDREA TORNIELLI
Ukristo sio falsafa, wazo, mwongozo wa kanuni za maadili. Ukristo ni tukio lililounganishwa na mshangao na nyuso. Huko Vanimo na kisha katika kijiji cha mbali cha Baro, Dominika alasiri moja yenye joto sana, tulipata uthibitisho wa hili kwa mara nyingine tena. Kulikuwa na mshangao na shukrani katika nyuso za Miguel De la Calle, Martín Prado na Tomás Ravaioli, wamisionari kutoka Argentina wa Shirika la Neno lililofanyika mwili ambao wanatumia maisha yao kwa furaha kutangaza Injili kwenye viunga vya dunia, katika nchi hii ya ajabu ambayo ina rangi za michoro ya Paul Gauguin.
Kulikuwa na mshangao na shukrani katika uso wa Papa Francisko, ambaye kwa karibu ya umri wa miaka 88, amefungwa kwenye kiti cha magurudumu, alipanda Hercules C130 ya Jeshi la Anga la Australia lililojaa vifurushi vya misaada na zawadi, ili kutimiza ndoto ya muda mrefu ya miaka kumi: ile ya kuwa hapa, pamoja nao na ya kukumbatia kwa macho na mikono ya baba mzee Mjesuit ambaye alikuja kuwa mchungaji wa ulimwengu wote wale wanaume wenye furaha, waliovalia mavazi meupe kama yeye, na juu ya watu wao wote. Wale watu waliojifunza kumjua Mama wa Yesu kutoka katika uso wa “Mama Luján” yaani, Mama Mtakatifu mlinzi wa Argentina.
Ilikuwa ni lazima kumwona Papa Francisko, akiwa ameketi katika chumba kidogo cha nyumba ya mbao iliyofunikwa na vyandarua wanakoishi wamisionari, huku akinywa mate akiwa ameketi karibu nao, baada ya umati wa wanaume, wanawake na watoto waliovaa nguo za rangi nyingi zilizofunikwa na manyoya machache au majani, na miili yenye kupakwa rangi. Kwa miaka mingi, Mrithi wa Petro amekuwa akiwasiliana na watu wa nchi yake ambao wanashuhudia upendo usio na masharti wa Mungu wa Yesu Kristo kati ya watu hawa. Hasa na mmoja wa hawa, Padre Martín, mmisionari huyo kijana, jana hakuwa na neno la kumshukuru rafiki yake ambaye alipinga kila kitu na kila mtu kuweza kuwa hata kwa masaa machache tu na kuona kwa macho yake tamasha la Kanisa lililochanga na changamoto zake elfu zilizopatikana kwa furaha.
Hakuna uhaba wa matatizo huko Vanimo na Baro. Watu wanaishi katika mazingira hatarishi, bila maji ya bomba au umeme, na kuna dawa chache. Vurugu, ukabila na unyonyaji wa utajiri mkubwa wa madini na mbao unaofanywa na mashirika ya kimataifa ni ukweli. Mapadre wa Neno lililofanyika Mwili, kwenye ufuko huu wa Bahari ya Pasifiki ulio katikati ya msitu na miamba ya matumbawe, mnamo 2018 waliunda Bendi iliyoundwa na watoto na vijana. Miongoni mwa tani za vifurushi vilivyosafirishwa na Papa kwenye ndege ya kijeshi pia kulikuwa na ala za muziki (violin na cellos.)
Papa Francisko, akiwa na furaha kama mtoto, aliweza kusikiliza nyimbo kadhaa. Wakati wa kuona tukio hilo mtu hawezi kujizuia kufikiria muujiza wa vile vijiji vya asili vya Paraguay vilivyoandaliwa na Wajesuit, pamoja na shule zao za uimbaji, ule mwangwi wake ambao unabaki katika vitabu vya historia na katika matukio kutoka katika filamu ya “Mission.” Chipukizi ndogo za Injili ambazo huchipuka polepole kati ya tamaduni za mababu na kurudia huruma, ukaribu, upole, upendo usio na masharti kuelekea mwisho wa walio sahaulika.
Maisha yanayotolewa kwa upendo hadi tone la mwisho. Furaha katika nyuso za wazee na watoto wengi wanaotabasamu. Furaha katika nyuso zilizochafuliwa na jua na jasho la wamisionari ambao leo hii wamevaa mavazi meupe kumkaribisha Askofu wa Roma, rafiki yao. Furaha katika uso wa Papa Francisko, ambaye alipanda katika Ndege ya kijeshi ya C130, lakini ambapo angependa kubaki hapa.