Tafuta

TERNA ni Kampuni inayofanya kazi katika sekta muhimu sana ya usambazaji wa umeme unaotumiwa na kila raia kila siku ya maisha yao. TERNA ni Kampuni inayofanya kazi katika sekta muhimu sana ya usambazaji wa umeme unaotumiwa na kila raia kila siku ya maisha yao.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

TERNA: Mtandao wa Mafao ya Wengi Ili Kupambana na Nishati Chafuzi ya Mazingira

Baba Mtakatifu aliwakumbusha wafanyakazi wa TERNA kwamba, wao wanafanya kazi katika sekta muhimu inayoshughulikia ustawi na mafao ya wengi, changamoto ya upyaishaji nishati ya umeme mintarafu kipaji cha ubunifu, kwa kuzingatia ukweli na uwazi bila kusahau umuhimu wa mtandao wa usambazaji wa umeme nchini Italia sanjari na wale wote wanaopoteza maisha wakiwa kazini. TERNA ijikite katika mapambano dhidi ya nishati chafuzi za mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shughuli kuu za Kampuni ya TERNA zinatokana na historia ya Italia ambayo kunako mwaka 1962, Sheria ya 1943 ilifungua njia ya kutaifisha nishati ya umeme, ikikabidhi jukumu la ENEL kwa hatua zote za mlolongo wa usambazaji wa umeme nchini Italia, ambao hapo awali ulikuwa mikononi mwa sekta binafsi. Nguvu inayosukuma mabadiliko ambayo yamesababisha mazingira ya sasa ya kufanya kazi ni mchakato wa kupunguza udhibiti uliokuzwa na Umoja wa Ulaya unaolenga kufanya usimamizi wa gridi kuwa huru. Katika utekelezaji wa Agizo la 79 la tarehe 16 Machi 1999, lililolenga kutenganisha umiliki wa Gridi ya Taifa ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme kutoka kwa usimamizi wa gridi yenyewe kwa kufuata mtindo unaoitwa "Mwendeshaji Huru wa Mfumo wa Umeme" Kampuni mbili mpya zilianzishwa yaani Kampuni ya TERNA mmiliki wa gridi ya upokezi nishati ya umeme nchini Italia, na GRTN (Mwendeshaji wa Gridi ya Taifa ya Usambazaji ya umeme.) ENEL akabaki kuwa ni mbia mkuu.

Wafanyakazi wa Kampuni ya Umeme ya TERNA
Wafanyakazi wa Kampuni ya Umeme ya TERNA

Kumbe Kampuni ya TERNA ni mwendeshaji mkubwa wa mtandao wa usambazaji wa umeme nchini Italia. Wanaendeleza mapitio ya nishati na maendeleo endelevu kwa kuzingatia mahitaji msingi ya watu na ubunifu. Hii ni kazi inayofanyika kila siku ili kujenga mazingira ya mazungumzo na uaminifu katika maeneo, ambapo TERNA inaendelea kujikita katika mafao muhimu kwa maisha ya kila mtu kiuchumi na kijamii. Hivi karibuni viongozi wakuu pamoja na wafanyakazi wa TERNA walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu aliwakumbusha wafanyakazi wa TERNA kwamba, wao wanafanya kazi katika sekta muhimu inayoshughulikia ustawi na mafao ya wengi, changamoto ya upyaishaji nishati ya umeme mintarafu kipaji cha ubunifu, kwa kuzingatia ukweli na uwazi bila kusahau umuhimu wa mtandao wa usambazaji wa umeme nchini Italia sanjari na wale wote wanaopoteza maisha wakiwa kazini. Baba Mtakatifu Francisko amekiri kuhusu mchango mkubwa unaotolewa na Kampuni ya TERNA katika ukuaji wa uchumi wa Italia na Ulaya katika ujumla wake.

Jitihada za makusudi zifanyike ili kuokoa maisha ya wafanyakazi
Jitihada za makusudi zifanyike ili kuokoa maisha ya wafanyakazi

Hii ni Kampuni inayofanya kazi katika sekta muhimu sana ya usambazaji wa umeme unaotumiwa na kila raia kila siku ya maisha yao. Ni katika mantiki hii kwamba, Kampuni inawajibika katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, ni kwa njia ya akili, uwezo, ujuzi na maarifa yao yanayowezesha umeme kupatikana majumbani. Baba Mtakatifu amewakumbuka wafanyakazi ambayo wanapoteza maisha yao wakiwa kazini. Jitihada za makusudi zinapaswa kufanyika ili kupunguza na kama si kumaliza vifo vya wafanyakazi maeneo ya kazi. Baba Mtakatifu ameipongeza Kampuni ya TERNA kwa kuendelea kujikita katika maboresho ya nishati rafiki, katika uzalishaji na ulaji. Kuna nishati chafu inayochafua mazingira nyumba ya wote; nishati inachafuliwa pia na ukosefu wa haki msingi za binadamu sanjari na uwepo wa vita; faida kubwa kwa ajili ya watu wachache ndani ya jamii na hasara kwa wafanyakazi. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanazalisha na kutumia nishati iliyo rafiki kwa mazingira na kwamba, hii ni changamoto shirikishi. Ushirikishwaji na demokrasia ya nishati ni kati ya changamoto mamboleo, mwaliko ni kuwawezesha raia kuwa huru na kamwe wasifungwe na mifumo kandamizi na badala yake, wawe ni jumuiya za nishati rafiki. Hii ni sekta muhimu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya afya za wateja wao na kwamba, wanawajibika vyema kudhibiti kinzani. Watu wajifunze kuratibu na kuthibiti kinzani. Hii ni sanaa ambayo waamini wanapaswa kujifunza, yaani namna ya kudhibiti kinzani na migorogoro ili kamwe vita isitokee.

TERNA inashughulikia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
TERNA inashughulikia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu kinachosimikwa katika majadiliano sanjari na uwezo wa kujadiliana. Ukweli na uwazi ni muhimu sana katika ustawi na ukuaji wa kampuni na namna bora zaidi ya kugawana faida na hatimaye kuchagua vipaumbele katika uwekezaji. Ameipongeza Kampuni ya TERNA kuwa na Kamati ya Maadili ambayo kimsingi inapaswa kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Makampuni na Mabenki makubwa, huku kukiwa na uwezekano wa washiriki kutoka nje. Baba Mtakatifu anasema kwa sasa kuna matumizi ya neno “Mtandao” kielelezo cha umoja, mshikamano na ushirika. Baba Mtakatifu anaishukuru TERNA kwa kuwafungia umeme maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Hiki ni kitendo kilicho pokelewa kwa furaha na moyo wa shukrani, kama muujiza uliokuwa unakoleza maboresho ya maisha yao. Umeme vijijini, ukaboresha maisha ya wanafunzi, watu wakawa na uhakika wa kuwa na maji ya moto kwa matumizi mbalimbali. Hali hii ni tofauti kabisa katika vijiji vingi Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, ambako nyakati za usiku, utaona vikundi vya vijana wakiwa wamekusanyika mahali penye umeme kwa ajili ya kujisomea, kwa sababu wengi wao hawana nishati ya umeme nyumbani kwao. Wakati wa vita, sehemu ya kwanza kushambuliwa ni vituo vya umeme ili kusababisha athari kwa maisha ya watu pamoja na kuharibu ari na mwamko wao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kazi ni kielelezo cha upendo jamii na udugu wa kiraia. Katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao wanatumia akili, nyoyo na upendo wao; mambo yanayopaswa kukumbukwa na hivyo kumshukuru Mungu daima.

Shirika la Umeme la Terna
04 September 2024, 13:51