Papa akumbuka waathiriwa wa kimbunga na mafuriko na kuomba amani penye vita
Na Angella Rwezaula – vatican.
Mara baada ya tafakari yake ya Katekesi tarehe 18 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha masikitiko kuhusiana na hali ya hewa mbaye inayoendelea katika maeneo mbali mbali duniani. Papa amesema “Katika siku za hivi karibuni, mvua kubwa imenyesha katikati mwa Ulaya, na kusababisha waathirika, kukosa watu na uharibifu mkubwa. Hasa, Austria, Romania, Jamhuri ya Czech na Poland zinalazimika kukabiliana na usumbufu wa kutisha unaosababishwa na mafuriko. Ninawahakikishia kila mtu ukaribu wangu, nikiwaombea hasa wale waliopoteza maisha na familia zao. Ninashukuru na kutia moyo jumuiya za Wakatoliki na mashirika mengine ya kujitolea kwa misaada wanayotoa.”
Kila tarehe 21 Septemba ni Siku ya Alzheimer Duniani
Baba Mtakatifu Francisko aidha amesema “Jumamosi ijayo, tarehe 21 Septemba itaadhimishwa Siku ya Alzheimer Duniani hivyo: tuombe kwamba sayansi ya matibabu hivi karibuni iweze kutoa matarajio ya matibabu ya ugonjwa huu na kwamba hatua zaidi na zinazofaa zaidi zianzishwe ili kusaidia wagonjwa na familia zao.”
Salamu za Papa kwa Wabenedikitini na Abati mpya
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea amesema “Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Hasa, ninasalimu Mkutano wa Maabati wa Shirikisho la Wabenediktini [linasema Kusanyiko] na, huku nikimtakia Abate mpya kazi njema - huyu ni kijana eh? “ Abate Rais aliyechaguliwa katika siku hizi, ninahimiza kila mtu kujitolea kwa upendo na msukumo wa kimisionari ili kuifanya roho ya Wabenediktini kuwa muhimu zaidi ulimwenguni.”
Wakarmeli walei
Baba Mtakatifu akiendelea amesema kuwa “Kisha ninawasalimu Walei Wakarmeli na kuwasihi wawe chachu ya Injili, hasa kuwafikia walio hatarini zaidi kuwa ishara ya Kanisa linalotoka nje daima.”
Kongamano la Jumuiya ya Ulaya ya Upasuaji
Salamu zangu za dhati pia ziende kwa washiriki katika Kongamano la Jumuiya ya Ulaya ya Upasuaji wa Cranio-Maxillofacial; kwa kikundi cha Palio wa Mtakatifu Michele, kutoka Bastia Umbra; kwa askari waliofika kutoka Marche, Trani na Roma-Cecchignola; kwa Parokia ya Mtakatifu Salvatore huko Cava de' Tirreni, wakitumaini kwamba kukaa katika mji wa milele kutaimarisha dhamira ya kila mtu kwa mshikamano wa Kikristo, katika mazingira tofauti ambayo wanafanya kazi.”
Salamu kwa vijana wazee,wagonjwa na wenye ndoa wapya
Hatimaye, mawazo yangu yanawaendea vijana, wagonjwa, wazee na wenye ndoa wapya. Mwanzoni mwa mwaka mpya wa shule ninawaalika ninyi wapendwa vijana hasa wanafunzi wa Kristo Mfalme wa Roma mliopo hapa kuishi kujitolea kwa masomo kama fursa ya kukuza vipaji ambavyo Bwana amewakabidhi kwa ajili yenu mema yote. Bikira wa huzuni, ambaye tulimkumbuka katika liturujia siku chache zilizopita, awasaidie ninyi, wagonjwa wapendwa na wazee, kuelewa katika mateso na shida wito wa kufanya uwepo wa utume kwa wokovu wa kaka na dada zetu na kuwasaidia wapendwa wanandoa wapya, ..."kuna wengi leo, eh!," Papa alisisitiza na kwamba "kukubali kazi na misalaba ya kila siku kama fursa za ukuaji na utakaso wa upendo wako.”
Papa aomba tusali kwa ajili ya Palestina, Israel,Ukraine,Myana na penye vita
Baba Mtakatifu aidha amesema: “kaka na dada, tuombe amani: tusisahau kwamba vita ni kushindwa. Tusisahau Palestina, Israel, tusisahau Ukraine inayoteswa, Myanmar na sehemu nyingi zenye vita, vitambaya. Mungu atujalie sote moyo unaotafuta amani ili tushinde vita ambayo, ni kushindwa daima. Baraka yangu kwa wote!” Amehitimisha Papa.