Tafuta

Burkina Faso Burkina Faso  (AFP or licensors)

Papa alaani shambulio la kigaidi huko Burkina Faso

Baada ya sala ya Malaika wa Bwana,Papa Francis alilaani vikali uvamizi wa hivi karibuni wa kutisha wa wanamgambo wa kijihadi katika nchi hiyo ambao uligharimu maisha ya watu wasiopungua 200,wakiwemo wanawake na watoto wengi.Mnamo Agosti wanamgambo wa itikadi kali walifanya vitendo viofu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatfu akiendelea mwishoni mwa sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe Mosi Septemba 2024 alieleza masikitiko yake kuhusu shambulio baya sana la kigaidi lililokumba kijiji kimoja nchini Burkina Faso Juma moja lililopita. Papa alilaani kitendo hicho na kueleza ukaribu wake kwa taifa zima:  “Nilihuzunika kujua kwamba Jumamosi tarehe 24 Agosti , katika manispaa ya Barsalogho, Burkina Faso, mamia ya watu, miongoni mwao wakiwa ni  wanawake na watoto, waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi. Katika kulaani mashambulio haya mabaya dhidi ya maisha ya binadamu, ninatoa ukaribu wangu kwa taifa zima na rambirambi zangu za dhati kwa familia za wahanga. Bikira Maria awasaidie wapendwa wa Burkina Faso kupata amani na usalama.”

Shambulio la wanajihadi 24-25 Agosti

Nchini Burkina Faso mnamo tarehe 24 na 25 Agosti ilikuwa eneo la mashambulizi mawili mabaya zaidi ya kigaidi katika historia ya nchi hiyo, ambayo yaligharimu maisha ya zaidi ya watu 200; lakini karibu 300 ndiyo waathiriwa wote kulingana na vyanzo visivyo rasmi. Shambulio la tarehe 25 Agosti, ambalo ni la umwagaji damu zaidi, lilitekelezwa na karibu wanajihadi mia moja ambao walivamia mji wa Barsalogho, kilomita 30 kaskazini mwa, mji mkuu wa mkoa wa Kati-Kaskazini. Kati ya wathirika takriban 200 (140 waliojeruhiwa) walikuwa wanawake, watoto na wazee. Shirika la Msaada kwa Kanisa Hitaji  linathibitisha kwamba ni karibu watu  22 kati ya waliokufa walikuwa waamini Wakristo. Kwa mujibu wa habari, kutokana na shuhuda za watu walionusurika, shambulio hilo lilichukua muda wa saa kadhaa na kuanza wakati wanajihadi zaidi ya 100 walipojitokeza wakiwa kwenye pikipiki na kuwafyatulia risasi raia na wanajeshi waliokuwa wakichimba mitaro ya kujihami ili kujikinga na mashambulizi hayo ya kigaidi .

Umoja wa Mataifa ulishutumu shambulio hilo

Mauaji ya mjini Barsalogho, yanayodaiwa na kundi lenye uhusiano na al-Qaeda, pia yalilaaniwa katika siku za hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, ambaye aliyeonesha mshikamano wake na mamlaka ya mpito katika mapambano yao dhidi ya ugaidi akiwahimiza ili kuhakikisha kwamba wale waliohusika na vitendo hivi vya kudharauliwa wanawajibishwa.

Shirika la ACN linaripoti shambulio lingine dhidi ya Jumuiya ya Kikristo

Siku iliyofuata, Dominika tarehe 25 Agosti 2024, wanamgambo wa Kiislamu walishambulia kijiji cha Sanaba, katika Jimbo la Nouna, magharibi mwa nchi. Kulingana na ripoti ya  Shirika la Kimataifa la Msaada wa Kanisa Hitaji (Acs,) Kundi kubwa la wapiganaji lilizunguka jamii, walikusanya idadi ya watu na kuwafunga wanaume wote wenye umri wa zaidi ya miaka 12 wa dini ya Kikristo na ya jadi na, kwa ujumla, wale ambao walichukuliwa kuwa wapinzani wa itikadi ya jihadi. Kisha magaidi hao waliwapeleka wanaume hao kwenye Kanisa la Kiprotestanti lililo karibu na kuwachinja 26 kati yao, na kuwatia ndani Wakatoliki kadhaa.

Moto wa vurugu za kimsingi

Kwa ujumla, nchini Burkina Faso, mwezi mzima wa Agosti ulikuwa na ghasia za wafuasi wa kiitikadi kali wa Kiislamu. Hapo awali, mashambulizi mawili ya kigaidi yalitekelezwa katika jimbo la Nayala, eneo la Boucle du Mouhoun. Mnamo Agosti 4, watu wenye silaha waliingia katika kijiji cha Nimena, na kuwateka nyara zaidi ya wanaume 100 wenye umri wa kati ya miaka 16 na 60, ambao hawajulikani waliko kwa sasa. Baadaye, tarehe 20 Agosti, vyanzo vya ndani viliripoti kwa AACS mashambulizi katika vijiji vya Mogwentenga na Gnipiru, ambapo sehemu ya wakazi walikimbia.

Papa alaaani Shambulio la kigaidi huko Burkina Faso
01 September 2024, 15:47