Masikitiko ya Papa kwa watoto zaidi ya 17 waliuawa na moto huko Kenya
Vatican News
Masikitiko makubwa yalioneshwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua iliyotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin iliyotumwa kwa Askofu Mkuu Antonio Muheria wa Nyeri, nchini Kenya, kwa sababu ya moto ambao watoto zaidi ya 17 wamepoteza maisha katika Shule ya Bweni ya Hillside Endarasha na karibu wengine 70 hawakupatikani wakiwemo wafanyakazi.
Ukaribu wa kiroho wa Papa
Baba Mtakatifu Francisko katika salamu zake ameonesha ukaribu wake wa kiroho kwa "wale wote wanaoteseka na athari za mkasa huo, hasa kwa majeruhi na familia zinazoomboleza.” Kwa hiyo, Papa “anazikabidhi roho za marehemu katika huruma ya upendo ya Mwenyezi Mungu” akitoa "sala zake kwa wale wote wanaojishughulisha na kutoa msaada na kuomba baraka za Bwana ili awape nguvu, amani na faraja."
Siku tatu za maombolezo
Moto huo katika Shule ya Msingi ya Bweni ya Hillside Endarasha ulizuka muda wa saa sita usiku, siku ya Alhamisi 5 Septemba 2024 kwenye shule hiyo ya bweni ambapo zaidi ya watoto 150 walikuwa wamelala. Shule hiyo, ambayo inakaribisha wanafunzi 800 wenye umri kati ya miaka 9 na 12 au 13, iko katika eneo la nusu vijijini, takriban kilomita 170 kaskazini mwa mji mkuu Nairobi, Kenya. Kwa mujibu wa Mamlaka, watu 14 walijeruhiwa, huku watoto 70 wakiwa bado hawajapatikana, ingawa hii haimaanishi kuwa wamekufa au kujeruhiwa. Rais William Ruto hata hivyo alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Jumatatu kwa kile alichokiita “msiba usiofikirika.”