Tafuta

Maadhimisho Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2024 huko Yaounde nchini Cameroon kuanzia tarehe 9 hadi 10 Septemba 2024 Maadhimisho Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2024 huko Yaounde nchini Cameroon kuanzia tarehe 9 hadi 10 Septemba 2024   (ANSA)

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani 2024

Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2024 huko Yaounde nchini Cameroon kuanzia tarehe 9 hadi 10 Septemba 2024 Papa anakazia: Umuhimu wa elimu na Maadhimisho yananogeshwa na kauli mbiu "Kukuza elimu kwa lugha nyingi: kusoma na kuandika kwa maelewano na amani", huu ni mwaliko wa kutafakari mchango wa kusoma na kuandika katika mchakato wa kudumisha umoja, mafungamano ya kijamii na uelewa wao wa pamoja. Lugha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani “International Literacy Day” yaliasisiwa kunako mwaka 1965 katika mkutano wa Mawaziri wa Elimu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliokuwa wamekutanika huko mjini Teheran nchini Iran. Mawaziri hao wakapendekeza kuanzishwa kwa Siku ya Kupamba na Ujinga Duniani kwa kuhimiza dhana ya usomaji endelevu. Wazo hili liliibuliwa kutokana na kiwango kikubwa cha watu wasiojua kusoma na kuandika duniani. Kunako mwaka 1966, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), lilitangaza kwamba, tarehe 8 Septemba ya kila mwaka ni Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani. Lengo ni kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la ujinga duniani. Hata leo hii, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado kuna umati mkubwa wa watu wasiojua kusoma na kuandika! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 773 ambao hawakubahatika kupata elimu ya msingi.

Tarehe 8 Sept. ni Siku ya kupambana na ujinga duniani.
Tarehe 8 Sept. ni Siku ya kupambana na ujinga duniani.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya maadhimisho Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2024 huko Yaounde nchini Cameroon kuanzia tarehe 9 hadi 10 Septemba 2024 anapenda kukazia umuhimu wa elimu katika maisha ya watu. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu "Kukuza elimu kwa lugha nyingi: kusoma na kuandika kwa maelewano na amani", huu ni mwaliko wa kutafakari kwa kina na mapana mchango wa kusoma na kuandika katika mchakato wa kudumisha umoja, mafungamano ya kijamii na uelewa wao wa pamoja.

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na ujinga
Siku ya Kimataifa ya Kupambana na ujinga

Vatican inapenda kuipongeza UNESCO katika kukuza na kudumisha anuwai ya lugha na tamaduni, bila kusahau ile ya lugha nyingi. Watu wanaofahamu lugha nyingi ni amana na utajiri mkubwa kwa jamii, ni watu wanaothamini utajiri wa tamaduni mbalimbali. Kumzungumzisha mtu katika lugha anayoifahamu ni sawa na kuzungumzisha katika akili na moyo wake. Lugha ni chombo mahususi cha mawasiliano katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kuondokana na mawazo mgando sanjari na maamuzi mbele. Ni chombo kinachochea majadiliano na mchakato wa watu kukutana. Huu ni mwaliko kwa watunga sera na wadau wa elimu kujizatiti kikamilifu katika kupambana na ujinga duniani, ili hatimaye, kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika msingi wa elimu, udugu, mshikamano na amani, ili hatimaye, kuondokana na hofu ya mashambulizi ya silaha na badala yake kukoleza kifungo cha udugu wa kibinadamu.

UNESCO 2024
09 September 2024, 15:27