Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa kuanzia tarehe 8 hadi 15 Septemba 2024 Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa kuanzia tarehe 8 hadi 15 Septemba 2024  (ANSA)

Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa & Miaka 150 ya Wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu

Maadhimisho yanaanza tarehe 8 hadi tarehe 15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, mwaliko kwa waamini kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tabia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu inategemea kujishusha kwa Mwenyezi Mungu kumwelekea mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni “Mwili mmoja” (1Kor 10:17) na hivyo kuunganishwa katika uwepo mmoja. Katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kwa hakika, upendo kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani ni umoja wa kweli: Mwenyezi Mungu aliyefanyika mwili huwavuta wote kwake (Rej. Papa Benedikto XVI “Mungu ni upendo 13-14). Huu ni upendo unaowazamisha waamini katika tanuru ya upendo wake usiokuwa na mwisho (Rej. Desiderio desideravi, 57), ambayo katika ishara ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inadhihirisha kwa ufasaha sana taswira ya upendo huo wa milele Huu ni mwaliko wa kujenga udugu wa kibinadamu ili kuuponya ulimwengu, kwa kutambua kwamba, kama jamii moja ya wanadamu ni wasafiri, wanaofanywa kuwa ni mwili mmoja, kama wana wa dunia ile ile inayowakaribisha binadamu wote licha ya tofauti zao za kiimani, kidini, kitamaduni na ki-hali ili kuweza kufufua zawadi ya Mungu ndani mwao. (Rej. 1 Tim 1:6).

Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa na Miaka 150 Moyo Mtakatifu wa Yesu
Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa na Miaka 150 Moyo Mtakatifu wa Yesu

Mataifa yote yanapaswa kutambua kwamba, ni ndugu wamoja; udugu unaopata chimbuko lake kutoka katika upendo kwa Ekaristi Takatifu unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja wanaowajibika kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu. Hii ni sehemu ya barua kutoka kwa Baba Mtakatifu aliyomwandikia Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Caracas, nchini Venezuela. Baba Mtakatifu ameridhia kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) yaadhimishwe Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador. Maadhimisho haya yanaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya.

Udugu wa Kuponya Ulimwengu: Nanyi nyote ni ndugu. Mt 23:8
Udugu wa Kuponya Ulimwengu: Nanyi nyote ni ndugu. Mt 23:8

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo wa Mungu tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwa sasa Kanisa nchini Ecuador linataka kupyaisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu katika maisha na utume wake, ili kuganga na kuponya nyoyo za watu waliojeruhiwa kwa matukio mbalimbali katika maisha yao. Haya ni matukio makuu katika maisha na utume wa Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu kwa ajili ya kunogesha mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda tayari kupyaisha imani inayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko anamwambia Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Caracas, nchini Venezuela kuwakumbusha waamini kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha, utume na umoja wa Kanisa. Ni mahali pa kuweza kukutana na kumpokea Kristo Yesu katika Neno na katika Ekaristi Takatifu, ili kuambata amana  na utajiri unaobubujika kwa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya kiroho. Anamtaka awafikishie salam na matashi mema, watu wa Mungu wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria wa El Quinche, waamini wote waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uponyaji wa Ekaristi Takatifu kwa Ulimwengu. Amemwomba pia aweze kuwafikishia watu wa Mungu baraka zake za kitume, wote wanaoshiriki Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa, ahadi ya Upatanisho na Matumaini yote.

Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu
Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu

Itakumbukwa kwamba, Kongamano la Ekaristi Kimataifa kufanyika Amerika ya Kusini ilikuwa ni mwaka 2004 kule Guadalajara. Baada ya Miaka 20 Kongamano linarejeshwa tena Amerika ya Kusini. Lengo ni kuhakikisha kwamba, matunda ya Ekaristi Takatifu yanasaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kupyaisha imani ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Huu ni mwaliko kwa waamini kuanza maandalizi mapema ili kuendelea kudumisha uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu lipewe nafasi yake katika maisha na vipaumbele vya waamini, kwa kujitahidi kumwilisha matendo yake Maadhimisho yanaanza tarehe 8 hadi tarehe 15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya.  Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo wa Mungu tarehe 25 Machi 1874.

Kongamano la Ekaristi 2024
06 September 2024, 14:19