Nia za Baba Mtakatifu Kwa Mwezi Septemba 2024 Kilio cha Dunia Mama Iliyojeruhiwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki imeadhimishwa tarehe 1 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kusikiliza Kilio cha Dunia Mama Iliyojeruhiwa kwa kujikita katika haki ya mazingira na nishati rafiki.” Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015, kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, 2015-2016. Baba Mtakatifu aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa majadiliano ya kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Dunia Mama na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 1 Septemba 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji wa Kazi ya Uumbaji Duniani, anasema, anatumaini kwamba, kutoka kwa kila mtu, taasisi, vyama, familia na kila mtu, kujitolea madhubuti kwa ajili ya utunzaji bora wa nyumba ya wote. Kilio cha Dunia Mama iliyojeruhiwa kinazidi kutisha na kinahitaji hatua madhubuti na za haraka. Haki ya mazingira bora, safi, salama, yenye afya, tija na endelevu pamoja na sheria zilizopo za kimataifa na inathibitisha kwamba utangazaji wake unahitajika sanjari na utekelezaji kamili wa mikataba ya Kimataifa ya utunzaji bora wa mazingira. Haki ya mazingira pia inatambua kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi, usimamizi na matumizi yasiyo endelevu ya maliasili, uchafuzi wa hewa, ardhi na maji, usimamizi usiofaa wa kemikali na taka, sanjari na upotevu unaosababishwa na viumbe hai huingilia kati watu kufurahia haki hii na kwamba, uharibifu wa mazingira una athari mbaya, za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kwa kufaidika kwa haki zote za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwenyezi Septemba 2024 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema “Kusikiliza Kilio cha Dunia Mama Iliyojeruhiwa.” Kuna kilio cha maskini wanaoathirika kutokana na majanga asilia wanaolazimika kuyahama na kuyakimbia makazi yao; Ukame wa kutisha, moto wa nyika; kuyeyuka kwa barafu na kuongezeka kwa kina cha bahari; dhoruba za maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, uchafuzi mkubwa wa mazingira ni chanzo kikuu cha ongezeko la magonjwa ya dharura na vifo vya ghafla, hatimaye, ni kupungua na kutoweka kwa anuwai ya kibaiolojia. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo pamoja na mtazamo mpya kuhusu ulaji, ili kuokoa mazingira nyumba ya wote. Jumuiya Kimataifa isikilize na kujibu kilio cha Maskini na Dunia Mama, ili kuweka uwiano mzuri kati ya binadamu, mazingira na Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote! Uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote ni janga linalogusa masuala ya kijamii na linahitaji majadiliano ya kina, uwajibikaji wa kila mtu na jamii katika ujumla wake, ili waweze kuwa na afya bora kwa kuishi katika mazingira bora na fungamani kwa maisha ya binadamu. Haki na wajibu ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko. Pale ambapo binadamu anageuka kuwa ni mtawala wa kazi ya uumbaji na kuanza kuchafua na kuharibu mazingira nyumba ya wote anakuwa ni chanjo cha majanga makubwa katika maisha yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kujizatiti katika mapambano dhidi ya umaskini, ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kubadili tabia, mitindo na mifumo ya maisha. Tumaini na kutenda pamoja na uumbaji wakati wa kazi ya uumbaji.
Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu anasema, mwanadamu amegeuka kuwa ni chanzo cha maafa yake, badala ya kuwa mlinzi na mtunzaji bora wa mazingira amegeuka na kuwa mmiliki wa kazi ya uumbaji, chanzo cha fedheha. Kwa upande wake, Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu kusali na kujibidiisha katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Naye Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika ujumbe wake katika Siku ya Kuombea Utunzaji wa Kazi ya Uumbaji Duniani kwa mwaka 2024 anasema, athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika imani, itakayowahamasisha kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote.
Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuelimishwa juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ikolojia kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chanzo, asili na hatima ya kazi yote ya uumbaji, tangu kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili ya wokovu wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatambua na kuenzi tunu msingi za maisha ya binadamu sanjari na kazi ya uumbaji; tayari kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anatoa mwaliko wa ushirikiano na mshikamano wa dhati kati ya Makanisa, waamini wa dini mbalimbali, ili kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote; maskini na mazingira wakipewa kipaumbele cha kwanza. Utunzaji bora wa mazingira na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni sawa na chanda na pete. Hii inatokana na ukweli kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kuwaathiri maskini zaidi katika jamii. Kumbe, hata kuna umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa sababu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya haki jamii.