Papa Francisko:ujumbe ni kwamba tunapaswa kubadilika na kuongoka!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 15 Septemba 2024, ametafakari Injili kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Akianza tafakari hiyo amesema: Injili ya Lirurujia ya siku inasimulia kuwa Yesu baada ya kuwauliza wafuasi wake kwamba watu walikuwa wanafikiria juu yake, aliwauliza moja kwa mjha wao: “Lakini ninyi mwasema mimi ni nani(Mk 8,29). Petro alijibu kwa niaba ya kundi zima akisema: “Wewe ni Kristo (Mk 8,30), yaani Masiha. Baba Mtakatifu ameongeza kusema: “pamoja hayo Yesu alipoanza kuzungumzia juu ya mateso na kifo kilichokuwa kikimsubiri, Petro mwenyewe alipinga, na Yesu alimkemea kwa ukali: “Nenda nyuma yangu, Shetani!, alimwambia kuwa ni shetani, kwa maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”(Mk 8,33).
Kwa kutazama tabia ya Petro tujiulize
Kwa kutazama tabia hii ya Mtume Petro tunaweza hata sisi kujiuliza swali juu ya nini maana kweli ya kumjua Yesu.” Kiukweli, Papa ameongeza, kwa upande wa Petro alijibu kwa uhakika kabisa akimwambia Yesu kuwa ni Kristo. Pamoja hayo, nyuma ya maneno hayo bado kuna namna ya kuwaza “kwa namna ya wanadamu, kwa akili ambayo inafikiri Mwalimu wa nguvu, masiha mshindi, ambaye hawezi kuteseka au kufa. Kwa njia hiyo basi, maneno ambayo Petro alijibu ni haki, lakini namna ya kuwaza haikubadilika. Yeye bado anapaswa kubadilisha akili, bado anapaswa kuongoka. Baba Mtakatifu alisisitiza tena “huo ndiyo ujumbe muhimu hata kwetu sisi. Kwa hakika hata sisi tulijifunza kitu juu ya Mungu, tunajua mafundisho, tunasali sala kwa namna ya kweli. Na labda swali la “Yesu ni nani kwangu?”, tunajibu vizuri, kwa kutumia baadhi ya mitindo tuliyo jifunza katika Katekesimu.
Lakini je tuna uhakika kwamba hiyo ndiyo maana ya kumjua Yesu kweli? Kwa uhalisia, ili kumjua Bwana haitoshi kujua kitu kutoka kwake, lakini inahitaji kujiweka katika ufuasi, kujiachia uguswe, na kubadilishwa na Injili yake. Hii ndiyo hasa uhusiano na Yesu, Mimi siwezi kujua mambo mwengi juu ya Yesu, kama sijakutana naye, ba bado mimi najua Yesu ni Nani? Mkutano unahitajika. Mkutano ambao unakubadilisha maisha: unakubadili namna ya kuwa, unakubadili namna ya kufikiria, mahusiano uliyo nayo na ndugu, uwezekano wako wa ukaribisha na kusamehe na chaguzi unazofanya katika maisha. Katika swali hili. Hayo yote hubadili ikiwa kweli umemjua Yesu! Kila kitu hubadilika. Baba Mtakatifu akiendelea amekazia kusema kwa kaka na dada waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwamba: “mtaalimungu na mchungaji wa kilutheri, Bonhoeffer, mwathirika wa chuki za kinazi, aliandika kuwa: “tatizo ambalo kamwe haliniachi na utulivu ni lile la kujua kwamba ni nini maana ya ukristo kwetu sisi leo hii kweli au hata Kristo ni nani.”
Askofu wa Roma aliongeza: “kwa bahati mbaya walio wengi hawajiulizi tena swali hilo na wanabaki watulivu, hata kuwa mbali na Mungu. Kinyume chake ni mihimu kujiuliza: mimi ninaacha kuangaishwa, ninajiuliza Yesu ni nani kwangu na ni nafasi gani aliyonayo katika maisha yangu? Ninamfuata Yesu kwa maneno tu, ninaendelea kuwa na mawazo ya kiulimwengu au ninajiweka katika ufuasi wake, kwa kuacha mkutano na Yeye ubadili maisha yangu? Atusaidie Maria Mtakatifu ambaye alikuwa anamfaamu vizuri Yesu na aliruhusu Mungu, abadili mipango yake na kumfuata Yesu hadi Msalabani,” Papa amehitimisha.