Mfuko wa Uchumi wa Papa Francisko: Mashuhuda! Wasiogope! Matumaini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, kwa kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Huu ni uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuchochea mchakato wa mageuzi ya kiuchumi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili dunia iweze kuwa na uchumi unaojikita katika misingi ya haki; uchumi fungamani au shirikishi bila kumwacha mtu awaye yote, kuchechemea nyuma ya maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa bahati mbaya uchumi mamboleo unaoendelea kukumbatia utamaduni wa kifo, uharibifu wa mazingira pamoja na kuwakatisha watu tamaa ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa na kuanza kuelekezwa ili kujenga uchumi unaofumbatwa katika misingi ya: haki, udugu wa kibinadamu, masuala fungamani pamoja na kuhakikisha kwamba, maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanawezeshwa kikamilifu, ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Hii ndiyo dhana ya uchumi unaojikita katika huduma ya upendo wa dhati, ili kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi wakati wa ujana wake, aliposigana na maamuzi ya Baba yake mzazi na kuamua kuambata tunu msingi za Kiinjili na hivyo kuyapatia kisogo malimwengu, leo hii ni mfano bora wa kuigwa katika kutafuta na kudumisha amani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na huduma kwa maskini, matendo makuu ya Mungu.
Kanuni maadili ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ujirani mwema, ni kati ya mambo msingi yaliyovaliwa njuga na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anataka kuunganisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unaojikita katika Ikolojia na uchumi fungamani. “Uchumi wa Francisko” ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu mkakati wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto endelevu iliyotolewa na vijana wakati wa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawajengea vijana uwezo wa kupambana na changamoto za maisha pamoja na kuendelea kuwachangamotisha wale vijana wanaojipambanua katika ujenzi wa misingi ya uchumi fungamani, yaani uchumi unaofumbatwa katika udugu wa binadamu na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Malezi na majiundo makini ya vijana ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu! Huu ni uchumi jamii unaojikita katika huduma kwa binadamu, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki zake msingi.
Ni uchumi unaofafanuliwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Wosia wake wa Kitume: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Ni uchumi unaoratibu matumizi ya rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wafranciskani katika umaskini wao, wakasukumwa kuwashirikisha maskini utajiri unaobubujika kutoka katika sadaka na majitoleo yao ya kila siku. Wafranciskani ni waasisi wa dhana ya uchumi fungamani na utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya matumaini, kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, usawa, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati.
Ni katika muktadha wa “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko”, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Septemba 2024 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Uchumi wa Francisko unaopania pamoja na mambo mengine; kuhakikisha kwamba sera na mipango hii inatekelezwa, ili kupyaisha uchumi kwa kufuata sera na mbinu mkakati inayotolewa na Baba Mtakatifu, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa na Maandiko Matakatifu yanayomfuasa Kristo Yesu ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alikazia umuhimu wa kuwa ni: Mashuhuda, Kamwe wasiogope na wawe na matumaini pasi na kuchoka wala kujikatia tamaa. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kuwa karibu zaidi na vijana, ili kuwasaidia waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kufuata njia nyoofu, ili kuepuka mabaya! Uchumi wa Kimataifa unahitaji mabadiliko ya dhati, kwa kuupenda uchumi katika mwanga wa Mungu unaofumbata tunu msingi za Kiinjili, wema na chemchemi ya moyo wa Kiinjili kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekuwa ni Mtoto wa mfanya biashara wa “kutupwa” alifahamu fika mazuri na madhara ya ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto ya kupenda sera na mikakati ya uchumi; kuwapenda na kuwaheshimu wafanyakazi na maskini pamoja na kutoa kipaumbele cha pakee kwa wale ambao wako katika shida, mahangaiko na magumu ya maisha.
Mtakatifu Francisko wa Assisi katika maisha na utume wake, alivua utu wake wa kale, akajivika upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na hivyo kutoa mwelekeo mpya wa maendeleo ya kiuchumi. Sera na mbinu mkakati wa “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni zile zilizo fikiwa kwenye Konventi ya Assisi tarehe 24 Septemba 2022, ushuhuda wa maisha ndio unaoleta mvuto sanjari na kuendelea kuwa thabiti katika maamuzi yao, kwa kurithisha tunu msingi za Kiinjili na kwa hakika hata uchumi utaweza kubadilika na kuwa mzuri zaidi. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kutokuwa ni viongozi wa woga na wasiwasi, bali wajasiriamali ambao wako tayari kutoka nje, tayari kumwilisha ndoto ya matumaini kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa historia anaiwezesha dunia kusonga mbele. Waendelee kutumaini pasi na kuchoka wala kujikatia tamaa. Watambue kwamba, biashara inayowaingizia watu faida kubwa kwa sasa ni biashara ya silaha, inayokita mizizi yake katika utamaduni wa kifo. Katika mwelekeo huu, demokrasia inatishiwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutaka kujimwambafai na kujikweza, hali ambayo inapelekea kukosekana kwa usawa. Wasiogope kwani Mwenyezi Mungu atawasaidia na kamwe Kanisa halitawaacha peke yao. Vatican itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na wajumbe hawa na kwamba, ushirikiano kama huu wataupata pia kutoka katika Makanisa mahalia, yaliyoonea sehemu mbalimbali za dunia na hivyo kujenga mtandao wa ushirikiano. Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, litaendelea kuusindikiza Mfuko wa “Uchumi wa Francisko”, ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu huu. Huu ni wajibu wa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi.