Tafuta

Wakimbizi na wahamiaji ni mashuhuda wa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo, anayeweza kugeuza ubaya na ukosefu wa haki na kuwa ni chemchemi ya ustawi, wema na mafao ya wengi. Wakimbizi na wahamiaji ni mashuhuda wa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo, anayeweza kugeuza ubaya na ukosefu wa haki na kuwa ni chemchemi ya ustawi, wema na mafao ya wengi. 

Kilio cha Wakimbizi na Wahamiaji ni Ujenzi wa Udugu wa Kibinadamu

"Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.” Mwa 4:9-10. Mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto inayowataka walimwengu kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, au kuwageuzia kisogo wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Papa Francisko katika maisha na utume wake, wakimbizi na wahamiaji ni kipaumbele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni katika muktadha wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, hivi karibuni, Baba Mtakatifu ameandika dibaji kwenye kitabu kilichotungwa na Don Mattia Ferrari kijulikanacho kwa lugha ya Kiitalia “Salvato dai migranti. Racconto di uno stile di vita.” Kitabu hiki kimechapishwa na “Edizioni Dehoniane Bologna, EDB.” Ni kitabu kinachosimulia maisha ya Padre mhudumu wa maisha ya kiroho anayetekeleza dhamana na utume wake kwenye Bahari ya Mediterrania, kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta leo na kesho yenye matumaini, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao.

Wakimbizi na wahamiaji wanalilia ujenzi wa udugu wa kibinadamu
Wakimbizi na wahamiaji wanalilia ujenzi wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ametoa kipaumbele kwa wakimbizi na wahamiaji na kwamba, hija yake ya kwanza ya kichungaji aliifanyia kwenye Kisiwa cha Lampedusa, mji maarufu kwa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ulioko Kusini mwa Italia kwani hapa ni mahali wanapopokelewa na kupewa hifadhi. Baba Mtakatifu anasema, walimwengu wanaulizwa swali la msingi kabisa “Kisha BWANA akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui, Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.” Mwa 4:9-10. Mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto inayowataka walimwengu kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, au kuwageuzia kisogo wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Undeni Tume ya Haki na Amani Majimboni na Parokiani
Undeni Tume ya Haki na Amani Majimboni na Parokiani

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mbele ya macho ya walimwengu kuna njia panda: ile inayoelekea katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika jumuiya ya kibinadamu; na kwa upande mwingine ni utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; na kuendelea kushuhudia damu ya watu wasiokuwa na hatia ikimwagika kwenye Bahari ya Mediterrania: Hii kimsingi ni njia panda ya utamaduni wa utu na udugu wa kibinadamu au utamaduni usioguswa na mateso ya wengine, kiasi kwamba, kila mtu anatenda kadiri anavyojisikia! Baba Mtakatifu anasema, katika miaka hii ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amebahatika kukutana na kuzungumza na idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji na kati yao, wametajwa katika Kitabu hiki. Hawa kimsingi ni ndugu wanaowasaidia watu wengine kugundua udugu wa kibinadamu na hivyo kujikita katika utamaduni wa ukarimu na upendo na kwamba, urafiki na maskini unaokoa kwani kwa njia yao, watu wanakutana na upendo wa Kristo Yesu anayeteseka kati ya ndugu zake walio wadogo na hivyo kuwawezesha kugundua kwamba, hata wao ni sehemu kubwa ya uzuri wa udugu mpana wa binadamu, kwa sababu wakimbizi na wahamiaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si tatizo wala mzigo wa kutua.

Kuna watu wanatafuta leo na kesho yenye matumaini.
Kuna watu wanatafuta leo na kesho yenye matumaini.

Wakimbizi na wahamiaji ni mashuhuda wa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo, anayeweza kugeuza ubaya na ukosefu wa haki na kuwa ni chemchemi ya ustawi, wema na mafao ya wengi na hivyo kila mmoja wao anakuwa ni daraja linalowakutanisha watu kutoka katika tamaduni na dini mbalimbali na hivyo kugundua utu wao kama binadamu. Udugu wa kibinadamu ni kilio cha wakimbizi na wahamiaji wanaopiga hodi ili utu, heshima na haki zao msingi ziweze kutambulika na kuheshimiwa, tayari kujenga udugu wa kibinadamu na utamaduni wa upendo. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha yao huko Baharini na Jangwani. Mama Kanisa yuko imara katika mchakato wa kuwasindikiza wakimbizi na wahamiaji kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu anayependa na kuota ndoto ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili watu wengi zaidi waweze kushiriki katika utume huu, tayari kujenga na kudumisha jumuiya inayojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia maskini, ili kujenga na kudumisha demokrasia; utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha hatima ya binadamu.

Utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine
Utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na utume wake, amekwisha kushiriki mikutano mikuu minne ya Kimataifa mintarafu wakimbizi na wahamiaji. Hii ni changamoto kwa kila Jimbo na Parokia kuanzisha Tume ya Haki na Amani, ili kujenga mtandao wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji na hivyo kuwawezesha watu wa Mungu kuendelea kukutana na kujadili kuhusu mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji katika maeneo yao. Wakimbizi na wahamiaji ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni ndoto ya Mungu na changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican chini ya uongozi wa Mtakatifu Yohane wa XXIII.

Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kuteteta haki za wakimbizi duniani.
Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kuteteta haki za wakimbizi duniani.

Kardinali Loris Capovilla, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwake, alipata chakula na wakimbizi pamoja na wahamiaji wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka Afrika ya Kaskazini, aliwapongeza kwa kuendelea kuchangia katika ujenzi wa utamaduni wa upendo dhidi ya utamaduni wa teknolojia, nguvu na silaha. Watu wote ni sawa kama walivyo mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, kazi ya uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kila mtu anayo sehemu ya uzuri, changamoto na wito wa kutembea kwa pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo; umoja, ushirika na mshikamano wa udugu wa familia kubwa ya binadamu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja na Kristo Yesu ni Mkombozi wa wote na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa wote. Macho ya watoto wa Mungu yanaelekezwa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele!

Wakimbizi na wahamiaji
22 September 2024, 09:28