Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina: Kielelezo Cha Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina alizaliwa tarehe 25 Mei 1887. Akafariki dunia tarehe 23 Septemba 1968 huko San Giovanni Rotondo, Kusini mwa Italia. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 2 Mei 1999 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri na hatimaye, tarehe 16 Juni 2002 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu na ni kati ya watakatifu wanaopendwa na wengi kwa nyakati hizi na Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 23 Septemba. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kichungaji Jimbo Katoliki la Benevento, Italia kunako tarehe 17 Machi 2018, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 50 tangu Padre Pio wa Pietrelcina alipofariki dunia na miaka 100 tangu alipopata bahati ya kuwa na Madonda Matakatifu. Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kuwashukuru wote kwa moyo wao wa ukarimu waliomwonjesha siku ile, akapata bahati ya kukutana na kuzungumza na wagonjwa mbalimbali na kwamba, ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika moyo wake. Hili ni tukio ambalo lilikuwa na umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa; ikawa ni nafasi ya kuweza kufafanua na kuzama zaidi katika maisha ya kiimani mintarafu Mafundisho ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina: maisha ya sala, unyenyekevu na hekima!
Huyu ni Mtakatifu aliyekuwa na imani na matumaini thabiti kwa Mwenyezi Mungu; akajitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watu wake; akalipenda na kuliheshimu Kanisa licha ya matatizo na changamoto zote alizopitia katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini, Mama Kanisa anao watoto wake ambao wanaogelea katika lindi la dhambi! Mtakatifu Padre Pio alilipenda Kanisa, kiasi hata akapewa neema ya kusamehe na kusahau! Haiwezekani kuendelea kuishi ndani ya Kanisa kwa kulishutumu Kanisa kila kukicha kama anavyofanya Shetani, Ibilisi! Waamini wawe na ujasiri wa kuonesha udhaifu na mapungufu ya Kanisa, lakini pia walipende, waliheshimu na kulijenga Kanisa. Makosa yarekebishwe kwa toba na wongofu wa ndani ili Kanisa lisonge mbele!
Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumpenda na kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika uhalisia maisha yao, ili kwa njia ya upendo huo, aweze kuwaletea maisha mapya, kwa kujisadaka zaidi kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Upendo wa Kimungu unasaidia mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, amani upendo na mshikamano. Kwa mfano na maombezi ya Mtakatifu Padre Pio, waamini wasichoke kujiaminisha kwa Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia upendo, wema na huruma yake isiyokuwa na kifani! Baba Mtakatifu anawatuma waamini kumshuhudia Kristo kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuishi na kutenda kama Wakristo; kwa kujenga na kudumisha urafiki na upendo kati ya watu, ili kufyekelea mbali “ndago za uadui na roho mbaya” ili hatimaye, kukuza na kudumisha udugu badala ya vita na mipasuko ya kijamii!