Tafuta

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec nchini Canada 20 hadi 22 Septemba 2024. Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec nchini Canada 20 hadi 22 Septemba 2024.  (Vatican Media)

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 ya Jimbo Kuu la Quebec, Canada

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Jean-Marc Noël Aveline wa Jimbo kuu la Marseille lililoko nchini Ufaransa kama Mwakilishi wake maalum katika hitimisho la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec, anasema alikubali ombi la ushiriki wake katika maadhimisho haya, ili kuendeleza uaminifu na furaha ya Mungu kwa waja wake. Jubilei ni kipindi cha furaha, toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo kuu la Quebec, lililoko nchini Canada linaadhimisha Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwake. Jubilei hii ilizinduliwa tarehe 8 Desemba 2023 na itahitimishwa rasmi kuanzia tarehe 20 hadi 22 Septemba 2024. Uzinduzi wa maadhimisho haya ulifanyika kwenye Kanisa kuu la kihistoria la “Notre-Dame-de-Québec.” Sherehe hii ya kiliturujia iliwakumbusha waamini matendo makuu ya Mungu toka mwanzoni mwa historia ya ukombozi wa binadamu. Baada ya dhambi ya Adam na Eva, Mungu hakutaka kuwaacha binadamu peke yao katika maovu. Kwa sababu hiyo alimtazama Bikira Maria na akamfikiria kwa upendo, na akataka awe Mama wa Mkombozi wa wanadamu. Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu akajibu kwa msamaha kamili. Huruma ya Mungu itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima. Siku hii Mlango Mtakatifu wa Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec ulifunguliwa. Kumbe, ni Mlango wa Huruma ya Mungu, ambao kwa njia yake yeyote aingiaye ataonja mapendo ya Mungu: anayefariji, anayesamehe, na anayewapatia waamini tumaini. Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec ni kipindi cha Mwaka Mtakatifu unaosimikwa katika toba na wongofu wa ndani; ni wakati wa kujitafutia rehema kamili, neema na baraka katika maisha. Ni kipindi cha hija takatifu za maisha ya kiroho na kwamba, kuanzia Mwezi Julai 2023 hadi Mwezi Oktoba 2024 Mlango wa Huruma ya Mungu utafunguliwa.

Jubilei ya Miaka 350 ya Jimbo kuu la Quebec, Canada
Jubilei ya Miaka 350 ya Jimbo kuu la Quebec, Canada

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Jean-Marc Noël Aveline wa Jimbo kuu la Marseille lililoko nchini Ufaransa kama Mwakilishi wake maalum katika hitimisho la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec, anasema alikubali ombi la ushiriki wake katika maadhimisho haya, ili kuendeleza uaminifu na furaha ya Mungu kwa waja wake. Anamtaka Kardinali Jean-Marc Noël Aveline katika maadhimisho haya awe ni shuhuda na chombo cha faraja na furaha ya Mungu katika maisha yao. Huyu ni mtu anayefahamu fika dhamana na maisha ya kichungaji; ndiyo maana Baba Mtakatifu anasema kwa hakika Kardinali Jean-Marc Noël Aveline ni shuhuda anayestahili kumwakilisha, kielelezo cha tumaini la watu wa Mungu. Mbegu ya neno la Mungu ilipandwa, kwa neema na msaada wa Kimungu iliweza kukua na hatimaye, kuzaa matunda mengi. Jumuiya ya waamini ikazaa matunda ya imani ya Kikatoliki inayoendelea kukua hadi wakati huu.

Jubilei iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha upatanisho wa kitaifa
Jubilei iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha upatanisho wa kitaifa

Maadhimisho ya Jubilei hii, ni mwaka uliowekwa wakfu kwa msingi wa Kanisa kuu la ajabu, washiriki wote  wa Jubilei hii watambue kwamba, kama vile vitu vyote vilivyoumbwa vimeelekezwa kwa Mwuumba wao, wanapaswa kujielekeza wenyewe kwa Mungu, ukweli wa kwanza na wema wa juu zaidi. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa kuwatakia heri na baraka watu wote wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Quebec wanaoshiriki katika maadhimisho haya ya Jubilei ya miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec, nchini Canada. Anamhimiza kutimiza kwa bidii wajibu aliokabidhiwa, ili watu wa Mungu waweze kukirimiwa amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho wa Kitaifa.

Jubilei ni kipindi cha furaha, toba na wongofu wa ndani
Jubilei ni kipindi cha furaha, toba na wongofu wa ndani

Inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Yakobo Mtume alizikwa Kanisani humo. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo kuu la Quebec, tarehe 8 Desemba 2023, Baba Mtakatifu Francisko, aliwatakia heri na baraka katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Quebec. Hili ni jimbo la kwanza kabisa kuanzishwa nchini Canada. Baba Mtakatifu akawaweka watu wa Mungu Jimbo kuu la Quebec chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.   Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala ambayo kimsingi ni chemchemi ya baraka na neema zote.

Quebec Miaka 350
19 September 2024, 13:31