Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Jimbo kuu la Quito, nchini Ecuador. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Jimbo kuu la Quito, nchini Ecuador. 

Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa: Ujumbe wa Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Jimbo kuu la Quito, nchini Ecuador anakazia: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu msingi wa ulimwengu mpya unaosimikwa katika haki na utu; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika Ekaristi Takatifu; Ujenzi wa ushirika katika sala kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC 24) Jimbo kuu la Quito, nchini Ecuador yamezinduliwa rasmi Dominika tarehe 8 na yatafikia kilele chake tarehe 15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo wa Mungu tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwa sasa Kanisa nchini Ecuador linataka kupyaisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu katika maisha na utume wake, ili kuganga na kuponya nyoyo za watu waliojeruhiwa kwa matukio mbalimbali katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Ufunguzi wa Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa
Ufunguzi wa Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho haya anakazia: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu msingi wa ulimwengu mpya unaosimikwa katika haki na utu; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika Ekaristi Takatifu; Ujenzi wa ushirika katika sala kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, waamini wanaweza kuendelea kushangazwa na Fumbo la Ekaristi Takatifu uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai. Huu ni ukimya uliofichwa kwenye Tabernakulo. Kumbe, udugu wa kibinadamu ni msingi wa ujenzi wa ulimwengu mpya unaosimikwa katika haki na utu. Ekaristi Takatifu inaamsha ari na mwamko wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kutembea kwa pamoja hata kama ni wengi lakini ni wamoja katika Mwili mmoja, Mkate mmoja na hivyo kuweza kukua kwa pamoja kama Kanisa linaounganishwa pamoja kwa Maji ya Ubatizo na kutakaswa kwa Moto wa Roho Mtakatifu.

Kauli mbiu: Udugu wa Kuponya Ulimwengu. Nanyi Nyote ni Ndugu Mt 23:8
Kauli mbiu: Udugu wa Kuponya Ulimwengu. Nanyi Nyote ni Ndugu Mt 23:8

Huu ni udugu unaobubujika kutoka katika muungano na Mwenyezi Mungu, unaosagwa pamoja ili kutengeneza Mkate, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu; ambao waamini wanaushiriki kikamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na mkutano wa watakatifu wa Mungu. Udugu wa Kiekaristi hauna budi kupyaishwa, kwa kuwa na ushirika kamili na Kristo Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, jambo la hatari lakini muhimu, kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Altare na kukomunika. Huu ni mwaliko kwa waamini kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu mara kwa mara, ili kupata kifungo cha Ekarisri Takatifu kinacholiunganisha Kanisa na Mwenyezi Mungu, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, mateso ya mwamini mmoja ni sawa na mateso ya Mwili wote mzima. Kumbe, waamini wanaalikwa na kuhamasishwa kuwa kama Simeoni wa Kirene aliyemsaidia Kristo Yesu kuubeba Msalaba wake, akielekea Mlimani Kalvari huku akiwa amebeba mwilini mwake mateso na mahangaiko ya binadamu wa nyakati zote, ili kuuponya ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujifunza somo hili na kuendelea kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaokita mizizi yake kwa Mungu na kati ya watu. Waamini watambue kwamba, wao ni wamoja katika Kristo Yesu chemchemi ya maisha yao; tayari kushiriki katika huduma ya uponyaji wa ulimwengu, Kristo Yesu awabariki na Bikira Maria wa El Quinche awalinde na kuwafunika kwa joho lake.

Kongamano la Ekaristi Takatifu 2024 Ecuador
08 September 2024, 16:05